Friday, September 9, 2011

Sababu za wanadamu kuchukiana ni nini hasa?

KATIKA maisha yetu bila shaka tuna watu wengi au wachache ambao toka moyoni mwetu tunawachukia na pengine tamaa yetu ni kuona wanapatwa na mabaya kila siku. Miongoni mwao ni watoto, wazazi,waume, wake na  ndugu zetu.

Pamoja na kuwepo kwa chuki ya asili ambayo nayo hufanya kazi kwenye maisha ya mwanadamu, lakini wengi wetu tuna chuki zinazotokana na orodha ya mabaya tuliyowahesabia wenzetu.

Mume anaweza kuwa na orodha ndefu ya matendo machafu ya mkewe tangu walipooana miaka saba iliyopita, ambapo kila siku anapomtazama tu huwa kama anatazama CD ya matukio yaliyopita na kuifanya chuki yake kukuwa kila siku.

Kwa bahati mbaya, wanadamu wengi wako hai kwenye mabaya, uwezo wao wa kukumbuka makosa ni mkubwa zaidi kuliko wema wanaofanyiwa.  Tabia hii inatokana na ukweli kwamba, akili zina tabia ya kukosoa muonekano na taarifa ya vitu, lengo ni kuweka ulinganifu wa jinsi mtu anavyojitambua.

Kwa mfano msichana akijitambua mwenyewe kwamba yeye ni mzuri, mtazamo wake kuhusu wanaume utakuwa ni wa kuwalinganisha na jinsi alivyo na wakati wote atapenda kuona anaokutana nao mtaani wawe kama yeye, vinginevyo atawachukia.

Bila shaka uchunguzi umebaini kuwa msingi wa chuki zetu ni ubinafsi wetu. Wanadamu ni wabinafsi kwenye mali zao, mafanikio yao, uwezo, matakwa na muonekana wao.

Kwa kutambua hilo, kinachotujengea chuki juu ya wenzetu ni ‘USISI’ ambao kila mtu anao. Wako wenye usisi wa udini, ukabila, rangi, jinsia, uwezo, elimu na tabia. Hali hii ndiyo inayowafanya wawaone wenzao kama wakosaji.

Unamchukia mumeo kwa sababu unataka awe kama unavyopenda, hupendani na mfanyakazi mwenzako, jirani yako, mke mwenzako kwa vile unajenga msukumo wa usisi kwenye mtazamo wako juu yake.

Ifahamike kwamba msingi huu wa maisha ni hatari kwa vile umekuwa mzigo mzito kwenye maisha ya wanadamu wengi. Watu wengi wamepata matatizo makubwa kwenye maisha yao kwa sababu walishindwa kujigundua kuwa wana usisi na hivyo kulazimisha ulimwengu ufanye watakavyo, jambo ambalo ni gumu.

Ni ukweli ulio wazi kwamba, hatuwezi kuishi kwenye mtazamo wa kutaka mapenzi yetu yatimizwe na kuwa na msukomo wa lazima wa kuifanya jamii inayotuzunguka itumikie mtazamo wetu. Kamwe hatuwezi kuwafanya wenzetu, watembee, waongee, wawe na tabia kama zetu.

Hii ina maana kwamba kama tulikwenda kwa mtu kutaka mkopo tukanyimwa, tulitaka msaada tukakosa, tuliomba heshima, tulitarajia chochote kwa wenzetu hatukupewa sawa na mahitaji, jawabu letu lisiwe chuki kwa vile haitusaidii kujengea usisi wetu.

Wajibu wetu mkuu kwenye maisha ni kujitambua na kuacha wengine nao watumikie kujitambua kwao kama binadamu. Tusiingie kwenye uhasama wa bure kushindania mtazamo. Tukumbuke mpaka tunaondoka duniani hali ya kila mmoja kujitambua mwenyewe haitafutika.

Mama Theresa aliacha neno la msingi kwenye maisha yetu lisemalo: “If you judge people, you have no time to love them.” Kama utakuwa mwenye kuhukumu wengine hutakuwa na muda wa kuwapenda Ni vema tusiwe wepesi wa kuhukumu badala yake tukubali ubinadamu wa wenzetu katika maisha.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...