Saturday, April 28, 2012

LICHA YA KUUMWA: Sajuki aingia mzigoni...



Licha ya kwamba afya ya msanii wa filamu za Kibongo, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ bado hairidhishi kutokana na maradhi yanayomsumbua, juzikati staa huyo na mkewe Wastara Juma walinaswa ‘lokesheni’ wakiendelea kurekodi filamu yao.

Paparazi wetu aliwanasa wanandoa hao wakiwa na baadhi ya wasanii maeneo ya Tegeta jijini Dar ambako walikuwa wakishuti filamu iliyopewa jina la Wakili huku Sajuki akiwa ndiye muongozaji.

Akizungumza, Sajuki alikiri kuwa afya yake bado siyo nzuri lakini ameona badala ya kukaa ndani ni vyema akajishughulisha ili kukabiliana na ugumu wa maisha.

“Bado hali yangu si nzuri lakini kama mtu unaumwa na huna kitu kingine cha kukusaidia katika maisha lazima uwajibike, naumwa lakini siwezi kukaa nyumbani kwa sababu kila dakika moja ya maisha yangu inahitaji fedha,” alisema Sajuki.


Naye Wastara alisema kuwa, afya ya mumewe bado hairidhishi ndiyo maana wameamua kuingia mzigoni ili kuhakikisha wanapata fedha kwa ajili ya matibabu.

 “Kama unavyomuona mume wangu, kimsingi anaumwa na zinahitaji fedha kwa ajili ya matibabu yake na kujikimu pia, ndiyo maana unatuona tumeamua kuendelea na shughuli zetu za kisanii kwani bila kufanya hivi tutakwama katika mambo mengi.


“Hata hivyo, bado tunahitaji msaada ili tuweze kufanikisha matibabu ya Sajuki ambaye tunatarajia kumpeleka India haraka iwezekanavyo,” alisema Wastara.


WADAU TUMSAIDIENI SAJUKI
Kufuatia hali ilivyo, wadau tujitokeze kumchangia Sajuki fedha kwa ajili ya matibabu kupitia simu ya mkononi kwa kutuma kwenye Tigo Pesa namba 0713 666 113 au kwenye akaunti namba 050000003047 katika Benki ya Akiba Commercial yenye jina la Wastara Juma Issa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...