Saturday, September 17, 2011

KIFO CHA KUSIKITISHA CHA BI. HARUSI KWENYE AJALI YA MELI



Ajali ya meli ya MV Spice Islander, imeacha maumivu makali kwa Watanzania wengi hususan wakazi wa Zanzibar. Familia nyingi zimeweka matanga kwani zipo zilizopoteza makumi ya watu ikiwemo ile iliyofiwa na ndugu 30 kwa mkupuo.

Yahya Awadh, 23, naye analia kwa staili yake kwa sababu mwanamke aliyeamini ndiye wa maisha yake, amemezwa kwenye ajali hiyo na mpaka alipozungumza na blog hii juzi (Jumanne) saa 8:26 mchana, mwili wake ulikuwa haujapatikana.

Munira, 19, amemuacha Yahya kwenye maumivu makubwa, kwani ameaga dunia kabla hajakamilisha ahadi yao ya kufunga ndoa Septemba 29, mwaka huu.

Yahya aliliambia Amani juzi kuwa kifo cha Munira kinasikitisha kwa sababu alifariki dunia wakati akizungumza naye kwenye simu.





Alisema, Munira alianza kuona hali ya hatari mapema na akawa anamjulisha kinachoendelea kila hatua ndiyo maana hata alipoanza kufikwa na mauti, hali hiyo ilimkuta wakizungumza.

“Kabla ya kufunga ndoa yetu, kwenye familia yao kukawa na ndoa nyingine ya ndugu yake, kwa hiyo alipata ajali akiwa anakwenda kwenye harusi ya ndugu yake, Wete, Pemba,” alisema Yahya na kuongeza:

“Munira alianza kuona hali ya hatari mapema, tatizo kifo kwa binadamu ni siri kubwa. Alipofika bandarini, alinipigia simu kunieleza kwamba meli ilikuwa imejaa sana, mimi nikamshauri aahirishe safari lakini aliniambia ameshakata tiketi.

“Safari ilipoanza, aliniambia watu ni wengi sana na hakukuwa na kupishana ndani ya meli. Akaniambia tena mwendo wa meli unatia wasiwasi.”

Yahya aliendelea kusema kuwa Munira kila alipozungumza naye, alimueleza wasiwasi wake kuhusu usalama wa meli hiyo kwa jinsi ilivyojaza na mwendo wake.





Alisema, saa 5:00 usiku (Ijumaa), Munira alimueleza: “Dear, meli imejaa kupita kiasi.”

Aliongeza: “Saa 5:45 usiku, aliniambia, ‘dear, hali ni mbaya, tuombee’, mimi nilimtoa wasiwasi, nikamwambia namuombea na Mungu atawalinda na wangeweza kufika salama.

“Ilipofika saa 6:30 usiku (Jumamosi), aliniambia ‘dear usilale, meli inapoteza uelekeo’, yaani tulikuwa tunawasiliana hatua kwa hatua.”

Yahya alisema kuwa kuna kipindi cha kama dakika 15 hivi, alipitiwa na usingizi simu ikiwa mkononi na aliposhtuka alikuta ‘missed calls’ nyingi kutoka kwa Munira.

“Haraka sana nikampigia, alipopokea aliniambia ‘dear nilikwambia usilale utuombee, meli imeshaanza kuzama’.  Nilichanganyikiwa, kwani ukiachana na sauti yake, kulikuwa na sauti za watu mbalimbali waliokuwa wanalia. Hali ilikuwa mbaya sana.

“Saa 7:07 usiku, mchumba wangu aliniambia, ‘dear yameshaingia ndani, ni hatari’.



Baada ya muda kidogo alisema, ‘dear maji hayo, tunakufa’, baada ya hapo hakuzungumza tena. Nikawa nasikia sauti ya mwangwi usioeleweka. Hapo nikahisi simu imemezwa na maji.

“Nilijaribu kuita bila mafanikio, Munira hakuitika, simu ikaendelea kutoa sauti ya mwangwi. Picha ikanijia, nikaona Munira wangu anapambana na maji kuokoa maisha yake lakini ndiyo hivyo, Munira wangu hayupo tena. Nasubiri waokoaji waliotoka Afrika Kusini kama wanaweza kupata mwili wake,” alisema Yahya na kuongeza:






“Namuomba Mungu aiweke mahali pema roho ya mchumba wangu, nitaendelea kumpenda hata kama ametangulia. Nitamkumbuka daima. Nawatakia makazi mema ndugu wengine wote waliokutwa na maafa kwenye ajali hiyo.”

Meli ya MV Spice Islander ilizama Jumamosi iliyopita saa 7 usiku, watu zaidi ya 250 wameshabainika kupoteza maisha, huku wengine zaidi wakitajwa kuwemo baharini na miili yao haijaokolewa.

Zaidi ya watu 800 waliokolewa wakiwa hai kwenye ajali hiyo, hivyo kuonesha kwamba meli hiyo ilikuwa imebeba watu zaidi ya 1000 wakati uwezo wake ni abiria 645.




No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...