Thursday, August 25, 2011

MTOTO ALIYEISHI NA NYANI AFANYA MAAJABU

MTOTO  Baraka  Bahati  Rose (14), (pichani) aliyeishi  na  nyani  porini  kwa  kipindi  cha  miaka  mitano  na  kuokolewa na maofisa wanyama  pori,  amebadilika  na sasa anaonesha maajabu katika kusakata soka na pia kufanya vizuri darasani.

Mwalimu mmoja wa Shule  ya  Msingi Kimanga,  Wilayani Ilala  jijini Dar es Salaam  aliyejitambulisha  kwa  jina la Christina, aliliambia gazeti hili wiki iliyopita kuwa Baraka amekuwa akifanya vizuri na kucheza mpira kitaalamu zaidi, hali inayomfanya apendwe na walimu na wanafunzi.

“Baraka anajitahidi sana  na  siyo  katika  masomo tu  bali hata   katika  mchezo  wa mpira  wa  miguu, ni staa na anapenda  kujisomea, amekuwa  akifanya vizuri sana hasa katika masomo ya Sayansi,” alisema Mwalimu Chris.





Baadhi   ya  wanafunzi wanaosoma  katika  shule hiyo   waliliambia  gazeti  hili   kwamba,  Baraka  ambaye yupo Darasa la Nne kwa  sasa amebadilika  kwa  asilimia  kubwa   katika   masomo  ya  Sayansi  na amekuwa   akicheza   mpira wa miguu vizuri kuliko wenzake.

“Tunapocheza mpira wa miguu na kuchagua timu, kila mtu anapenda awe katika timu yake,” alisema mtoto mmoja wa kiume aliyejitambulisha kwa jina la Said.

Wanafunzi  hao  walisema kuwa Baraka amekuwa akiwapenda wenzake tofauti na awali  ambapo  alikuwa  haongei  vizuri Kiswahili   na  hakuwa  na  uhusiano  mzuri   na  wanafunzi wengine.





Mtoto Baraka  aliokolewa  na  maafisa  wanyama pori miaka kadhaa  iliyopita  katika  pori  la Usangu, Wilaya ya Bukombe,  Shinyanga  baada ya askari hao kumuua nyani  aliyekuwa akimtunza porini.

Mwenyekiti wa Serikali ya  Mtaa  wa  Kimanga, Pastor  Kyombia  kwa  kushirikiana na mlezi wa Baraka  aitwaye  Rose Mbwambo wamekuwa  wakimtunza mtoto  huyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...