Thursday, August 25, 2011

Unamfumania mpenzi wako lakini hauko tayari kumkosa, ufanyeje?



Nimemfumania, kaamua kunipotezea
Swali:Niliwahi kuwa na mpenzi wangu lakini siku za hivi karibuni nilimfumania na rafiki yangu laivu wakiwa katika mazingira yanayoonesha kuwa walikuwa wakifanya mapenzi.

Baada ya kumnasa niliumia sana hasa kutokana na maelezo yake ya awali kwamba, angenipenda daima na kamwe asingenisaliti.
Cha ajabu baada ya tukio hilo, kutokana na kukasirishwa nikaamua kumpotezea nikijua angenitafuta na kuniomba msamaha.

Cha ajabu tangu siku hiyo na yeye akawa hana ‘taimu’ na mimi kama mtu ambaye hajuti kwa kitendo alichokifanya na wala hajuti kunikosa. Mimi nampenda sana na nahisi siko tayari kumkosa. Nimtafute nimwambie kuwa yaliyopita nimesamehe tuendelee na uhusiano wetu au nimuache tu? Nisaidie katika hili Anko.

Jibu:Kwanza kabisa kitendo alichofanya huyo mpenzi wako kinaonesha wazi kwamba, hana mapenzi ya dhati na wewe na kama utang’ang’ania kuendelea kuwa naye, ipo siku atakuja kukuumiza zaidi ya hapo.

Kama ni mtu anayekupenda, angeonesha kujutia kosa lake na hapo ningeweza kukushauri umsamehe kisha umpe nafasi nyingine lakini kama kaamua kuuchuna, sioni sababu ya wewe kumtafuta. Muache na hata kama itakuwa ndiyo moja kwa moja amini kwamba huyo hakupangwa kuwa mumeo. Wako yuko njiani.

Wivu wa mpenzi wangu
 unatishia amani ya penzi letu
Swali: Anko Shalua, mpenzi wangu ana wivu sana, inafika wakati naona ni kero kwangu kwani wivu wake umepitiliza. Je, ni kweli wivu una nafasi katika mapenzi?

Je, kuna faida zozote za wivu huu ambao wakati mwingine hutishia amani ya penzi letu? Kama zipo naomba unisaidie ili nijue nisimchukie mpenzi wangu kwani huenda ana nia njema ni tatizo la mimi kutomuelewa tu.
Mohammed R.
Kibamba.

Jibu:Huko nyuma nilishawahi kuandika makala iliyokuwa inahusu wivu na nafasi yake katika mapenzi. Nikasema kwamba, wivu katika uhusiano wa dhati una nafasi kubwa na nikaongeza kuwa, endapo utaingia kwenye uhusiano na mtu na akaonesha kutokuwa na wivu kabisa na wewe, huyo penzi lake kwako litakuwa na walakini.

Hata hivyo, niseme tu kwamba kila kitu kikizidi kiwango kinakuwa na madhara, wazungu wanasema ‘everything too much is harmful’.Wivu nao ukizidi sana ni tatizo na kweli inaweza kuwa sababu ya nyie kuachana. 
Kwa kifupi wivu usio wa kupitiliza una
faida kama zifuatazo;

Kwanza inaonesha kujali. Sote tunaamini pasipo na wivu hata chembe, hapana mapenzi ya dhati. Mpenzi wako anapoonesha wivu kwako anakujulisha ni kiasi gani anakujali na kukupenda na kwamba wewe ni mtu maalum sana kwake.

Jamani, mahali penye mapenzi yasiyo na wivu hata kidogo, panatia shaka! Na mara nyingi majibu yake ni kutokuwa ‘sirias’ katika uhusiano huo au huenda kuna kupitisha muda tu na kwamba labda hakuna ‘future’ na mpenzi huyo au ni dalili ya kuchuja kwa penzi.

Pili, inadhihirisha kwamba anathamini uhusiano wenu. ‘Siyo kama sikuamini mume wangu, bali wivu wangu kwako ni katika kuuthamini uhusiano wetu, mimi na wewe ni umoja wenye thamani kubwa, tusiruhusu kuuchezea nje yetu!  Huu ni mfano wa ujumbe unaoonesha maana na nafasi ya wivu katika uhusiano wa kimapenzi.

Tatu, ni katika kukumbushana. Kauli au matendo yanayoashiria kumuonesha wivu mpenzio yanasaidia kwa kiasi kikubwa kumfanya asijisahau katika jukumu la kulienzi penzi lenu hata akiwa mbali ya upeo wa macho yako.

Nne, ni kujijengea heshima. Kwa namna moja au nyingine, wivu pia huweza kukujengea heshima. Kwa mfano mume mwenye wivu na mkewe hujijengea heshima ya kwamba kweli anamjali na kumpenda mkewe lakini pia anaweka mazingira ya kutosumbuliwa kwa mke wake huyo kumjengea heshima yake kama mke wa mtu.

Tano, inasaidia kubadilisha tabia. Ukiwa na wivu, unaotokana na mavazi tatanishi anayopendelea kuvaa mpenzi wako kwa mfano, huenda ikasaidia kubadili tabia yake.

“Ni kweli umependeza na umetoka ‘chicha’ ile mbaya mpenzi, lakini mh! Naogopa wanaume wakware watakusumbua honey, unaonaje ukavaa simpo tu?” Kama anakupenda huenda akabadilika kidogo na hivyo ‘vivazi vyake.

Niliyoyaeleza hapo juu ni baadhi tu ya faida za wivu.Kwa maana hiyo isifike wakati ukamchukia mpenzi wako kwa kuonesha wivu kwako. Yawezekana anafanya hivyo kwa lengo la kuboresha na si kuharibu uhusiano na  kutokuelewa kwako ndiko kunakufanya uone ni kero.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...