Saturday, June 9, 2012

MTOTO WA KIGOGO AFANYA PATI YA BUNDUKI



MTOTO wa kigogo serikalini, Peter Rupia amefanya pati ya bunduki.
Peter alifanya pati hiyo hivi karibuni nyumbani kwake, Mbezi Beach, Dar es Salaam akiwashirikisha marafiki zake ambapo walilewa na kulengana shabaha wakati risasi zikiwa ndani ya bunduki.
Huku akitambua kuwa ni kosa kisheria, Peter aliruhusu silaha hiyo ya moto itumike kuwatishia wanawake (kwa utani) ambao walikuwa wakinyoosha mikono juu kama ishara ya kusalimu amri.
Uwazi lina picha zinazoonesha jinsi pati hiyo ya bunduki ilivyofanyika ambapo baadaye wahusika walipolewa chakari, walivua nguo na kufanya vitendo visivyoandikika...
Shuhuda wa tukio hilo, alisema bunduki hiyo aina ya ‘shortgun’ kwanza alipewa kijana mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Sammy lakini baadaye kila aliyekuwa na hamu ya kuichezea, hakukuwa na kipingamizi cha kufanya hivyo.
Hata hivyo, aliyetia fora kucheza na silaha hiyo ni Sammy ambaye alikuwa akiichukua bunduki hiyo na kulenga mbingu au muelekeo wa bahari huku wasichana waliokuwa wamelewa wakifurahia kitendo hicho bila kujua hatari ya kuchezea chombo hicho kilichokuwa na risasi za moto sita.
Habari zinasema kuwa Sammy licha ya kulenga bunduki huku na kule, alikuwa akiichukua bunduki hiyo na kuzunguka nayo kwa wasichana mbalimbali ambao nao walikuwa wakiigusa huku akiwa ameikumbatia mfano wa mtoto mchanga, akiwa amevaa bukta na kubaki kifua wazi.
“Sisi tulishangaa, kwa nini sehemu ya ulevi kama ile itolewe bunduki ndani tena ikiwa na risasi na kupewa watu kuichezea? Huko ni sawa na kumchezea sharubu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema,” alisema mtoa habari wetu.
Habari zinasema awali ilikuwa haijulikani bunduki hiyo ilikuwa ya nani lakini baadaye wakagundua ni ya Peter kwani alionekana kuibeba na kuiweka ndani.
HOT POT lilipata baadhi ya picha za pati hiyo na kuzungumza na Peter ambaye alisema yupo Arusha lakini akamtupia lawama rafiki yake, Sammy kwamba ndiye aliyehusika na picha ambazo sasa zimesambaa kona mbalimbali jijini Dar.
MAKAO MAKUU YA POLISI
HOTPOT lilifika makao makuu ya jeshi la polisi nchini na kukutana na maofisa kadhaa wa ngazi za juu wa upelelezi na wakashangazwa na kitendo cha kuchezea bunduki hadharani kama ilivyokuwa katika pati hiyo.
Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP) ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji, alisema kisheria silaha hairuhusiwi kumuazima mtu yeyote na kuichezea kama walivyokuwa wakifanya watu hao.
Alisema kwa kuwa kuna taarifa kwamba suala hilo lipo katika Kituo cha Polisi cha Kawe, wao makao makuu ya polisi watafuatilia kuona hatua iliyochukuliwa.
“Kitu cha kwanza tulichokifanya tumeona kwenye kumbukumbu zetu kuwa amemilikishwa kihalali kwa jina la Peter M. Rupia,” alifafanua kamanda huyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...