Tuesday, April 17, 2012

BIBI AKUTWA UCHI KWENYE KABURI LA KANUMBA...





Bibi Kizee huyo akiwa amezungukwa na wananchi baada ya kukurupushwa eneo la tukio.

Kaburi la Marehemu Steven Kanumba.
BI. Kizee anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 70, ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, usiku wa kuamkia Jumatano, wiki iliyopita alinusurika kifo baada ya kudaiwa kukurupushwa na wapita njia akifanya mambo yasiyoeleweka kwenye kaburi la aliyekuwa msanii maarufu nchini, Steven Kanumba, maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Shuhuda mmoja aliyedai alikuwa miongoni mwa waliomkurupusha bibi huyo kwenye kaburi la Kanumba akiwa mtupu, amesema alipigwa na butwaa baada ya kumuona bi kizee huyo katika kaburi hilo na baadaye akamuona tena maeneo ya Mwananyamala Mchangani, nje ya nyumba namba MWL/MCH/49 akiwa amezingirwa na kundi la watu lililokuwa likitaka kumchoma moto wakidai ni mwanga.

BIBI AJIELEZA, AJICHANGANYA
Bibi huyo, akiwa amezingirwa na umati wa wananchi wenye hasira kali, alipotakiwa ajieleze alikotokea, alijichanganya kwani jibu lake la kwanza alidai ameanguka kutoka angani akitokea Tabora.

Alipozidi kubanwa kwa maswali, alibadili kauli na kusema alianguka akiwa safarini kutokea Tanga, kauli zilizowapandisha hasira wananchi wenye imani potofu za ushirikina, wakiongozwa na dada mmoja aliyejitangaza kuwa amepandisha mashetani na kudai eti bibi huyo ni mwanga kwa mujibu wa mashetani yake.

MASHETANI YACHOCHEA HASIRA
Mashetani ya dada huyo yalizidi kuwaongeza hasira wananchi hao wenye imani za kishirikina ambao walianza kukusanya vitambaa na makaratasi ya maboksi huku wengine wakianza kutafuta mafuta ya taa ili wamwagie kisha wamchome moto bibi kizee huyo, ndipo walipotokea wasamaria wema waliomuokoa na kumkimbiza Kituo cha Polisi cha Mwananyamala Mwinjuma.

“Ilikuwaje bibi kama huyu akurupushwe na kundi la watu kwenye kaburi la Kanumba halafu wamkose na baada ya muda aonekana hapa? ni lazima kuna kitu,” alisikika akisema shuhuda mmoja eneo hilo.

POLISI WANENA
Kufuatia tukio hilo, siku iliyofuata mwanahabari wetu alifika kituo cha polisi alichokimbizwa bibi huyo ili kupata ukweli zaidi ambapo askari mmoja aliyekutwa kituoni hapo, aliyeomba jina lake lisiandikwe kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo, alikiri kupokelewa kwa kikongwe huyo.

“Ni kweli bibi huyo aliletwa hapa kituoni saa tisa usiku lakini kulikuwa hakuna kosa lolote la jinai tuliloona kuwa anastahili kufunguliwa mashitaka. Jeshi la polisi haliamini ushirikina, baada ya watu kutawanyika na kuona kuna usalama tulimuachia, tumefarijika kuona wananchi hawakujichukulia sheria mikononi, waendelee kufanya hivyo.” alisema askari huyo.

WALICHOSEMA MADAKTARI
Marehemu Kanumba alifariki Aprili 7, mwaka huu Sinza, Vatican jijini Dar es Salaam ambapo madaktari bingwa watano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili walioufanyia uchunguzi mwili wake, walisema kifo hicho kilitokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo ulioathiri mfumo wa upumuaji, hali ambayo kitaalamu huitwa Brain Concussion.

Kanumba alizikwa Aprili 10, mwaka huu katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na mazishi yake kuhudhuriwa na maelfu ya watu wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilali.
Kifo cha ghafla cha msanii huyo kimezua gumzo sehemu mbalimbali nchini kutokana na kupendwa na mashabiki wake wengi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...