Tuesday, June 12, 2012

Watoto waliovimba wapasuliwa



HATIMAYE watoto wawili wa Sophia Rashidi (22) ambao ni Omari Rashid (4) na Maulid wa miezi kumi, waliolazwa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wamefanyiwa upasuaji.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita hospitalini hapo, Sophia ambaye ni mkazi wa Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambaye habari zake ziliwahi kuandikwa na gazeti hili hivi karibuni, amesema anawashukuru wote walioguswa kwa namna moja au nyingine na matatizo ya watoto wake na kutoa michango ya hali na mali ili kunusuru maisha yao.

“Nikiri kuwa baada ya gazeti moja kuandika habari kuhusu mateso ya watoto wangu waliokimbiwa na baba yao, watu wengi wamejitokeza kuwasaidia, wengine wamenifungulia akaunti yenye jina la Sophia Rashid Luwingo namba acc/20910000481 NMB.

“Wamesema kwa kufanya hivyo nitasaidiwa zaidi. Naomba atakayependa kunisaidia atumie akaunti namba hiyo na sina cha kuwapa, thawabu atawapa Mungu mwenyewe,” alisema mama huyo na kuongeza kuwa watoto wake baada ya kufanyiwa upasuaji, wanaendelea vizuri.

Akizungumza na Afisa Ustawi wa Jamii wa Moi, Mary Ochieng alisema mama huyo amehamishiwa Wodi ya Makuti Muhimbili kutoka Moi baada ya upasuaji.

“Mimi pia nawashukuru waliosoma gazeti hilo na kumsaidia mama huyu. Sisi kama taasisi ya tiba tutawasaidia kimatibabu na kuhakikisha afya zao zinaimarika. Nawaomba watu waendelee kuwachangia kwa kuwa tatizo bado wanalo na hawana uwezo wowote,”alisema Ochieng.
Alibainisha misaada inayohitajika kuwa ni pamoja na chakula kwa watoto hao, nguo, fedha na baiskeli ya kumsaidia mama huyo kubebea watoto wake.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...