Tuesday, June 12, 2012

MAHABA: UNAWEZA KUMPENDA KABLA HUJAMUONA?!?



HAPA ndiyo sehemu pekee ya kupanua mawazo na kukuza ubongo wako juu ya mambo yanayohusu uhusiano na mapenzi. Kama ni mara yako ya kwanza kuanza kupitia ukurasa huu, umekutana na kona muhimu sana. Huna cha kupoteza. Utajengeka kila siku.

Rafiki zangu, leo nimekuja na mada mpya baada ya kuhitimisha ile ya wiki iliyopita. Nina imani kuna mengi mliyojifunza. Mada ya leo inatokana na maswali mengi ya aina moja niliyoyapata kwa muda mrefu kutoka kwa wasomaji mbalimbali.

Hebu msikie huyu: “Pole na kazi kaka Shaluwa, kuna kaka nawasiliana naye. Kiukweli tumezoeana sana, juzi hapa amesema eti ananipenda na anataka kunioa. Mimi nipo Mbeya, yeye anaishi Dar es Salaam.

“Hatujawahi kuonana, zaidi ya kuzungumza kwa njia ya simu tu. Nilifahamiana naye baada ya kukosea namba, ndipo tukakubaliana kuwa marafiki. Tafadhali naomba msaada wako maana ninachanganyikiwa kabisa. Ni kweli ananipenda?”. 

Kilio kama hicho nilikipata pia kutoka kwa msomaji mmoja ambaye naye sitachapa jina lake gazetini. Huyu alisema: “Nimekutana na rafiki kwenye Facebook, tunawasiliana mara kwa mara, ninahisi kumpenda huyo msichana. Naye ana kila dalili za kunipenda, tatizo sijaanza tu kumweleza. Hivi, inawezekana kweli tukapendana kabla ya kuonana?”

Bila shaka kuna picha umeipata kupitia maswali ya wasomaji hao wawili. Niliwaahidi kuandika mada ambapo ndipo wangepata majibu yao. Je, wewe upo kwenye kundi gani?
Umewahi kukutana na jambo hilo? Unadhani unaweza kumpenda mtu kabla ya kukutana naye? Sauti pekee inaweza kumfanya mtu ampende mwenzake kwa dhati na mapenzi yao yakadumu? Twende tukajifunze.
INAWEZEKANA?
Hili ni jambo la kwanza linalotakiwa kupatiwa majibu kabla ya kuendelea na mada hii. Huu ni mtazamo hasi. Jibu kwa kifupi tu ni haiwezekani. Utawezaje kumpenda mtu ambaye hujamuona?
Misingi ya kumpenda mwingine ikoje? Kanuni zipo wazi; KUPENDA ndiyo jambo la kwanza, ambapo ukweli ni kwamba huanza na kutamani, sasa itawezekanaje kumtamani mtu ambaye hujawahi kukutana naye?
Baada ya kupenda, kuna mambo mengine ya msingi ambayo ni muhimu kuzingatiwa ili kujihakikishia kwamba uliyempata ni mwenzi sahihi. Kuna suala la kuchunguzana tabia n.k, yote haya yatawezekana vipi kufanyika kabla ya kukutana?
Najua ni wengi wamekumbana na hili ninalolizungumzia hapa, unashindwa cha kufanya na kubaki gizani. Leo utarudi kwenye mwanga! Unajua chanzo cha yote hayo ni nini? Twende kwenye kipengele kinachofuata.
HUANZA HIVI...
Chanzo kikuu cha udanganyifu huu wa mapenzi huwa ni vyombo vya mawasiliano. Mfano mtu amepiga simu amekosea namba...mara anaanza ‘uko wapi? Haina neno, tunaweza kuwa marafiki?’
Mazoea yakizidi, kila mmoja huanza kumwuliza mwenzake vitu anavyopendelea na mambo mengine. Baadaye wanatongozana! Huelezana mambo mengi sana na ahadi nyingi wakiamini kwamba wanapendana kwa dhati!
MAPENZI YA HISIA
Kimsingi sababu ya haya yote ni hisia tu. Njia ya mawasiliano inaweza kukoleza au kuimarisha uhusiano ambao tayari upo. Mfano kama unaishi Moshi na mpenzi wako yupo Mwanza, mnaweza kuboresha uhusiano wenu kwa kuwasiliana kwa njia ya simu, waraka pepe na mitandao ya kijamii.
Kinachotokea kwa marafiki wapya ambao wanahisi tayari ni wapenzi na wanapendana ni zile hisia za ndani zinazowaingia wakati wa mawasiliano yao. Pengine walianza kuzungumzia mambo ya mapenzi na kujikuta wakitamani kuwa karibu.
Jambo kubwa zaidi ni kwamba mhusika hutawaliwa zaidi na hisia, maana kwa sababu hawafahamiani, watakuwa wanauliza; ‘Wewe ukoje? Mrefu, mfupi, mwembamba, mnene au?’ halafu mwenzake atamjibu, ‘mrefu kiasi, si mnene sana, kifupi nina umbo namba nane...navutia na ni maji ya kunde’.
Kifupi mtu anaweza kujielezea vyovyote atakavyo, hivyo kumfanya mwenzake amtengeneze ajuavyo kichwani mwake na kujihakikishia kwamba anampenda kwa dhati mwenzake kumbe anajidanganya!
TABIA BANDIA
Mbaya zaidi ni kwamba, wakati wapenzi hawa wanaojidanganya wakiendelea kuwasiliana si rahisi kujuana vizuri kitabia kwa sababu wengi huonesha tabia bandia. Mambo yao ya ndani wanayaficha kwa nguvu na kuonesha mema tu.
Hapo ndipo mwanzo wa penzi feki kwa kudanganyika na tabia za kutengeneza.
HULKA MBAYA
Kuna wengine ni tabia zao za asili. Amezoea kupata wapenzi kwa kupitia kwenye simu na mitandao ya kijamii. Usishangae kuna wengine wanapiga namba hata wasizozijua, akikutana na mtu wa jinsia tofauti na yake, anaanza mambo yake. Akimaliza haja zake anakuacha!
ACHA KUJIDANGANYA
Ni vizuri sasa ukatoka kwenye ulimwengu wa giza na kurudi kwenye ulimwengu unaonekana. Kwa hakika ni vigumu sana kumpenda mtu ambaye hujamuona, labda kama unataka kucheza na muda wako.
Wako anakuja, vuta subira ukifanya mambo yako kwa usahihi. Usijidanganye na matapeli wa mapenzi. Wapo ambao wanafanikiwa kuingia kwenye mapenzi lakini mwisho wao hauwi wenye mafanikio.
Penzi la dhati hubebwa na vitu vingi sana, ukiachana na UPENDO kuna suala la tabia na mengine mengi ambayo huwezi kuyajua kwa njia ya kuwasiliana pekee. Utajihakikisha umempenda kwa kumtengeneza kichwani mwako, mwisho wa siku unakutana na mtu ambaye yupo tofauti na mawazo yako, itakuwaje hapo?
Ondoka kwenye giza! Kwa leo naishia hapa, hadi wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi ya hii, USIKOSE!

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...