Thursday, August 25, 2011

Dead Sea: Bahari ambayo mtu hawezi kuzama

Mtu akielea juu ya maji ya Dead Sea

SI rahisi kuamini kwamba kuna bahari au ziwa lolote duniani ambapo mtu akiingia hawezi kuzama.  Lakini, kwa waliowahi kufika Mashariki ya Kati na kuiona bahari inayojulikana kama Dead Sea,

 wakajaribu kuingia katika maji yake au kuwaona watu waliokuwa wakielea katika maji hayo huku wakisoma magazeti,  wanaamini tangu siku hiyo.

Inaitwa Dead Sea ambapo tafsiri yake kwa Kiswahili ni “Bahari Iliyokufa”.  Iliitwa hivyo kutokana na ukweli kwamba maji yake yana chumvi nyingi mno kiasi kwamba si rahisi kwa viumbe vyenye uhai kuishi katika maji yake.

Kwa Kiarabu, bahari hiyo inaitwa “al-Bahr al-Mayyit” na kwa Kiyahudi inaitwa “Yam Ha-Mela”  yote yakimaanisha “Bahari ya Chumvi”.

Ifahamike pia kwamba pamoja na eneo hilo la maji kuitwa bahari, kwa kweli ukubwa wake ni kama ziwa la kawaida tu.

Bahari hiyo ambayo pia huitwa Salt Lake yaani “Bahari ya Chumvi”, iko katikati ya Jordan kwa upande wa Mashariki.Upande wa Magharibi inapakana na Israel na Ukingo wa Magharibi (Palestina).

Uso wake na kingo zake ziko mita 422 chini ya usawa wa bahari, ambacho ni kipimo cha chini zaidi katika uso wa dunia katika eneo lililoko katikati ya ardhi kavu.

Ikiwa moja ya bahari au maziwa yenye chumvi nyingi zaidi, Dead Sea maji yake yana chumvi kwa asilimia 33.7, japokuwa maziwa Assal lililoko Djibouti na maziwa ya McMurdo Dry Valleys eneo la Antarctica (kama vile Don Juan Pond) yana viwango vya juu zaidi vya chumvi.

Dead Sea ina kiwango cha chumvi ambacho ni mara 8.6 zaidi ya kile kilichomo katika bahari.  Hivyo, wingi huo wa chumvi ni moja kwa moja hauwezi tena kuruhusu viumbe hai kuishi ndani yake, na ndiyo maana ikaitwa Bahari Iliyokufa.

Hata hivyo, kuna aina fulani za bakteria na mimea ambayo huweza kuishi katika maji hayo.   Kwa kifupi, mazingira ya Dead Sea yako sawa kabisa na ziwa liitwalo Great Salt Lake lililoko Utah, nchini Marekani.

Urefu wa ziwa hilo ni kilomita 67 na upana wake (katika sehemu ndefu zaidi) ni kilomita 18, na mto pekee unaomwaga maji ndani yake ni Mto Jordan.

Uzito wa maji yake ni kilo 1.24, jambo ambalo linafanya uogeleaji ndani yake kuwa mgumu, lakini maji hayohayo hutoa burudani tosha.  Mtu unaweza ukajilaza juu yake ukabaki unaelea muda wote huku ukisoma gazeti au ukinywa bia!

Maajabu ya bahari au ziwa hilo, ambalo katika Biblia, linatajwa liliwahi kuwa makimbilio ya Mfalme Daud (David)  ni kwamba imekuwa ikivutia maelfu ya watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani. 

Ilikuwa pia ni moja ya vituo vya mwanzo duniani vya tiba tangu enzi za mfalme “Herod the Great”.

Miongoni mwa bidhaa zinazopatikana katika bahari hiyo ni chumvi za aina ya “potash”, mbolea, madawa ya kuhifadhia viumbe visioze, na kadhalika.

Nadharia zilizopo ni kwamba kiasi cha miaka milioni tatu iliyopita kile ambacho leo ni bonde la Mto Jordan, Dead Sea na Wadi Arabah lilikuwa  kila mara linafurika maji kutoka Bahari ya Mediterranean.  Maji yaliyokuwa yakifika huko kutokea kupitia Bonde la Jezreel. 

Mafuriko hayo yalikuwa yakilikumba eneo hilo na kutoweka kufuatana na mabadiliko ya hali ya hewa. 

Matokeo yake ni kwamba ziwa ambalo lilikuwa katika eneo la Dead Sea, ambalo liliitwa “Ziwa Sodoma”, lilibakia na marundo ya chumvi ambayo unene wake ukafikia kilomita tatu.

Hivyo, baada ya mafuriko hayo kukoma, eneo hilo likabaki na maji na chumvi katika kile kinachojulikana leo kama Dead Sea.

Kama ilivyotajwa mwanzoni, bahari hiyo imekuwa ni kituo kikubwa cha tiba kwa magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na magonjwa ya ngozi ambapo walioathirika huoga maji yake,

wakaishi kwa muda sehemu hiyo ambayo  iko chini ya usawa wa bahari, jambo ambalo hupunguza ukali wa mionzi ya madhara ijulikanayo kama “ultraviolet”.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...