Monday, April 9, 2012

Maneno Ya Mwisho Ya Kanumba Kwa Mama Yake Mzazi



Mama Mzazi wa Steven Kanumba anayeitwa Flora Mtegoa.

WAKATI Taifa la Tanzania likiwa katika majonzi mara baada ya kupoteza moja kati ya vijana wake walio peperusha vyema ndani na nje ya mipaka pendera yake kupitia tasnia ya Filamu STEVEN KANUMBA, yafuatayo ni mahojiano kati ya mdau wa blog ya G. Sengo mkoani Kagera mwandishi wa habari anayeitwa Nicolaus Ngaiza, aliyoyafanya na Mama Kanumba (Flora Mtegoa).

Katika mahojiano yaliyofanyika leo majira ya saa nane mchana katika uwanja wa ndege Bukoba katika harakati za safari kuelekea jijini Dar es salaam ILIKUWA HIVI:-

Nicolaus Ngaiza:- Mama unamwelezeaje Steven Kanumba katika kipindi cha uhai wake?
MAMA:- Kanumba mtoto wangu mtiifu, rafiki yangu, mpendwa wangu, mtotowangu wa karibu na jana niliongea naye kwenye simu na alfajiri naambiwa kafa.

Nicolaus Ngaiza:- Pengine alizaliwa sehemu gani mwaka gani?
MAMA:- Kanumba alizaliwa tarehe 8/1/1984 mkoani Shinyanga, katika hospitali ya Government Shy.

Nicolaus Ngaiza:- Baba yake yuko hai?
MAMA:- Baba yake yuko hai yuko Shinyanga anaitwa Charles Kanumba

Nicolaus Ngaiza:- Katika kipindi hiki kigumu unawambiaje watu wa Bukoba?
MAMA:- Naomba waniombee kwani hali yangu siyo nzuri kwani niko katika kipindi hiki kigumu.

Nicolaus Ngaiza:- Labda mama kijijini kwenu ni wapi?
MAMA:- Mimi natoka Wilayani Muleba, kata ya Izigo, kijiji cha Itojo.

Nicolaus Ngaiza:- Steven Kanumba sisi tunamjua kwa jina hilo jeh! hakuwa na jina la kinyumbani?
MAMA:- Hakuwa na jina lolote la kinyumbani zaidi ya hilo Kanumba la Kisukuma yeye ni msukuma.

Nicolaus Ngaiza:- Tungependa kujuwa neno la mwisho mlio weza kuzungumza pamoja.
MAMA:- Aliniambia mama natuma nauli uje tuagane naondoka naenda Marekani, akiwa mwenye furaha, tunataniana...

Nicolaus Ngaiza:- Labda aliwahi kukwambia ndoto zake katika maisha kwamba analenga kufanya nini?
MAMA:- Yeye ndoto zake ni kuendeleza sanaa yake na ninashukuru alikuwa amefika mbali kisanaa.

Nicolaus Ngaiza:- Labda kifamilia alikuwa ameoa au alikuwa na mtoto?
MAMA:- Hajawahi kuoa na hakuwa na mtoto...

CHANZO: MJENGWA BLOG

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...