Friday, September 9, 2011

Mama azaa jiwe...

...Jiwe alilojifungua Ngeme Makala.

UKISTAAJABU ya Musa, utayaona ya Firauni. Ndivyo unavyoweza kusema kuhusiana na tukio la kustaajabisha la mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Kunzugu, Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara, Ngeme Makala (25),  kujifungua jiwe badala ya binadamu.

Tukio hilo la ajabu ambalo limevuta hisia za wengi lilitokea hivi karibuni nyumbani kwa mwanamke huyo kijijini hapo.

...Ngeme Makala aliyejifungua jiwe.

Mpaka sasa, baadhi ya watu wanasema ni tukio la kushtusha lililowahi kutokea kwa mwaka huu wa 2011 licha ya kwamba matukio ya wajawazito kujifungua viumbe wa ajabu ni kitu cha kawaida.

Akiongea kwa masikitiko makubwa na mwandishi wetu, Ngeme alisema kuwa katika mambo ambayo hataweza kuyasahau maishani mwake ni hili la kujifungua jiwe badala ya binadamu.

...Kadi ya Kniniki ya Ngeme .

“Kwa kweli sijui niseme nini. Ni tukio ambalo hadi sasa bado siamini. Sidhani kama nitasahau maishani mwangu, unabeba mimba ukitegemea kupata mtoto, lakini kumbe siku ya mwisho unapata jiwe!” alisema Ngeme.

Hata hivyo, nyuma ya tukio hilo kuna maajabu matano ambayo kwa mtu yeyote mwenye ufahamu wa kawaida anaweza kuamini dunia imefikia ukingoni kama siyo mwisho.

...Kadi ya Kniniki kwa ndani.

MWANZO WA MAAJABU
Ngeme anasema: “Tukio la kwanza ambalo lilianza kunishangaza ni baada ya ujauzito wangu kufikisha miezi sita kwani ulipotea ghafla na kuzua maswali mengi kwa watu, akiwemo mume wangu.

“Nilikwenda kliniki manesi wakaniambia kuwa, ujauzito haukuwa na joto. Lakini pia kwa mtazamo mimi sikuwa na mimba wala dalili zake.

MAAJABU YA PILI
Mwanamke huyo alitumia dawa za mitishamba kuurudisha ujauzito huo jambo ambalo liliwashangaza majirani zake kuona kwamba, ujauzito unaweza kupotea kisha ukarudishwa kwa dawa za porini.

...Ngeme akiwa na mumewe, mkononi ameshika jiwe alilojifungua hivi karibuni.

“Mume wangu alinipeleka kwa bibi mmoja ambaye baada ya kumweleza tatizo alinipa dawa za mitishamba, nikatumia ndani ya wiki moja tu, mimba ikaanza kuonekana tena na kuendelea kukua ambapo mtoto alicheza kama kawaida.

“Nilipohudhuria kliniki wauguzi walinithibitishia mimba kucheza na mtoto kuongezeka kimo.

MAAJABU YA TATU
Ujauzito wa mwanamke huyo ulikaa muda mrefu zaidi, kwani mpaka anajifungua jiwe hilo, ulishatimiza miezi 11 tumboni.
Matarajio ya awali kutoka kwa madaktari, mwanamke huyo alikuwa ajifungue Juni mwaka huu, lakini akapita hadi Agosti.

MAAJABU YA NNE
Wakati wa kujifungua, jiwe hilo lilijaa damu nzito pande zote kuashiria kwamba, mtoto alikuwa katikati yake. Hali hiyo ilimpa wakati mgumu mkunga wa kijiji hicho, Monica Lazaro ambaye alianza kuamini kuna kitu nyuma ya pazia juu ya ujauzito wa mwanamke huyo.

...Ngeme.

MAAJABU YA TANO
Tangu kuzaliwa kwa jiwe hilo, bibi mtu amekuwa akimfunika khanga huku akimwita mjukuu na ilifika mahali akasema atamhifadhi ‘mjukuu’ wake huyo mpaka akili yake itakapoamua vinginevyo.

DALILI ZA KUJIFUNGUA
Ngeme anasema: “Siku hiyo nilihisi kuumwa uchungu tangu saa 1:00 asubuhi, kutwa nzima nilikuwa nahangaika, nikawa nakwenda haja ndogo kila wakati. Ilipofika alfajiri maumivu yalizidi, ghafla chupa ikapasuka nikaanza kusukuma, ajabu badala ya kutoka mtoto nikaona jiwe likiwa kwenye damu.”

Kwa upande wa mumewe, Nyamulekela Kennedy (33), alisema kuwa muda wote wa ujauzito mkewe alikuwa akihudhuria kliniki na kuambiwa hakuwa na tatizo, kiumbe kilikuwa kikicheza kama kawaida, ukiondoa tatizo la kupotea kwa ujauzito wakati fulani.

Kuhusu mkewe kujifungua jiwe, Nyamulekela alisema baada ya kuona likiwa limetapakaa damu, alilazimika kuita watu na viongozi wa serikali ya kijiji hicho, akiwemo mwenyekiti wake, Magesha.

HISTORIA YA FAMILIA KWA UFUPI
Mume huyo anasema Ngeme ni mke wake wa pili baada ya kuachana na wa kwanza ambaye alipata naye watoto watatu.

MAAJABU MENGINE
Wazee wa Kabila la Wasizaki walimweleza mwanaume huyo kuwa wapo wanawake waliowahi kujifungua chura, mapande ya nyama au moshi lakini si jiwe. Wakamwambia kuwa, kitendo cha mkewe kuzaa jiwe kimetokana na nguvu za giza.

Aidha, mkunga wa kijiji hicho alikiri kukuta Ngeme ameshajifungua jiwe likiwa limetapakaa damu na majimaji mengi chini yaliyosababishwa na chupa ya uchungu kupasuka na kudai tukio hilo si la kawaida.

Mmoja wa madaktari wa Hospitali Teule ya Bunda ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kitaalam kitu kama hicho hakiwezi kutokea.

Nazo habari ambazo si rasmi zinadai kuwa tukio hilo ni la pili kutokea katika Wilaya ya Bunda ambapo iliwahi kuripotiwa mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Igundu-Kibara, Bunda, kujifungua kinyonga badala ya binadamu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...