Sunday, November 27, 2011

MAHABA: Sifa za MPENZI wa KWELI



1- Mpenzi/rafiki wa kweli ni yule ambaye hatangoja kujua nini unahitaji yaani hana sababu ya kusubiri kuombwa ndiyo asaidie au atoe. 

2 - Ni yule atakayejua wakati gani huna furaha au una furaha na atakuwa na wewe kwa hali zote mbili .

3 - Ni yule atayekuwa tayari kukusikiliza kwa kile utakachosema, hatojali umeongea baya au zuri .

4 -Atakuwa na wewe wakati wa shida na raha. Hatakuacha mtu wa kuvizia vizia na kujisogeza wakati ukiwa na raha.

5 – Mpenzi/rafiki wa kweli atakuheshimu na hatopenda kuwa nyuma na kukuacha bila msaada .

6 – Mpenzi/rafiki wa kweli ni yule atakayekupenda kwa moyo wake wote na wala si kwa ajili ya shinikizo fulani (pesa au mali)

7 – Mpenzi/rafiki wa kweli ni yule atakayeonyesha kuthamini nafasi yako kama rafiki au mpenzi mbele ya wengine

8 - Kwenye ukweli mpenzi mzuri atasema bila kukuficha na atapenda kukuonyesha mifano ya namna ya kuwa mkweli .

9 -Mpenzi/rafiki wa kweli ni yule anayejiamini, asiyeyumba katika maamuzi hata kama atalazimika kufanya maamuzi magumu .

10 - Atakuwa tayari kuvumilia hatakuwa mwepesi wa hasira wala kutumia lugha chafu au ubabe. Ni hayo tu jipeme na umpime umpendaye!

FABOLOUS, INTER COLLEGE BASH ILIVYOBAMBA!!!


                                   Fabolous akifanya makamuzi.
..Sehemu ya nyomi iliyohudhuria


Juma Nature na kundi lake la Wanaume Halisi.


SHOO ya Inter College Bash iliyokuwa inahusisha vichwa makini kutoka nchini Marekani na hapa Bongo, usiku wa kuamkia leo ilifana vilivyo katika viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo Fabolous aliweza kupiga shoo iliyochukua zaidi ya dakika 30 wakati wazawa wakitumia zaidi ya saa nane. Mbali na Fabolous ambaye ilikuwa kawaida kwake kufanya vizuri, wasanii wa Bongo waliosisimua mioyo ya mashabiki wao ni Juma Kassim ‘Juma Nature’ na kundi zima la Wanaume Halisi, Seleman Msindi ‘Afande Sele’, Wanaume Family, Haroun Kahena ‘Inspector Haroun’ akiongoza kundi zima la Gangwe Mob. Wengine ni Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’, Jay More, Nako 2 Nako, Joe Makini , Niki wa Pili, Elias Barnaba, Manzese Crew, Kikosi cha Mizinga kikiongozwa na Kala Pina na THT Dances.
Selemani Msindi 'Afande Sele' akiwa kazini.


Kiongozi wa kundi la Gangwe Mob Haroun Kahena ‘Inspector Haroon’ (kushoto), akionyesha uwezo wa kundi hilo na mwenzake Luteni Kalama.


Naseeb Abdul ‘Diamond’ akiwajibika.


Msanii wa muziki wa kizazi kipya Bongo ‘Hamisi Mwijuma ‘Mwana FA’ (kulia), akitoa burudani na msanii mwenzake, Shetta.


Joe Makini naye hakuwa nyuma kutoa burudani.

Comedy ZONE


Jamaa aliona hana kazi offisini hivyo akaamua ampigie simu secretary ili amzingue... Kwa bahati mbaya alikosea na kumpigia simu bosi wake....

Jamaa: "Oya we mpuuzi lete chai vikombe viwili haraka mezani kwangu na chapati 3..!!!"
Bosi: "Hivi unajua unaongea na nani??!"

Jamaa baada ya kugundua kampigia bosi wake akaa kimya....
Bosi: "Nauliza hivi... Unajua unaongea na nani??!"

Jamaa (Kwa kuzuga ikabidi tu ajibu...): "Hapana..."
Bosi: "Mimi ni bosi wako humu ndani..."

Jamaa (Akakaza sauti na yeye): "Hivi na wewe unajua unaongea na nai??!"
Bosi: "Hapana, nani wewe?!"

Jamaa(Kwafuraha zaidi): "Daaaaah, asante MUNGU!!!!"
Then akakata simu!!!!!

VINEGA NAO WAFANYA KUFURU DAR...



Wasanii wa kizazi kipya waliowahi kutamba zamani waliounda kundi la Vinega wakiongozwa na Mkurugenzi wa Deiwaka Entertainment, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (pichani juu) usiku wa kuamkia leo wamefanya onesho lililohudhuriwa na maelfu ya watu katika Viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam. Yafuatayo ni baadhi ya matukio yaliyojiri kiwanjani hapo:.
...sehemu ya yomi iliyokuwepo
Mwekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Freeman Mbowe, akiwapa hai, mashabiki kabla ya kuanza kuchana mistari.
Sister P akikamua.
...Zay B jukwaani
..Daz baba na makamuzi yake
Dj Sox wa Mabaga Fresh
Mkoloni akiwajibika
Mkoloni akiwajibika
Mr. Simple, ambaye pia ni Diwani kwa tiketi ya Chadema
...Kinadada wakifuatilia makamuzi
...Mashabiki wakiwa na mzuka
...Sugu anapoweka pembeni uheshimiwa na kukamata Mic
Dada wa kitasha akiserebuka baada ya kunogewa na bongo flava

Wednesday, November 23, 2011

MAHABA: JINSI YA KUMTAMBUA MWANAMKE ANAYEKARIBIA KUKUACHA!


Kuna tofauti kubwa ya kimaamuzi kati ya mwanaume na mwanamke kwenye suala la kuachana. Inaelezwa kwamba, wanaume ni rahisi kwao kuamua ndani ya dakika moja na kutangaza kuvunja uhusiano, lakini kwa wanawake maamuzi yao mara nyingi hutanguliwa na dalili, ingawa hata wanaume nao wanazo.

Uchunguzi unaonesha kuwa, wanawake wengi hawawezi kuficha sana hisia zao za mapenzi, lakini pia kwenye chuki hawakujaaliwa uvumilivu. Wanasaikolojia wanakiri kwamba, kutambua mawazo yaliyomo ndani ya mwanamke kwa kumtazama muonekano wake usoni ni rahisi kuliko mwanaume ambaye anatajwa kuwa na uwezo kuficha mawazo yake.

Muongozo huo wa kitaalamu wa kumtambua mwanamke anayekaribia kukuacha ni kazi rahisi, ambayo inaweza kuanzia kwenye kona ya mazoea ya tabia zake za kila siku kwenye uhusiano wa kimapenzi. Ni imani yangu kuwa kila mwanaume anamfahamu mpenzi wake katika sura mbili za chuki na furaha yake.

Atakuwa mwanaume wa ajabu ambaye atarudi nyumbani kwake na kushindwa kusoma sura ya mkewe na kujua kama ana furaha au amekwazika.
Ninapotazama uwezekano rahisi wa kumtambua mwanamke, nafika mahali pa kuamini kuwa dokezo chache nitakazotoa hapa chini zinaweza kuwa msaada kwa wanaume wengi kujua kama wamekaribia kuwekwa kando kimapenzi.

KUPENDA KUJITENGA
Mwanamke ambaye anapenda kujitenga na mpenzi wake atakuwa kwenye hatua za awali za kuelekea kuachana naye. Tabia ya mwanamke kutopenda kukaa karibu na mumewe au mpenzi wake inatajwa kama ishara ya kuchoka au kukinai penzi. Hoja inabaki pale niliposema pa yeye kushindwa kuamua haraka na hivyo kutengeneza kwanza hali ya kumpuuza mpenzi wake.

KUPOTEZA HAMU YA TENDO
Mwanamke ambaye hafurahii tendo la ndoa kwa mumewe au mpenzi wake yuko kwenye hatua za kuacha. Mara zote msisimko wa kimapenzi huashiria utoshelevu wa kihisia ambao ndiyo unaoelezwa kuwa ni muhimu kwenye uhusiano wa kimapenzi kuliko kitu kingine chochote.
Hii ina maana kwamba, mwanamke anayetosheka na kuvutiwa na mwanaume aliyenaye hawezi kukosa hisia za kimapenzi hasa anapokuwa na mwenza wake faragha.

KUPENDA KUKOSOA
Kama nilivyosema, kujua historia ya penzi lenu namna lilivyoanza ni jambo muhimu kwa sababu husaidia kujua kama kuna mabadiliko hatari ya tabia za mwanamke.
Ikitokea mpenzi wako ambaye hapo mwanzo alikuwa msikivu na ghafla ukaanza kuona amekuwa mkosaji na mpingaji wa mwenendo wako au kila unachofikiria kukifanya, tambua kuwa hiyo ni ishara kuwa amechoka kilichobaki ni nafasi ya kukuacha.

UHUSIANO NA MTU MWINGINE
Licha ya kwamba usaliti kwenye uhusiano limekuwa suala la kawaida siku hizi, lakini mwanamke ambaye atakuwa hafichi uhusiano wake wa pembeni na kuacha minong’ono ikikufikia huku yeye akionesha kutojali malalamiko yako ya kusalitiwa, ujue hiyo ni ishara kwamba mwanaume wa pembeni amemfikisha kwenye hitaji la moyo wake na hivyo kuachana na wewe si jambo la gharama kwake.

KUTOKUKUTEGEMEA
Mwanamke ambaye ana kusudio la kukuacha huanza kwa kuuondoa utegemezi. Ikiwa alikuwa anakuomba nauli, fedha ya matumizi, ada na huduma nyingine atasitisha bila kukuambia na bado utaona anaendelea kujimudu kama kawaida au kuteseka kimya kimya. Kuacha kukutegemea kama zamani ni dalili za kuweza kuishi bila wewe na hivyo kutafsiri uwezekano wa kukuacha wakati wowote.

MAISHA: Nguvu tano muhimu kwa mwanadamu kuwa nazo



Wengi wetu tuna ndoto za kuwa watu wenye nguvu katika jamii tunazoishi. Kama ukifanya uchunguzi kwa watu kumi tu waliopo karibu yako utagundua kuwa wanapenda kupata uwezo zaidi ya ule waliona sasa, kitakachowatofautisha ni aina za uwezo wanaouhitaji katika maisha yao. Wapo wenye kutamani kuwa wacheza mpira zaidi ya uwezo walionao, wapiganaji mahiri, matajiri, wasomi na wasanii maarufu.


Kimsingi kila mmoja anahitaji kuwa zaidi ya alivyo sasa, kwa vile mabadiliko hasa ya kimafanikio ndiyo jicho la kila mmoja wetu. Lakini swali gumu linalowashinda wengi kufanikisha tamaa za kuwa na nguvu au uwezo kwenye jamii zao ni jinsi ya kufanya ili wawe kama watakavyo. 



Kama nilivyotaja awali kwamba kuna nguvu za aina nyingi miongoni mwa wanadamu, lakini nguvu tano tunazokwenda kuziangalia ni muhimu kwa mwanadamu kuwa nazo na zinaweza pia kutumika kama njia ya kupata nguvu nyingine zaidi.



Tuanze kwa kuangali nguvu ya kwanza iitwayo The power influencing others au nguvu ya USHAWISHI. 

Katika jamii yetu kuna watu hodari sana kushawishi wenzao, wagome, wafanye uasi waibe, waue na hata wasome kwa bidii. Hata kwenye siasa ili mtu akubalike zaidi anatakiwa kuwa na nguvu hii.



Aina nyingine inaitwa nguvu ya MAPENZI The power of love. Kuna watu hawana pesa kabisa, lakini wana nguvu ya kupendwa, kila wakiingia mahali wanakuwa nyota, wanawavutia wengi. Hivyo ni jukumu la binadamu kuhakikisha kuwa anapata nguvu hii pia na kuitumia katika maisha yake.



Nyingine ni ya UFAHAMU The power of Knowledge, hii inatokana na ufahamu wa mtu juu ya mambo yakiwemo masomo. Katika familia na jamii tunaona kuna watu ambao huaminiwa na wengi na kuwa vinara wa kuulizwa juu ya ufumbuzi wa matatizo au vitu fulani kwa vile wanajua mambo mengi yahusuyo maisha. 



Nguvu nyingine ni ile ya JAMII, Social Power. Bila shaka tumepata kusikia jamii ikisimama na kumtetea mtu kwa maandamano hata kama mwenyewe yuko kifungoni. Nguvu hii inategemea wingi wa marafiki zako kwenye jamii unayoishi. Nyingine ni ya UJUZI ‘Skill power’. Wengi wetu tunakuwa wanyonge kimaisha na kushindwa katika mengi kwa sababu hatuna nguvu hii inayoweza kutupa nafasi ya kukabiliana na maisha, ndiyo maana tumesikia wenzetu wakiamua kujiua pale tu walipokutana na ugumu au kikwazo kidogo cha kimaisha.



Kitaalamu ipo pia nguvu ya MAFANIKIO, The power of Success. Unapokuwa unapata mafanikio zaidi katika maisha yako unakuwa na nguvu ndani ya jamii yako kwa vile wengi watakutazama wewe kama mfano wa mafaniko na hivyo kujipatia wafuasi watakao kuwa nyuma yako. 



Baada ya kutoa mifano hiyo michache ya nguvu ambayo wengi wetu tunapenda kuipata kwenye jamii zetu nitakuwa nimebakiza jibu la swali UNAWEZAJE KUWA MWENYE NGUVU KATIKA JAMII? 



Siri ya kuwa mwenye nguvu katika jamii ni moja tu nayo ni kufanya vitu kwa nguvu, usahihi na umakini mkubwa, ili wengine wakuamini bila kukutilia shaka yoyote. Jibu hili halitofautishi aina ya nguvu tulizozitaja au zile ambazo hatukuzigusia katika somo hili.



Tatizo kubwa miongoni mwa wengi ni kutaka kuwa na nguvu bila kutenda mambo kwa usahihi. Tufahamu kuwa ukitaka kuwa na ushawishi lazima watu wakuamini, ili wakupende unatakiwa kuishi kwa wema, uwe na marafiki lazima uwavutie kwa tabia zako, uwe mwanajamii kwa kujitolea, ujuzi utafute kwa kusoma na kujifunza kila siku, mafaniko yatafute kwa bidii sana bila kuchoka. JAMII IKIKUAMINI KWA MATENDO YAKO, UTAKUWA NA NGUVU. 

Tuesday, November 22, 2011

DUNIA IMEKWISHA: Binti abakwa na baba yake kwa miaka 13 mfululizo...





Mtuhumiwa ambaye ni baba mzazi wa binti huyo, bwana Muzamil Said.
KUNA watu wanasema dunia imevaa sketi ndiyo maana wanaotakiwa kujenga ndiyo hao hao waharibifu. Baba bila soni, kavua nguo mbele ya mwanaye wa kike, akambaka. Hakukoma, akaendelea tena na tena.

Ni madai mazito yaliyopo polisi. Binti mwenye umri wa miaka 16 (jina tunalo), anamtuhumu baba yake mzazi, Muzamil Said kwa kumbaka mfululizo.

Shauri lipo Kituo cha Polisi Mbagala, jalada lina kumbukumbu namba MBL/RB/10719/2011 KOSA LA KUBAKA.
Kwa mujibu wa binti huyo, baba yake alianza kumbaka tangu akiwa na kadirio la miaka mitatu mpaka mwaka huu mchezo huo ulipobainika. Kwa hesabu hizo, ni wazi alitendwa ukatili huo kwa miaka 13.

MCHEZO ULIVYOANZA
Binti huyo, anaishi na baba yake Mbagala, eneo la Nzasa B, anasimulia: “Nakumbuka nilikuwa kama na miaka mitatu hivi, baba na mama yangu mzazi walitengana. Tangu wakati huo, sijamuona tena mama yangu kwa maana aliondoka moja kwa moja.

“Baada ya hapo tulianza kuishi wawili, mimi na baba tu. Ni kipindi hicho baba alianza kunibaka, nilikuwa napata maumivu makali lakini yeye aliendelea. Ikafikia hatua nikawa siwezi hata kuzuia mkojo. Nikibanwa tu najikojolea.
Binti ambaye amekuwa akibakwa na baba yake kwa takribani miaka 13.
“Ikafika kipindi, baba akamtafuta mama mwingine (mama wa kambo), tukawa tunaishi wote lakini mara kwa mara usiku baba alimtoroka huyo mama na kuja kunibaka.

“Mwezi huu ndiyo mama aligundua, kwani kama kawaida yake, baba alimtoroka na kuja kulala kwangu. Baadaye mama alikuja kimya kimya na kumkuta akiwa ananibaka. Mama akamgombeza baba kwa kilugha.

“Mama akaniuliza ile tabia imeanza lini? Nikamueleza kila kitu. Nikamfafanulia na jinsi nilivyo na tatizo la kutokwa na mkojo. Mwanzoni baba aliniambia eti akiniingilia mara kwa mara tatizo la mkojo litaisha lakini nimebaini kuwa si kweli, kwani linaendelea mpaka leo.

“Nilikuwa nasoma Shule ya Msingi (jina kapuni), darasa la tano lakini nimeacha kwa sababu sipo sawa. Tatizo la kukojoa linaendelea na akili yangu pia imevurugika.”

KAULI YA MWENYE NYUMBA
Alhaj Abdilah Mohamed Mwahu ndiye mwenye nyumba wa Muzamil na hili ni neno lake: “Huyo binti alikuja kunilalamikia, ikabidi niwashirikishe wapangaji wengine, mwisho tukakubaliana tumuokoe binti kwa kulifikisha suala lake kwenye vyombo vya sheria.

“Tulianzia serikali za mitaa kabla ya kupeleka shauri Kituo cha Polisi Mbagala. Polisi walimkamata lakini akaachiwa kwa dhamana, na sasa hatujui alipo.”

SERIKALI YA MTAA, NZASA B
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Nzasa B, Jeruin Mkude alisema: “Suala hilo lipo lakini polisi hawanipi ushirikiano.”
UTAMU imebaini kuwa, shauri la Muzamil limeganda polisi, kwani tangu baba huyo alipopewa dhamana, mpaka sasa hajarudi kuripoti na hajulikani alipo.

Comedy ZONE


Tangazo kwa wachaga wote. 


Chuo kipya kabisa cha kichaga (CHAGGA TECHNICAL COLLEGE) kinatangaza kozi mpya kwa mwaka wa masomo 2011/2012 kama ifuatavyo..
1.) UBAHILI Miezi 3.
2.) ULEVI miezi 2. 
3.) KUUZA DUKA mwezi 1. 
4.) KUACHA WAKE VIJIJINI miezi 4.
5.) KUENDESHA PIKIPIKI wiki 2. 
6.) KUSOGEZA MIPAKA YA SHAMBA LA JIRANI miezi 6.
7.) UTAPELI wiki 2. 

Atakayejiunga mapema atapewa ofa kozi ya kupika mbege na kutembeza Ndizi BUREEE!!! Wahi nafasi ni chache... Nyote MNAKARIBISHWA!!!!

Monday, November 21, 2011

MAHABA: Penzi lenu halina amani kisa, simu zenu za mkononi?



Ni wiki nyingine tunakutana tena kupitia safu hii ambayo kimsingi tunakumbushana na kuelimishana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi. Naamini wewe msomaji wangu umzima bukheri wa afya na uko tayari kabisa kupitishia macho kile ambacho nimekuandalia kwa siku hii ya leo.
Mara kwa mara nimekuwa nikiandika makala zinazohusu 
tatizo la simu za mkononi kwa wapenzi kwani limekuwa ni kama wimbo wa taifa sasa. 

Tumekuwa tukishuhudia wapenzi wakiachana, walio katika ndoa wakitengana na wengine kukorofishana kila mara huku baadhi wakibaki katika uhusiano wa mashaka, chanzo kikiwa ni simu za mkononi.
Aidha, nimekuwa nikipokea simu nyingi sana kutoka kwa watu mbalimbali wakielezea namna ambavyo chombo hiki cha mawasiliano kimekuwa kikisababisha mtafaruku kati yao na wapenzi wao.

“Sina amani kaka yangu, mimi na mpenzi wangu tumekuwa ni watu wa kugombana kila wakati kwa sababu ya simu yangu ya mkononi, mara nyingi anahisi namsaliti na kila ninapoongea na simu anadhani naongea na wanaume zangu, naumia sana hadi wakati mwingine kuona bora nisiwe na simu kwani inaweza kusababisha nikaachana na mpenzi wangu wakati bado nampenda,”anaeleza Maria wa Dodoma.
Kwa kweli simu za mkononi kwasasa zimekuwa ni sumu katika uhusiano na hii inatokana na baadhi ya watu wasiowaaminifu kuzitumia katika kuwasaliti wapenzi wao.

Nilichodhamiria kukiandika wiki hii ni jinsi unavyoweza kumfanya mpenzi wako asihisi kwamba unamsaliti kwa kutumia simu yako ya mkononi. Nikuhakikishie tu kwamba, kwa kuzingatia haya nitakayoandika na kama mpenzi wako ni mtu mwenye uelewa mkubwa, simu zenu za mkononi haziwezi kuwaletea matatizo.
Kwanza, kama kweli wewe ni muaminifu kwa mpenzi wako unatakiwa kujiamini kila unapokuwa karibu naye na wala usioneshe kujishtukia. Wapo ambao kila wanapokuwa na wapenzi wao, wakipata sms tu, watajificha ili wasome haraka kisha wafute. Wakipigiwa wakiwa na wapenzi wao kama hamjui anayempigia basi atakata na kuizima kabisa. 

Hivi unapofanya hivyo unataka mpenzi wako akufikirieje? Utamjengea mazingira gani ili akuamini na kutohisi kuwa kuna mshikaji mwingine anakuzingua ama una uhusiano naye wa kimapenzi kwa siri? 
Kimsingi kujishtukia kwako pale unapokuwa na mpenzi wako kunaweza kukuharibia. Ndiyo maana nasema, kama kweli unampenda huyo uliyenaye usiweke mazingira ya usiri kwenye simu yako. Wakati mwingine kuwa tayari kumjibu pale atakapokuuliza ni nani aliyekupigia simu au ujumbe huo unatoka kwa nani. Siyo kila mara atakuuliza lakini pale atakapokuuliza mjibu.

Pili, unatakiwa kutambua kuwa wewe ni mpenzi/ mke au mume wa mtu. Hivyo basi siyo busara kujirahisi na kumpa kila mtu tena wa jinsia nyingine namba yako ya mkononi. Itoe kwa watu muhimu ambao hata siku wakija kukupigia simu ukiwa na mpenzi wako iwe rahisi kujieleza. 
Unaweza kumkuta msichana anakutana na mvulana na anatongozwa, awali anakataa lakini mwisho anaombwa namba yake ya simu na anaitoa. Utamuelewa vipi msichana kama huyu? Huyu ndiye wale nataka sitaki kama hujui. 

Hivi wewe huelewi kwamba wanaume wengi siku hizi wakishapata namba ya simu tu wameshamaliza kazi? Nasema wameshamaliza kazi kwa sababu ni wataalam wa kutongoza kupitia kwenye simu.
Sasa siku mtu kama huyo akikutumia ujumbe wa kimapenzi na mpenzi wako akauona utamwelezaje? Hawezi kukuelewa.
Tatu,unatakiwa kuwa makini sana na watu wanaokutaka kimapenzi. Hawa hata usipowapa namba yako ya simu wanaweza kufanya juhudi za kuipata kupitia kwa watu wako wa karibu. Kwa maana hiyo basi, wanaokusumbua ni vyema ukamweleza mpenzi wako. 

Hiyo itakusaidia! Lakini kama jamaa anakuimbisha kila unapokutana naye kisha unanyamaza, siku mpenzi wako atakapokuja kuwakuta sijui utamueleza nini akuelewe! Itakuwa ngumu.
Hata wewe mwanaume kama kuna mwanamke anakushobokea, mpe taarifa laazizi wako kwamba unajua demu fulani ananisumbua. Kimsingi usimfiche mpenzi wako katika kila jambo kwani waswahili wanasema, mficha maradhi kifo kitakuja kumuumbua!

Friday, November 18, 2011

Maajabu ya DUNIA: BINADAMU AGEUKA MTI




NI miujiza ya Mungu. Mitihani ipo kila kona kwa aina mbalimbali lakini hatutakiwi kukufuru. Tunapaswa kukubali matokeo na kuomba nusura kwa Muumba, kwani kazi yake haina makosa.

Binadamu ageuka mti! Unaweza kudhani ni simulizi ya miujiza lakini huo ndiyo ukweli. Ndugu yetu anayeitwa Dede Koswara, 41, raia wa Indonesia hivi sasa hatamaniki na wengi wanamwita ‘nusu mtu, nusu mti’.

Dede hajarogwa, isipokuwa amepata maradhi hayo baada ya kushambuliwa na virusi hatari wanaoitwa Human Papilloma (HPV), hivyo kubadili kabisa muonekano wake.


HALI HALISI YA DEDE
Alianza kushambuliwa na virusi hivyo akiwa na umri wa miaka 17, kwa maana hiyo ni tatizo ambalo ameishi nalo kwa miaka 24 sasa.

Ugonjwa ulianza kumshambulia kwenye mikono na miguu kabla ya kuhamia maeneo mengine ya mwili wake mpaka kichwani.
Tatizo ni kubwa kiasi kwamba vioteo vya upande wa mikono na miguu, vinashabihiana na miti mikavu, ubao mkavu ambao haujaondolewa magome yake.

Alishafanyiwa upasuaji mara tisa kuondoa tatizo hilo lakini mafanikio yakawa kupunguza kwa asilimia 95 kabla ya kuanza kuota tena.

Viotea ambavyo vinamfanya Dede aonekane kama mti, kitaalamu vinaitwa mapembe (cutaneous horns).
Hupatwa na maumivu makali kutokana na hali hiyo, hivyo kumfanya ashindwe kutembea au kufanya lolote lile.

Januari, 2008, akiwa na umri wa miaka 37, alifanyiwa upasuaji wa kwanza. Alipata nafuu na kueleza: “Namshukuru Mungu, angalau naweza hata kutembea.”

Alipopatwa na maradhi hayo, alikuwa anajishughulisha  na kazi za uvuvi lakini kwa sasa ameshindwa kumudu.

NGUMU KUPONA
Dk. Rachmad Dinata wa Hospitali ya Hasan Sadikin, Indonesia, amesema: “Hawezi kupona kwa asilimia 100 lakini maisha yake yanakuwa bora. Tumemtibu na kupunguza ukali wa ugonjwa, alikuwa anategemea watu kumfanyia kila kitu lakini sasa anaweza kula yeye mwenyewe, kuandika na kutumia simu ya mkononi.”

Dk. Anthony Gaspari, raia wa Marekani anayetokea Chuo Kikuu cha Maryland, amejitolea kufanya utafiti kubaini tiba kamili ya ugonjwa wa Dede. Taarifa yake ya awali, imeeleza kuwa virusi hao ambao ni adimu duniani, wamemfanya Muindonesia huyo aishiwe kabisa na kinga za mwili.

Dede ameweka tumaini lake kwa daktari huyo wa Marekani na ameeleza: “Naamini nitapona ila sijui lini. Kuna siku nitakutana na mwanamke na nitafunga naye ndoa. Natamani niwe baba wa familia na baadaye niwe na watoto. Napenda sana nibaki hai mpaka nitakapowaona wajukuu.”
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...