Saturday, April 21, 2012

MAHABA: Kung’ang’ania penzi ni hatari, chunga sana!



NIANZE kwa kuwasalimu marafiki zangu. Natumaini mko poa na mnaendelea na majukumu ya kila siku. Kupitia hapa tunapata kujifunza na kuwekana sawa katika masuala mbalimbali yanayohusu mapenzi.

Leo nimeona tuzungumzie hili la kung’ang’ania penzi kwani athari zake ni kubwa sana katika uhusiano. Anayeng’ang’ania huwa anaumia siku zote.

Natambua nguvu za mapenzi. Naheshimu sana hisia za mtu aliyependa kweli.Pamoja na hayo yote, lakini yakupasa kuwa makini kugundua sehemu unayong’ang’ania ni salama kwako au unapoteza muda wako bure.

Jaribu ‘kuu-control’ mwili wako. Usikubali kupelekwapelekwa na hisia za matamanio ya mwili. Utamu huwa unakuja pale unapong’ang’ania sehemu sahihi lakini vinginevyo, ni mateso bila chuki.

Nasema hayo kwa sababu, wapo wengi wanaendeshwa na hisia kulazimisha mapenzi sehemu ambayo hawapaswi kufanya hivyo. Ieleweke kuwa mapenzi siyo mchezo wa kuigiza, hivyo usipokuwa makini katika hili mwishowe utakuja kujuta kwa kupoteza muda wako kwa mtu asiyekuwa na hata chembe ya mapenzi kwako.

Tatizo hili, lipo pande zote mbili kwa wanawake na wanaume.Utakuta mtu anang’ang’ania sehemu pasipo kujali adha za baadaye za maisha anayoyang’ang’ania. Dondoo chache zifuatazo hapa chini, zitakusaidia kutambua athari za kung’ang’ania na ikibidi ujiepushe mapema!

TAMBUA MALENGO
Ni vema ukamtambua mpenzi wako ana malengo gani kwako, Je, anawaza kama wewe unavyowaza? Kama mpo tofauti kimawazo ni dhahiri kuwa mapenzi yenu yatakuwa ni kipofu. Bora liende. Hakuchi kunakucha.

Mkiwa wote hamtambui malengo katika uhusiano wenu au mmoja wenu ndiyo anatambua na mwingine hatambui hapo hakuna mapenzi bali mateso tupu ndiyo yanayotawala.

MCHUNGUZE KWA MAKINI
Yawezekana kabisa mtu akaongopa, haswa katika siku za mwazo za uhusiano. Mtu huyo ni rahisi kuchomoza makucha yake ndani ya muda mfupi. Utambaini kama utafanya uchunguzi kwa makini utajua kama alikuwa muongo, utachukuwa hatua za haraka.

Pale unapobaini kuwa pengine mwanzoni aliingia kwa kuahidi mambo makumbwa ya uhusiano, jaribu kumweka karibu mara kadhaa kwa kumshauri na kumkumbushia ahadi alizoziweka pale awali.
Binadamu unapomkumbusha ahadi zake katika lugha nzuri, kama alipitiwa ni rahisi kukumbuka na kubadilika mara moja. Angalizo hapo ni kwamba usiwe mtu wa kumkumbushia kila wakati halafu mtu habadiliki, usimng’nga’anie.

SOMA ALAMA ZA NYAKATI
Tabia ya mtu siku zote huwa haijifichi. Kuna baadhi ya watu huwa hawabadiliki hata ufanye nini. Utaumiza kichwa chako bure usiposoma alama za nyakati. Msome mpenzi wako kwa kutazama jinsi alivyo. Ni mtu wa aina gani? Mwanzoni na sasa amebadilika kwa kiwango gani?

Unaweza kuwa unang’ang’ania pasipo kujua huyo unayemng’ang’ania ni mfupa uliomshinda fisi. Kama ni mwanaume utakuta anamsururu wa wanawake . Haoni hata sababu ya kung’ang’aniwa. Hana malengo yoyote, hawezi kuheshimu mapenzi hata siku moja.

Hata kama umempenda vipi, kamwe huwezi kuwa tayari mpenzi wako awe malaya wa kupindukia labda kama huna malengo naye. Muonye kadiri ya uwezo wako, ukiona habadiliki chukua hatua moja mbele.

MWEKEE KIPIMO
Kumwekea mpenzi wako kipimo ni jambo zuri. Tatizo ambalo amekuwa akikusumbua nalo kila wakati, ni vema ukalipima kwa kuangalia uwezekano wa mhusika kubadilika.
Pigana kwa nguvu zote kuhakikisha mpenzi wako anarudi katika mstari lakini ukibaini ni asili yake, achana naye kwani yawezekana hajawahi kukupenda zaidi ya kukutamani tu.

JIWEKEE MIKAKATI
Usiwe mtu wa kukurupuka. Kuwa na mikakati na mpenzi wako. Mara nyingi mwanaume au mwanamke ambaye hana malengo na mwenzake huwa hataki kusikia mkipanga mikakati.Kujiwekea mikakati na ukamshirikisha mwenzako ni silaha kubwa sana ya kumtambua mpenzi wako kama mpo pamoja katika safari au la. Utakuta ukianza kuzungumzia mikakati ya mapenzi mwenzako anaanzisha stori nyingine tofauti, chunga sana!

Mapenzi huwa ni hisia lakini kuna wakati hata mtoto mdogo anaweza kubaini kama sehemu aliyojiweka hakuna faida. Sasa kama mtu hana malengo na wewe katika mapenzi unadhani nini hatima yake?

Jipange vema, mtazame unayempenda kama na yeye anakupenda kweli. Ni hatari sana kumng’ang’ania mtu asiyekuwa na malengo kwani mwisho anaweza kufikia hatua hata ya kuoa au kuolewa halafu ndoa ikawa haina amani 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...