Monday, April 9, 2012

KAJALA KESI UPYAA!




KESI inayomkabili msanii maarufu wa filamu Bongo, Kajala Masanja na mumewe, Faraja Chambo juzi (Jumatano) iliingia hatua nyingine baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar inaposikilizwa kesi yao ya kutakatisha fedha haramu kusema itaanza kusikilizwa upya baada ya upelelezi kukamilika.
Katika kesi hiyo, mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Leonard Swai aliwasomea mashitaka wanandoa hao na kusema mnamo Aprili 14, mwaka 2010, walimuuzia nyumba, Emmilian Rugalila ambayo iliwekwa kizuizi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) huku wakijua ni kosa kisheria.

Mwendesha mashitaka huyo alisema kuwa, nyumba hiyo iliwekewa kizuizi na Takukuru baada ya kubainika ilinunuliwa kwa fedha haramu zilizopatikana kwa njia ya rushwa. 

Baada ya kusomewa shitaka hilo, kila mmoja alikana kutenda kosa hilo mbele ya hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Sundi Fimbo ambaye alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa upya Aprili 18, mwaka huu kufuatia upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi na washitakiwa walirudishwa rumande katika Gereza la Segerea, Dar.

Kitendo cha wanandoa hao kunyimwa dhamana kiliibua simanzi ambapo baadhi ya ndugu waliokuwa mahakamani hapo walionekana wakifarijiana huku wakifutana machozi.

Aidha, ndugu hao walionekana wakiwapa Kajala na mumewe dawa za meno, mikate, fedha za matumizi na kadhalika ambapo Kajala alipokea kwa huzuni na kuishia kusema: “Mimi nasali ili Mungu aniokoe, nanyi niombeeni ndugu zangu.” 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...