Saturday, August 13, 2011

MSHIRIKI WA J.K ANYONGWA

Mkurugenzi wa Kampuni ya Muyabi Publishers, Richard Masatu enzi za uhai wake.

Jiji la Mwanza limepata mshtuko mkubwa kutokana na msiba mzito wa kifo cha Mkurugenzi wa Kampuni ya Muyabi Publishers, Richard Masatu ambaye ni mshirika mkubwa wa Rais Jakaya Kikwete mkoani humo.

Masatu ambaye kampuni yake ndiyo mchapaji wa Gazeti la Kasi Mpya, inadaiwa amenyongwa na kutupwa mtaroni ingawa taarifa kamili ya kipolisi bado inangoja uchunguzi.

Enzi za uhai wake, Masatu alipata kuwa swahiba wa JK pamoja na mfanyabiashara wa kimataifa Bongo, Rostam Aziz, pia anatajwa kuwepo kwenye mtandao uliofanikisha Uchaguzi Mkuu 2005.

Masatu, alishiriki tena kwenye Uchaguzi Mkuu 2010, hivyo enzi za uhai wake alikuwa kiungo muhimu wa kufanikisha ushindi wa urais wa JK, huku karata yake ikisomeka turufu mkoani Mwanza.

TAARIFA YA KIFO CHAKE
Masatu alifariki dunia Agosti 8, 2011 kwa kile ambacho wakazi wengi wa Jiji la Mwanza wanaamini kwamba alinyongwa na watu wenye kisasi naye.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Masatu alihudhuria ufungaji wa maonesho ya kilimo, Nane Nane kwenye eneo la Nyamhongolo, Igoma, Mwanza.

Habari zinasema kuwa baada ya kutoka Nyamhongolo kwenye maonesho hayo, Masatu aliongozana na marafiki zake, wakiwemo baadhi ya viongozi wa Jiji la Mwanza pamoja na mwandishi mmoja wa habari (majina tunayo) hadi kwenye Hoteli ya Cross Park.

Baadaye, Masatu na wenzake walihama kutoka hotelini hapo na kutua majeshi kwenye Baa ya Ndama, Igoma.
Gazeti hili linashibishwa ‘data’ kwamba wakiwa hapo huku wakipata ‘kilaji’, mara kwa mara Masatu alikuwa anatoka na kwenda kuzungumza na simu pembeni bila kuwataarifu wenzake.

Chanzo chetu kilipasha: “Inaonekana alikuwa anazungumza na watu, halafu inaonekana hakupenda wale marafiki zake wajue alikuwa anazungumza nini.

“Ndiyo maana alikuwa anatoka mara kwa mara nje ya baa kuzungumza na wale watu kwenye simu. Mara ya mwisho alipotoka hakurudi tena.”
Mtoa habari wetu aliongeza kuwa watu waliokuwa na Masatu kwenye baa hiyo, walimngoja mpaka wakachoka kabla ya kuamua kuondoka.

Aliendelea kusema kuwa usiku wa siku hiyo (Agosti 8), Masatu alikutwa amelala barabarani akiwa hajitambui kwenye Barabara ya Nyerere (Mwanza-Musoma) jirani na Baa ya Ndama.
Habari zinasema kuwa vijana waliomuokota Masatu, walimchukua na kumkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.

Alipofikishwa hospitalini hapo, alipatiwa matibabu lakini ilipofika Jumatano saa 8:00 usiku (Agosti 10) alifariki dunia.

KAULI YA MKE WA MASATU
Edna Masatu ambaye ni mjane wa marehemu, aliliambia gazeti hili nyumbani kwake juzi (Jumatano) saa 2:00 asubuhi kuwa kuna mtu alikuwa akimpigia simu marehemu mume wake na kumtolea lugha za matusi na vitisho.

Mke wa marehemu, Eda Masatu akiwa na huzuni.
“Tulikuwa tunazungumza
Nilipomuuliza zaidi akaniambia ningoje akirudi nyumbani atanisimulia.

“Baada ya hapo nilitulia nikimngoja arudi nyumbani lakini muda ulikwenda bila yeye kurudi. Ikabidi nimpigie tena simu, wakapokea watu wengine, wakaniambia mume wangu amepata ajali, kwa hiyo wanampeleka Sekou Toure.

“Nilifika Sekou Toure, nilimkuta mume wangu yupo hoi. Kwa bahati aliponiona alinitambua, akaniambia nimshike kifuani, baada ya hapo hakuzungumza neno lingine tena. Hilo ndilo lilikuwa neno la mwisho kwa mume wangu,” alisema Edna.

Aliendelea kusema: “Nilifanikiwa kumkagua mume wangu, nikagundua alikuwa na jeraha kubwa chini ya kidevu, mguu wa kulia ulivunjika, wa kushoto ulikuwa na jeraha, mkono wa kushoto ulichubuka, pia jicho la upande wa kushoto lilivia damu.”

KIFO TATA
Edna alisema kuwa walikwenda polisi kuripoti tukio la mume wake kwamba alipata ajali lakini kituoni kesi ilibadilika.

Alisema, polisi walieleza kwamba hakukuwa na tukio la ajali lililofahamika, kwa hiyo ikaamuliwa kuandikwa ni Kifo cha Mashaka.

Kwa mujibu wa Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) wa Mwanza, Deusdediti Nsimeki, maelekezo ya kufungua jalada la Kifo cha Mashaka yalifuata baada ya kuwepo kwa malalamiko ya awali kutoka kwa marehemu juu ya watu waliokuwa wanamsumbua kutokana na maisha yake katika tasnia ya habari.

Nsimeki alisema, alishakutana mara kadhaa na marehemu katika maeneo ya nje ya kazi, hivyo akaongeza kwamba kuna uwezekano wa kuwepo jambo lililojificha kuhusu kifo hicho.

Alisema, uchunguzi utafanyika na itabainika sababu ya kifo cha marehemu. Jalada limewekwa kwenye Kitabu cha Ripoti za Kipolisi (Report Book ‘RB’) nambari MW/RB/7430/2011 na MW/IR/5555/2011 KIFO CHA MASHAKA.

MWANZA WAMLILIA
Watu mbalimbali mkoani Mwanza wamemlilia Masatu kuwa alikuwa mtu mcheshi na kulitaka jeshi la polisi lifanye uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake.

“Yule alikuwa mpambanaji, kuna suala la migogoro ya kisiasa kwa sababu yule jamaa alikuwa anatofautiana na wengi. Alikuwa na maadui wengi wa kisiasa, kwa hiyo wengi tunaamini ameuawa.

“Inauma kwa sababu alikuwa na mchango mkubwa kwa nchi yetu. Alianzisha chombo cha habari kwa lengo la kuitumikia nchi yake katika eneo la habari,” alisema Kibendera Ngosha wa Mabatini, Mwanza.

Mama wa marehemu akilia kwa uchungu, hapa akipewa pole na Mwenyekiti wa eneo hilo.

Lucy Masanja wa Nyakato Mecco, Mwanza alisema: “Yule baba alikuwa mtu mzuri sana, tunamlilia kwa sababu ni ngumu kupata mtu mcheshi kama yule, alikuwa na tabia ya kushirikiana na watu na hakuwa mtu wa kujikweza.”
Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...