Sunday, June 10, 2012

ANUMBA FEKI, LULU FEKI WAZUA GUMZO...



Jambo limezua jambo mjini! Siku chache baada ya kifo cha aliyekuwa mwigizaji nguli, Steven Charles Kanumba ‘The Great’ huku mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’ akiwa nyuma ya nondo za Segerea, Dar kuhusiana na kifo hicho, mtaani wameibuka watu wawili wanaofanana na mastaa hao na kusababisha gumzo kubwa...
Taarifa zilizotua kwenye dawati hivi karibuni zilieleza kuwa kuna binti aliyetajwa kwa jina la Yolanda Michael (Lulu fotokopi, pichani), mkazi wa Tip Top jijini Dar ambaye amefanana na Lulu  na amekuwa akipata wakati mgumu anapokatiza mitaani akihisiwa ni Lulu halisi.
Wakati Yolanda akiendelea kuzua gumzo, Tadei Pius (Kanumba fotokopi), naye mkazi wa Dar amekuwa akileta songombingo la aina yake kwa mashabiki wa marehemu Kanumba ambao wakimuona hudai kuwa kumbe The Great hajafa kutokana na kufanana kwao.
Mwanzoni Risasi Jumamosi halikuamini maneno ya mitaani, hivyo kwa nyakati tofauti, mapaparazi wetu waliwatafuta watu hao na kuwaweka kwenye mizani ambapo picha zao zilibainisha kufanana kwa asilimia nyingi (tazama ukurasa wa mbele).

BOFYA HAPA KUMSIKIA YOLANDA!
Akihojiwa ‘exclusively’ na mapaparazi wetu, Yolanda, binti wa miaka 18 aliweka wazi kuwa mara kadhaa amenusurika vipigo kutoka kwa watu ambao walitaka kumuadabisha wakidai kuwa yeye ni Lulu (Elizaberth Michael) wakimtuhumu kwa kifo cha Kanumba.
“Kama mtakumbuka siku ya mazishi ya Kanumba kuna msichana aliyenusurika kichapo, basi ni mimi na siyo siku hiyo tu, hakuna kipindi cha maisha yangu ambacho niliishi kwa tabu kama baada ya kifo cha Kanumba,” alisema Yolanda mwenye ndoto ya kuwa mwigizaji mkubwa.
Mbali na kufanana umbile, pia Yolanda anafanana na Lulu orijino kuanzia pua, macho, midomo na sehemu mbalimbali za mwili.

MAJINA YA BABA ZAO
Pia, jina la baba yake ni Michael kama lilivyo la baba wa Lulu orijino (Michael).

HEBU MSIKIE KANUMBA FOTOKOPI
Akizungumza na paparazi wetu, Thadei Pius Michael (jina kama la baba Lulu na Yolanda), ambaye ukimuoana huulizi kwa jinsi alivyofanana na marehemu Kanumba, amekuwa akipata wakati mgumu kwa watu wanaopita katika eneo lake la kazi ya ufundi gereji.
“Hata kabla ya kifo cha Kanumba, watu wengi walikuwa wakiniambia kwamba wakidhani ni Kanumba waliponiona,” alisema kijana huyo mpole anapozungumza na kuongeza:
“Baada ya kifo cha Kanumba ndiyo hali imekuwa mbaya zaidi kwani watu wakiniona wanadhani ni mzimu wa marehemu Kanumba.
“Wengine wamekuwa wakinizunguka na kunikagua kwa kunitazama hali ambayo inanikosesha amani.”
Baadhi ya wananchi, walidai walishindwa kuamini kutokana na jamaa alivyofanana na The Great kuanzia midomo, macho, pua, urefu na baadhi ya sehemu nyingine za mwili.

“Ama kweli duniani wawiliwawili, najua Mungu ana makusudi yake kwa sababu haiwezekani wakafanana kwa kiasi hiki,” alisema Dullah, mkazi wa Dar.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...