Thursday, September 8, 2011

FUMANIZI DUKANI!




TIMBWILI la aina yake likiacha vumbi hewani liliibuka hivi karibuni kufuatia mwanamke aliyefahamika kwa jina la mama Paul kumfumania mumewe, Vincent Njeta ‘baba Paul’ akijivinjari na kimada ndani ya duka lao la biashara.

Tukio hilo ambalo ni miongoni mwa machache yaliyowahi kufunga mtaa nchini, lilijiri saa 4 asubuhi ya Septemba 2, mwaka huu maeneo ya New White Inn, Sinza Kijiweni, jijini Dar es Salaam.

Katika mzozo huo wa fumanizi, kuna watu walisikika wakisema kwamba, baba Paul ambaye anamiliki duka la kuuza pombe aina ya Banana maeneo hayo, amekuwa akitumia sehemu yake hiyo ya biashara kujiachia na vimwana.

NI MARA YA TATU KUFUMANIWA!
Habari ziliendelea kudai kwamba, hii ni mara ya tatu kwa baba Paul kufumaniwa na mkewe akifanya kamchezo hako ndani ya duka lake na kila anaponaswa huwa anamuomba msamaha mkewe na kuyamaliza kimyakimya.

Kwa mujibu wa mashuhuda, siku hiyo majirani wa baba Paul waliochoshwa na tabia ya mwanaume huyo kuingiza ‘mademu’ ndani ya duka ndiyo waliokwenda kumtonya mkewe ambaye naye alifika haraka na kumnasa mumewe.

Katika ‘sheshe’ hilo ambalo mwanamke aliyefumaniwa aliponyoka mikononi mwa mama Paul  na kutimua mbio akiwa na khanga tu, baba Paul alikatwa kidole na damu nyingi kumwagika.

Akiongea kwa jazba huku akiwa amemkunja mumewe, mama Paul alisikika akisema kuwa amechoshwa na mwenendo wa mumewe huyo huku pia akilalamikia kitendo chake cha kutorudi nyumbani siku tatu nyuma (toka Eid Mosi).

“Nimechoka  baba Paul jamanii…leo hii ni mara ya tatu nakufumania na ‘viwanawake’ vyako dukani, sikubali nataka talaka yangu vinginevyo leo utanitambua, halafu una siku tatu hujarudi nyumbani wewe,” alisikika mama Paul.

Kutokana na vurugu kuwa kubwa, wasamaria wema waliwapigia simu maafande wa Kituo cha Polisi cha Urafiki-Ubungo, Dar ambao baada ya muda mfupi walivamia eneo la tukio na kufanikiwa kuzima songombingo hilo kisha kuwabeba wanandoa hao mpaka kituoni.





No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...