Saturday, June 9, 2012

MAHABA: Ukimya wako utakuongezea heshima ya ndoa



KAMA kawaida tumekutana katika kona yetu ya Mapenzi na Uhusiano ili kujuzana mawili matatu, leo nataka nilijibu swali la dada yangu mmoja ambaye amekuwa hana raha kutokana na hawala wa mumewe kumtumia ujumbe wa matusi kila kukicha, pia wengine wakifikia hatua ya kumtangazia kuwa wana ujauzito wa mumewe.
Amekuwa akikosa raha kila siku kutokana na vitimbi anavyofanyiwa na wanawake hao. Alichosema kila akimuuliza mumewe humwambia aachane nao lakini anachoshukuru upendo wa mumewe ambaye ni dereva wa pick- up upo vilevile.
Aliniomba ushauri kwani wanawake hao wamekuwa wakimkosesha amani ndani ya moyo wake.
Kwanza, nampa pole dada yangu kwa yote yaliyomsibu juu ya hao wanawake waliokosa heshima na kushindwa kujua thamani ya ndoa. Kabla sijamjibu, ningependa kuwahabarisha wanawake wote wanaoingilia uhusiano wa watu, wajaribu kuziheshimu ndoa za watu, si busara kumtukana mke wa mtu, jiulize kama ungekuwa wewe ungefanyaje?
Wengi wenu huwa hampendi ndoa na kutanguliza starehe mbele na kufanya mgeuzwe chombo cha starehe na si mwanamke wa kukaa na mumewe. Pia nataka nieleze kitu kimoja kwa muolewaji; ni kosa kubwa kujibizana au kutukanana na mtu aliye nje ya ndoa yako, ni kumpa kichwa na kuamini ameweza kukuchokoza na ukaguswa.
Niwape siri wote walio ndani ya ndoa wanaopata matatizo ya kusumbuliwa na hawala wa waume zao. Wachukulieni kama mbu walio nje ya chandarua wasio na uwezo wa kuwauma zaidi ya kupiga kelele.
Siku zote kelele za mbu hazikunyimi usingizi. Ushauri wangu kila anapotokea mtu wa kukutukana kwa vile tu wewe umeolewa na yeye kuachwa solemba, usijisumbue kwa lolote, jiepushe naye kwa kukaa kimya, usimjibu kwa vile wewe umeshapata.
Ukimya wako ni pigo zito kwake kuliko kutukanana. Muache abwabwaje mwisho wake atachoka, kama mbu nje ya chandarua.
Mwisho nazungumza na wanaume msiojua thamani ya mwanamke ndani ya ndoa. Ni kosa kubwa kumlinganisha mkeo na hawala, kufanya hivyo ni kumdhalilisha mkeo. Mkomeshe hawala yako ili amheshimu mkeo kwani kama yeye angekuwa bora, ungemuweka ndani.
Mwanaume mwenye tabia hizo ni zaidi ya mnyama, hafai kuwa baba wa familia. Kama ulikuwa bado una tamaa zako za mwili, kwa nini ulikimbilia kuoa? Mjengee heshima mkeo ambaye ana dhamana kubwa mbele ya Mungu.
Kwako wewe uliye nje ya ndoa, heshimu ndoa ya mwenzako, kuiba penzi si kibali cha kuingilia ndoa ya mtu, usiwe hayawani uliyekosa mkia.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...