Sunday, September 18, 2011

MAAJABU AJALI YA MELI: Mtoto miezi 4 aelea bila boya...



MWACHENI Mungu aitwe Mungu! Wakati Visiwa vya Zanzibar vikiendelea kuomboleza msiba mkubwa wa kuwakosa ndugu zao waliokuwa wakisafiri kwa meli iliyopinduka na kuzama ya MV Spices Islander (pichani),  maajabu yanabaki kwa mtoto mchanga wa miezi minne aliyekutwa akielea bila boya la kuogelea.

Kwa mujibu wa waokoaji wa tukio hilo lisilosahahulika lililotokea eneo la Nungwi, ambapo meli hiyo ilikuwa ikitokea Unguja kwenda Pemba, mtoto huyo ambaye jina lake halikupatikana alikuwa akielea kwa saa 5 tangu ilipozama meli hiyo.

Ilidadavuliwa kuwa, baada ya waokoaji kufika eneo hilo wakiwa na helkopta, walimuona mtoto huyo ambapo ilibidi wambebe peke yake na kumuwahisha katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.

ASHTUKA USINGIZINI, AANZA KULIA
Ilielezwa kuwa, katika harakati za kumuokoa, alipoguswa ndipo aliposhtuka kutoka usingizini na kuanza kulia huku mama yake akisadikiwa kuzama baharini na kufariki.


Kwa mujibu wa Runinga ya Channel Ten, mtoto huyo alikutwa akielea juu ya maji licha ya kutovalishwa kifaa chochote maalumu cha kuogolea.





AIBUA MJADALA MZITO
Hata hivyo, taarifa ya kutozama kwa mtoto huyo iliibua mjadala mzito ambapo kwa mujibu wa wanamaji, inawezekana alikuwa amevalishwa nepi na ‘pempasi’ yenye nailoni ndiyo maana hakuzama.

Kundi lingine lilidai kuwa, hata kama angekuwa amefungwa pempasi, angezama eneo la kichwa na kubakiza sehemu iliyofungwa pempasi ikiwa juu hivyo wao waliamini ni Mungu tu!

 Hata hivyo, habari za uhakika zilidai kuwa mtoto huyo anaendelea vizuri.
Hadi gazeti hili linatinga mitamboni, zaidi ya watu 240 waliripotiwa kupoteza maisha na zaidi ya 600 kuokolewa katika ajali hiyo mbaya.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...