Tuesday, August 16, 2011

KIBABU CHA LOLIONDO HATIMAYE KORTINI



Baadhi ya wagonjwa  wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi waliokunywa kikombe cha Mchungaji Ambilikile Masapile (pichani) mwaka huu katika Kijiji cha Samunge, Loliondo mkoani Arusha hatimaye wameamua kumburuza mahakamani  kiongozi huyo kwa madai kwamba dawa yake haitibu kabisa na wamedanyanywa.

Wakizungumza nyakati tofauti wiki iliyopita kwa sharti la kutoandikwa  majina yao, watu hao ambao wako katika Muungano wa Vyama vya Watu  Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (TANOPHA) walisema kwamba wao ni kati ya waathirika waliopelekwa na chama chao Samunge kupata tiba lakini cha ajabu ni kwamba tangu  wanywe dawa hiyo wamekuwa wakipimwa hospitalini na kuonekana kuwa bado  wana virusi vya ugonjwa huo.

Waliendelea kusema kwamba  kila wakienda kupima ili waone kama wamepona, wamekuwa wakielezwa na daktari kwamba  hakuna mabadiliko na kikombe hakijawasaidia lolote lile, hivyo  wameona ni udanganyifu na utapeli mkubwa hivyo wameamua  kumfikisha mahakamani wakati wowote.

“Hatuwezi kupoteza muda na fedha  zetu kwa kwenda kunywa dawa  ambayo haitibu, hii ni kuwarubuni  wananchi, wengi wameuza mali zao, wengine  kutumia akiba ya fedha walizokuwanazo kwenda Loliondo wakijua kwamba wangepona lakini cha kushangaza ni kwamba baadhi yetu wanakufa.

“Wengine wako mahututi baada ya  kupewa kikombe, tulikuwa na matumaini ya kupona hadi tuliacha kutumia vidonge vya kurefucha maisha vya ARV, hatuna mengi  zaidi  ila  tunaomba umtafute  mwenyekiti  wetu  akueleza zaidi,” alisema mmoja wa wanachama hao.

NIA YA MWENYEKITI WA TANOPHA
Mwenyekiti wa TANOPHA, Julius Kaaya  alipotafutwa kwa njia ya simu juzi ili  kueleza madai hayo ya wanachama  wake, alisema kwamba ni kweli  walipelekwa watu 14 kwenda  kunywa dawa Loliondo lakini hakuna hata mmoja aliyepona kwani kila  wanapopimwa hospitalini  wanaonekana bado wana virusi.

“Nakumbuka kwamba kipindi  tunaenda huko Loliondo Machi, 19 mwaka huu tulifanya mkutano na waandishi wa habari, tulifika Samunge Machi 22, ambapo Machi 24 walikunywa dawa hiyo kila mmoja  akiwa na matumaini ya kupona, baada ya siku 20 tangu wanywe dawa hiyo walienda hospitali kuangalia  kama wamepona, daktari aliwaambia  hakuna hata mmoja aliyepona, “ alisema Kaaya.

Aidha, aliendelea kusema kwamba  wanachama hao hawakukata tamaa ,   baada ya siku 90 walirudi tena hospitalini kuangalia kama kuna hauweni, daktari aliwapima na kuwaambia hakuna mabadiliko hata kwa mtu mmoja.
Aliendelea kusema kwamba  wanachama hao baada ya kuelezwa  hivyo walikata tamaa na kuamua  kuendelea kutumia ARV.

“Wengi ambao tunajua kwamba  wana HIV na walikunywa kikombe  wanapukutika na hata juzi tulihudhuria  mazishi ya mmoja wapo, hii dawa  haitibu kwani kuna wagonjwa wa kisukari ambao waliinywa hawajapona .

“TANOPHA ina vyama 230 vilivyosajiliwa na mimi ndiye  mwenyekiti wao, nimekuwa nikipokea taarifa za baadhi ya wanachama wetu  waliokwenda Samunge ambao waliacha kutumia ARV wakijua kwamba wamepona, wengi  wamefariki.

“Babu wa Loliondo amedanganywa  na  shetani na siyo kwamba  alielezwa na Mungu, nashangaa viongozi wa dini wanaompigia debe  wakati wao siyo wataalamu  wa kujua kama dawa hiyo inaponya  au la, ni ushabiki wa kidini usiokuwa na maana, lengo lao ni kuchuma fedha kwa wagonjwa.

Kwa nini wasiwaachie wataalamu kushughulikia  suala hilo?
“Wanasiasa waliokunywa dawa hiyo na kupigwa picha na vyombo vya habari walihamasisha wananchi   kwenda huko kunywa dawa, hawakupaswa kufanya hivyo, wao kama viongozi wangesubiri  kwanza wapate matokeo ya utafiti wa Wizara  ya Afya.

“Ni kiongozi gani aliyejitokeza na kuonyesha cheti chake hadharani  mbele ya vyombo vya habari kwamba amepona, wanaona aibu, ile siyo dawa ni maji tu.

“Wizara ya Afya nao wameingiliwa na wanasiasa ambao wamekuwa wakidai  kwamba inatibu wakati Waziri wa Afya  kwa upande wake anasema  kwamba  dawa ya Ukimwi bado haijapatikana  duniani.

“Wizara inasema bado wanaendelea  kuifanyia uchunguzi hiyo dawa ya Masapile,mpaka lini? Watutajie wangapi walikunywa maana mpaka sasa hakuna  idadi kamili, kwa kweli  wengi  wamefariki ,wengine wako hoi, nawashauri wasiache kutumia ARV.

“Wanaoishi na virusi wasione  aibu  wajiamini watumie ARV, watambue kwamba ni tatizo limeshawapata na  wakifanya hivyo bila kuwa na hofu  wanaweza  kuishi miaka mingi,” alisema Kaaya.

Alipoelezwa kuwa kuna watu waliokunywa kikombe wanataka kumfikisha mahakamani Mchungaji Masapile, Kaaya alisema hata yeye yupo tayari endapo atampata mtu wa kumsaidia kufungua kesi.

“Masapile ameharibu taifa, ingekuwa kesi inafunguliwa bure kwa kweli ningeshafanya hivyo na kama wanachama wangu wameamua kumfikisha kortini,  nawaunga mkono,” alisema Kaaya.

MCHUNGAJI MTIKILA
Naye Mchungaji wa Kanisa la Full Salvation, Christopher Mtikila kwa upande wake amesema kwamba dawa hiyo haitibu na analishughulikia suala hilo ili kumfikisha mahakamani pamoja na mawaziri, wabunge na viongozi wa  juu waliokunywa kikombe.

“Mawaziri hao wamewahamasisha wananchi kwenda Loliondo kunywa dawa, lazima tuwashitaki pamoja na viongozi wa dini waliopiga debe,” alisema Mtikila. Viongozi wa dini waliohamasisha ni Askofu Thomas Laizer na Martine Shayo.

Baadhi ya Mawaziri waliopata kikombe ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli.Wabunge ni Augustine Mrema, Edward Lowassa na wakuu wa mikoa ni Yohana Balele na Abbas Kandoro.

MAJIBU YA BABU KWA WASIOPONA
Mwandishi wetu wa Arusha wiki iliyopita alizungumza na msaidizi wa Mchungaji Masapile kwa njia ya simu, Paulina Lucas na kuulizwa kuhusu malalamiko hayo akasema wasiopona ni wale ambao hawana imani.

“Kama hawajapona siyo makosa yetu. Tuliwaambia kabla kuwa katika tiba hii kigezo cha kwanza ni kuwa na imani na hapa tuna uthibitisho wa kutosha wa watu walioponywa na maajabu ya dawa hii wakiwemo wagonjwa wenye Ukimwi,” alisema Paulina.

Alidai kuwa kuna baadhi ya watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi si wakweli kwani kuna uwezekano kuwa wamepona lakini wanashindwa kuweka wazi kwa malengo ya kukosa fedha wanazopewa na wafadhili.   

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...