Saturday, June 9, 2012

BONGO KIMENUKA




Mtuhumiwa wizi kwa kutumia mtandao mmoja wa simu za mikononi, Maenda akiwa mikononi mwa polisi. 

KIJANA mmoja aliyefahamika kwa jina la Maenda, juzikati alinaswa na polisi wa doria kwa madai ya kujaribu kujipatia fedha kwa njia ya wizi kwa kutumia mtandao mmoja wa simu za mikononi (jina tunalo).
Ishu hiyo ilijiri Mtaa wa Aggrey maeneo ya Msimbazi, jijini Dar kwenye duka linalouza simu za mikononi.
Kwa mujibu wa chanzo, Maenda alikuwa akijiandaa kupokea kiasi cha shilingi laki nane (800,000) kutoka kwa mke wa mmiliki wa duka hilo aitwaye Shadrack Chado, Mama Chado.
Akizungumza na gazeti hili, Chado alisema kuwa saa sita mchana siku ya tukio, simu yake ya mkononi ilipoteza mawasiliano ghafla ambapo kwenye skrini kulisomeka neno NO SERVICES.
Alisema baada ya muda mkewe alipigiwa simu kwa namba yake na mtu aliyeigiza sauti ya Chado.
Chado akaongeza: “Huyo mtu akamwambia mke wangu kuwa anamtuma fundi ampe shilingi lakini nane.
“Bahati mbaya sana siku za nyuma tuliwahi ‘kulizwa’ kwa mtindo huo. Kwa hiyo mke wangu akamjibu yule aliyepiga simu amtume huyo fundi fedha ipo, kisha akaniambia mimi ndiyo tukajipanga ili huyo mtu atakapokuja tumnase.”
Chado aliongeza kuwa baada ya muda kijana huyo alifika dukani hapo bila kufahamu kuwa Chado mwenyewe amejaa tele na anafahamu mchongo mzima.
Akasema mlango uligogwa na mgongaji alipoingia na kupokelewa na Mama Chado, alisema ametumwa kuchukua shilingi laki nane na mumewe.
Chado akaongeza kuwa kwa sababu polisi nao walikuwa ‘chobingo’ walitokea na kumkamata kijana huyo ambaye baada ya kupigwa maswali aliweka wazi kwamba katika mtandao wao wa wizi yupo mfanyakazi mmoja wa kampuni husika ya simu na rafiki wa karibu wa Chado aliyemtaja kwa jina la Ally ambaye naye anamiliki duka la simu.
Chado akamfafanua Ally hivi: “Ally ni rafiki yangu mkubwa, kumbe nd’o alikuwa akitumia ukaribu wetu kuratibu mpango wa kuniibia, amenisikitisha sana nilidhani rafiki kumbe adui.
“Walichotaka wao, kama wangefanikiwa kuchukua hizo fedha, baadaye simu yangu ingerejea katika mawasiliano kama kawaida.”
Aidha, polisi hao walimtia mbaroni Ally huku mfanyakazi wa kampuni hiyo ya simu akisakwa baada ya kutimka kufuatia kupata habari za ‘kubumburuka’ kwa dili hilo.
Tukio hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi, jijini Dar kwa kuandikiwa jarada No: MS/RB/6361/2012 ‘WIZI KWA NJIA YA MTANDAO’.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...