Saturday, September 17, 2011

MV Spice Islanders ilibeba abiria 3,000

Meli ya MV Spice Islanders ikielewa katika bahari eneo la Nungwi Zanzibar nchini Tanzania, inasadikiwa kuwa kabla ya kupata ajali meli hiyo ilikuwa imebeba abiria 3000, huku uwezo wake ukiwa abiria 6000



MELI ya MV Spice Islanders iliyopata ajali mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha vifo vya takriban watu 200 na majeruhi 619 ambao waliokopolewa, ilibeba abiria 3,000 wakati uwezo wake ni kubeba abiria 600 tu.Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa idadi hiyo kubwa ya abiria, haijumuishi mizigo ambayo kiasi chake bado hakijajulikana.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Fakhi Dadi alisema jana kuwa mkoa huo umepoteza watu 1,600 katika ajali hiyo, huku Wilaya ya Wete pekee ikiwa imepoteza watu 1,141.Dadi alisema hayo alipokuwa akizungumza mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

“Wilaya ya Micheweni imepoteza watu 367, huku Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ikipoteza watu 27 na Wilaya ya Chakechake imepoteza watu 148,” alisema Dadi na kuongeza:

“Kwa idadi hiyo ikijumlishwa na idadi ya watu 619 waliosalimika katika ajali hiyo na wengine 204 waliotambuliwa na kuzikwa na wengine watano waliookotwa Mombasa, huenda meli ile ilikuwa na watu 3, 000,” alisema Dadi.

Kutokana na takwimu zinazoendelea kukusanywa, hadi sasa zaidi ya watu 2,000 hawajulikani walipo, mbali ya wale 198 walioopolewa na kuzikwa na wengine 619 walionusurika.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...