Wednesday, April 25, 2012

Mama: Wachumba wa Kanumba wananisumbua




MENGI yanaendelea kuzuka baada ya kifo cha gwiji wa filamu za Kibongo, Steven Charles Kanumba, safari hii wasichana  wanaodai ni wachumba wa marehemu, wamemzukia mama yake mzazi na kutaka kutambuliwa kama sehemu ya familia hiyo...



 HABARI KAMILI
Akizungumza katika mahojiano maalum, mama mzazi wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa alisema kwamba baada ya kifo cha mwanaye anapata wakati mgumu kutokana na wasichana wanaomfuata wakidai walikuwa na uhusiano na mwanaye.

“Inanishangaza sana, wengi wanakuja. Wananiulizia na nikiwakaribisha wananipa pole ya msiba, halafu wanajitambulisha. Wanakuja kwa nyakati tofauti lakini madai yao yanafanana.

“Eti walikuwa wachumba wa Kanumba. Ninapowadadisi sana ni kwa nini wamekuja na madai hayo muda huu, wanasema eti wanataka kutambuliwa na familia. Nikiwauliza ili iweje, wanasema basi tu!

“Najiuliza sana, hivi hawa wasichana walikuwa wapi, wakati mwanangu akiwa hai? Mbona hawakuja wakati huo kusema wana uhusiano naye? Mimi nabaki na maswali yasiyo na majibu,” alisema mama huyo na kuongeza.


“Sijaelewa mantiki hasa ni nini, lakini ngoja nione. Kama nitaona ni jambo kubwa linalohitaji usaidizi, nitafanya hivyo, lakini kwa sasa naacha kama lilivyo.”

 ISHU YA WATOTO
Akiendelea kushuka na mistari, mzazi huyo wa Kanumba alisema, amesikia pia kuhusu wanawake wanaojitokeza kwenye vyombo vya habari na kudai kuzaa na Kanumba, jambo ambalo linamuacha mdomo wazi.

“Kwa nini walikuwa kimya muda wote? Hata hivyo, Kanumba mwenyewe hakuwahi kuniambia hata siku moja kuwa ana mchumba ama mtoto. Mimi naamini kama jambo hilo lingekuwa la kweli, sehemu pekee ya kupata suluhu ilikuwa kwa wazazi (akimaanisha pamoja na yeye).

“Sasa kama ndivyo, ni kwa nini hawakufika nyumbani na kunieleza juu ya jambo hilo? Hapa ukichunguza vizuri utagundua kuna tatizo. Sisi kama familia, hatuna taarifa rasmi ya uzao wa mwanetu.”

 KANUMBA HAKUWA NA MCHUMBA
Mama Kanumba anasema, kwa mujibu wa mwanaye, mpaka mauti yanamkuta alikuwa hana mchumba na hakuwahi kumtambulisha kwa msichana yeyote kuwa ni mchumba wake.

“Sikuwahi kutambulishwa na Kanumba kuhusu mchumba. Licha ya kutokunikutanisha, hata kuniambia tu, hakuwahi sasa hao watoto wanatokea wapi? Kwa sasa nitaendelea kushikilia maneno ya marehemu mwanangu,” alisema.

 TUJIKUMBUSHE
Miezi michache kabla ya Kanumba kufariki dunia, akiwa katika mahojiano na Mtangazaji Zamaradi Mketema wa Clouds Tv, alisema hana mke, mchumba wala mtoto.

Wakati akifanya mahojiano hayo katika runinga hiyo, alikuwa na mama yake mzazi muda wote wa mahojiano katika kipindi cha Take One kinachozungumzia mambo ya sanaa na wasanii wa filamu za Kibongo.

Aidha, wiki chache kabla ya kifo chake, katika Kipindi cha Mkasi kinachoendeshwa na Salama Jabir katika Runinga ya Afrika Mashariki (EATV), alirudia maneno yale yale, kuwa hana mchumba wala mtoto. 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...