Katika hili niseme tu kwamba, huu ni ulimbukeni uliopitiliza, kuridhishana huko kimapenzi kuna madhara makubwa na wale wanaoendekeza mchezo huo, ipo siku watajuta na kutoa machozi huku wakikosa watu wa kuwabembeleza.
Tubadilike jamani, tuache kufuata mkumbo kwa kufanya yale ambayo yanahatarisha maisha yetu eti kwa kisingizio cha kuogopa kuachwa au kusalitiwa.
Baada ya kugusia kidogo mada hiyo ya wiki iliyopita sasa nirejee kwenye mada yangu ya wiki hii.
Nazungumzia suala la uaminifu ambalo ni nguzo muhimu katika uhusiano ulio ‘siriasi’.
Kila mmoja atafurahi kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu ambaye ni muaminifu kwa sababu hakuna anayefurahi kusalitiwa.
Kila mtu anataka kufurahia penzi lake peke yake na wengine waishie kuona tu kama siyo kula kwa macho. Lakini sasa, uaminifu siku zote ni lazima uanzie kwako. Nasema hivyo nikimaanisha kwamba, itakuwa ni vigumu kutarajia kuwa na mpenzi ambaye ni muaminifu wakati wewe siyo muaminifu.
Unataka mpenzi wako asitoke nje ya ndoa wakati wewe mwenyewe una mademu kibao huko nje, inakuja kweli? Itakuwaje jambo la kukuuma ukisikia mpenzi wako anakusaliti wakati wewe kusaliti ni sehemu ya maisha yako ya kila siku?
Tambua unavyoumia wewe ukisikia penzi lako linamegwa, ndivyo anavyoumia mpenzi wako hivyo ni bora ukajiangalia kabla ya kumgeukia mwenzako.
Kwa nini mada hii?
Yupo rafiki yangu mmoja ambaye aliwahi kunieleza jinsi anavyoumia kumuona mkewe akiwa anapiga stori na wapangaji wenzake wa kiume. Jamaa anasema anahisi mkewe anaweza kushawishika kumsaliti kutokana na ukaribu wao.
Cha ajabu sasa mwanaume huyo ni kiwembe kupita maelezo. Mara nyingi nimekuwa nikitumia muda wangu kumsihi abadili tabia, atulie na mke wake ambaye ni mzuri kuliko hata hao mademu lakini amekuwa mgumu kunielewa. Kila demu mzuri anayekatiza mbele yake anataka amuonje.
Sasa hebu jaribu kuangalia, jamaa ana wivu na mkewe kwa sababu ya ukaribu tu na wanaume lakini yeye ni mwingi wa habari na wengi wanajua.
Hivi huyu anatarajia awe na hisia kwamba mkewe hamsaliti wakati yeye ni msaliti aliyebobea?
Inawezekana kweli mama huyo wala hana mpango wa kumsaliti mumewe lakini mwanaume huyu anahisi anaweza kusalitiwa kutokana na tabia zake za kumsaliti mkewe.
Yaani anahisi anavyomfanyia ndivyo anavyoweza kufanyiwa, kitu ambacho kinaweza kuwa hakina ukweli.
Ndiyo maana nikasema, uaminifu uanzie kwako.
Jenga mazingira ya kumfanya mpenzi wako akuamini na yeye ‘automatikale’ atafanya hivyo.
Wanaosaliti ndiyo wanaosalitiwa,
uchunguzi usiyo rasmi uliofanyika unaonesha kuwa, wanandoa ambao siyo waaminifu ndiyo wanawashawishi wenzao kuangalia uwezekano wa kutoka nje ya ndoa.
Kwa mfano, mume anarudi nyumbani akitokea kwa kimada, mkewe anamhitaji faragha anaambiwa amechoka.
Baadaye mke anapata umbeya kuwa, mumewe ana ‘kitu’ kingine kinamzuzua. Katika mazingira haya ndipo unakuta baadhi ya wanawake ambao si wavumilivu huangalia namna ya kulipiza kisasi kwa kutafuta ‘vidumu’.
Hujawahi kusikia mwanaume anatoka kwenda kwa wanawake mke naye anatoka kwenda kwa mabuzi? Hujawahi kusikia au kusimuliwa mke kaenda kumsaliti mumewe gesti akakutana uso kwa uso na mwenza wake akiwa na kimada? Hiyo inaashiria kuwa, wapenzi na wanadoa wanarithishana mambo mazuri na mabaya.
Ndiyo maana wataalam wa mambo ya mapenzi wanasema, kama wewe ni bingwa wa usaliti basi tambua na wewe unasalitiwa lakini hujui tu. Lakini ukitulia, unakuwa na asilimia flani ya kumfanya mpenzi wako atulie.
Ushauri wangu
Tulia na wako ambaye moyo wako umeridhika kuwa naye. Mpende kwa maana halisi ya kumpenda, tena kwa asilimia zote.
Tamaa za kijinga ziweke pembeni.
Kuwa muaminifu kwake ili iwe chachu ya yeye kutulia lakini nikuhakikishie tu kwamba, kama wewe si muaminifu kwa mwenza wako ni vigumu kutengeneza maisha ya furaha.
Kuwa muaminifu kwake ili iwe chachu ya yeye kutulia lakini nikuhakikishie tu kwamba, kama wewe si muaminifu kwa mwenza wako ni vigumu kutengeneza maisha ya furaha.