Tuesday, June 12, 2012

WABONGO WALA KICHAPO CHINA




HALI ya hatari imewazingira Watanzania walioko nchini China kwa biashara, baada ya Wachina kuanza tabia ya kuwadhulumu, kuwapiga na kuwapa mateso mbalimbali.
Habari kutoka China, zilizojazwa nyama kwa picha za matukio ya Wabongo wakiloa damu kwa kichapo, zinaeleza kwamba jamaa hao wamegeuka waonevu wa kiwango cha juu kwa Watanzania.
CHANZO CHA STORI
Mtanzania, Bicklen Nazaleno Kibiki alipewa kichapo na Wachina waliomvamia hoteli aliyofikia kwenye Jiji la Guangzhou.
Chanzo chetu kilisema: “Bila sababu, Wachina walimvamia huyu mwenzetu wakati anapandisha mizigo yake hotelini, wakampiga. Tulipompeleka Kibiki polisi kuripoti, tukageuziwa kibao, akaambiwa alipe faini.
“Kuna Mtanzania mwingine mbali na huyu Kibiki, yeye alipigwa barabarani baada ya kwenda polisi, akalipishwa faini, bahati nzuri Waafrika wenzetu kutoka Nigeria, waliungana na sisi, tukamsaidia akatoka, amesharudi Tanzania na hataki tena kurudi China.”
WACHINA BWANA!
Mtoa habari wetu alisema Wachina pia wamekuwa na tabia mbaya mno wanapokutana na Watanzania, akatoa mfano: “Mtanzania akienda saluni kunyoa, anaweza kuambiwa, mfano shilingi 10,000 lakini akishamaliza, anaambiwa shilingi 20,000.
“Hapo ni lazima ulipe hiyo pesa, vinginevyo utapigwa na ukienda polisi utageuziwa kibao. Hawa watu wakiwa kwao ni wakatili sana, lakini sisi kwetu tunaishi nao vizuri.”
USHUHUDA MWINGINE
Mtanzania Jas au maarufu kama Mchungaji ambaye kwa sasa yupo hapa nchini, alimueleza ripota wetu: “Nilikaa China kwa miezi minane nikiwa nafanya kazi zangu kwa usalama. Nilipokamilisha mizigo yangu wakati nataka kurudi Bongo nilivamiwa na Wachina.
“Ilikuwa hivi, wakati nashusha mizigo kwa kutumia toroli la Hoteli ya Dong Feng ambayo ndiyo nilikuwa naishi pale Guangzhou, alitokea Mchina akaanza kutupa mizigo yangu. Nikamuuliza kwa nini anafanya hivyo, akanijibu tenda ya kushusha mizigo hotelini ni yake, kwa hiyo lazima nimlipe pesa.
“Tukaanza kubishana, kwani siyo lazima kumlipa yeye pesa ukizingatia, nikitumia toroli la hoteli, silipii hata shilingi moja. Wakati tunabishana, wakatokea wenzake wakaanza kunipiga. Nikiwa nimejeruhiwa, tulikwenda hospitali, huko nikaambiwa nilipe faini vinginevyo viza yangu itafungwa.
“Ikabidi nitoe dola 600 (zaidi ya shilingi 900,000) kuwalipa wale Wachina. Hii ndiyo hali halisi, bila kutafuna maneno ni kwamba Wachina wakiwa kule kwao wanawatesa Watanzania na polisi wa kule muda wote wanawalinda.”

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...