Saturday, June 9, 2012

SHANGAZI KATILI



Mtoto Aneth Joackim.
-Amharibu kwa maziwa mtoto huyu
MAMA mmoja aliyetajwa kwa jina Magreth Hallal, mkazi wa Tegeta Wilaya ya Kinondoni amefikishwa Kituo cha Polisi cha Tegeta akidaiwa kumfanyia ukatili kwa kumuunguza mtoto kwa maziwa ya moto na kumsababishia maumivu makali.
Akizungumza, mtoto huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Aneth Joackim (7) alidai kuwa alipigwa na Magreth ambaye ni shangazi yake, kisha kusukumwa ambapo aliangukia sufuria iliyokuwa na maziwa yaliyokuwa yamecheshwa, hivyo kuungua usoni.
Alidai kuwa baada ya kufanyiwa kitendo hicho cha kikatili, shangazi yake huyo hakuweza kuchukua hatua zozote za kitabibu na badala yake alimpiga marufuku kutoka ndani kwenda nje.
Hata hivyo, chanzo chetu cha habari kilisema kuwa mtoto huyo alipigwa na kusukumwa Mei 22, mwaka huu na akagundulika na mjumbe wa shina namba 20 wa eneo hilo, Amos Mkama Chuma, hivyo kwa kushirikiana na wananchi wakampeleka zahanati ya serikali iliyoko Tegeta jijini Dar es Salaam Mei 26, jeraha likiwa katika hali mbaya.
Mwandishi wetu alipozungumza na mjumbe huyo, alisema walikwenda kumshitaki mama huyo polisi Tegeta na akafunguliwa jalada namba TGT/RB/1621/2012 Kujeruhi.
“Mtoto ameungua sehemu za shavu na jicho, lengo letu ni kuhakikisha mgonjwa anatibiwa lakini pia aliyefanya kitendo hiki achukuliwe hatua za kisheria kwa sababu tunajiuliza, kwa nini hakumpeleka hospitali baada ya tukio?” alisema Chuma.
HOT POT lilimtafuta mtuhumiwa Magreth na alipohojiwa kuhusu madai hayo alisema ilikuwa ni bahati mbaya tu, alipoulizwa kisa cha kutompeleka hospitali alisema anamiliki duka la dawa hivyo alikuwa akichukua dawa na kumtibia nyumbani.
Naye Waziri wa Wanawake, Jinsia na Watoto, Sofia Simba ambaye ana dhamana ya watoto, alipozungumza mwishoni mwa wiki kuhusiana na sakata hilo, alisema hana taarifa lakini atalifanyia kazi.
“Ni kosa kubwa sana kumnyanyasa mtoto, nitafuatilia,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...