Monday, August 1, 2011
Tiba ya kikombe serikali yasema haitibu...
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda amepasua jipu na kusema hakuna utafiti wowote wa kisayansi uliothibitisha kuwa dawa za asili zina uwezo wa kutibu Ukimwi.
Kauli hiyo ilitolewa na waziri huyo wakati anazindua Kituo cha Matibabu ya Wagonjwa wa Ukimwi na Mafunzo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Waziri Mponda ameyasema hayo huku maelfu ya watu wakiwa tayari wamekunywa tiba ya mitishamba ya vikombe inayotolewa na watu mbalimbali akiwemo mwanzilishi wake, Mchungaji Ambilikile Masapile, maarufu ‘Babu’ wa Kijiji cha Samunge, Loliondo aliyedai kuoteshwa na Mungu kutibu magonjwa sugu ukiwemo Ukimwi.
Magonjwa mengine aliyotaja kuwa yanatibika kwa mitishamba kwa dozi ya kikombe kimoja ni kisukari, shinikizo la damu, kifafa pamoja na magonjwa mengine yanayosumbua katika tiba za kisayansi.
DAWA ZA KUREFUSHA MAISHA
Dk. Mponda alisema wagonjwa wa Ukimwi wanatakiwa kutumia dawa za kurefusha maisha (ARV) na akawataka waende kwenye vituo vya afya kupewa.
Aliongeza kuwa vituo vyote vya afya vinatoa dawa za ARV lengo likiwa ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye tatizo la Ukimwi anapata dawa hizo mahali alipo.
Alisema kuna vituo 50 vya afya ambapo 30 ni vya serikali na 20 ni vya watu binafsi ambavyo vinatoa msaada kutoka kwa wadau wa maendeleo.
“Wagonjwa wanaokwenda kupata tiba asili waache kwa kuwa bado zinafanyiwa utafiti,” alisisitiza waziri na kuzua minong’ono kutoka kwa watu waliokuwa wakimsikiliza wakisema ina maana waliokunywa wamejisumbua.
Akifafanua zaidi, Waziri Mponda alisema dawa hizo za mitishamba zinafanyiwa utafiti katika Hospitali ya Muhimbili na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Aliongeza kuwa kuna waathirika 110,000 wanaoishi na virusi vya Ukimwi na kati yao 72,000, wanaendelea kutumia dawa za ARV na kwamba hayo ni maendeleo katika kupambana na ugonjwa huo.
TAHARUKI
Tamko hilo la Waziri Mponda limesababisha taharuki kubwa kwa baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakipiga simu katika ofizi za gazeti hili wakidai kuwa serikali imechelewa mno kutoa tamko hilo.
“Watu wengi wameuza mali zao ili waweze kutibiwa kwa mitishamba inayotolewa kwa kikombe sehemu mbalimbali nchini, serikali inapojitokeza sasa na kusema haitibu, inatushangaza, wengi wameumia tayari,” alisema mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la John, mkazi wa Arusha.
Mara baada ya tiba hiyo ya Babu kutangazwa, mawaziri, baadhi ya wakuu wa mikoa, makamanda wa jeshi na wananchi walifurika kwa mzee huyo na watoa tiba wengine wa vikombe huko Tabora, Morogoro, Mbeya na Iringa kupata dawa.
Baadhi ya mawaziri, waliokunywa dawa hiyo ya mitishamba ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira na wabunge Nimrodi Mkono (Musoma Vijijini) na Augustine Mrema (Vunjo), Rose Nyerere, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yohana Balele na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro.
ASILI YA DAWA YA BABU
Mchungaji Masapile aliwahi kuulizwa kuhusu asili ya tiba yake, akasema : “Asili ya dawa hii ni Mungu mwenyewe, mti ni wa kawaida kama miti mingine ila Mungu ameweka neno lake ndani ya mti, hivyo neno ndilo linaloponya.”
Hakuishia hapo, alisisitiza kuwa Mungu akitoa neno lake ndani ya mti huo, basi mti hautakuwa na nguvu hiyo ya uponyaji. Hata hivyo, hadi sasa Babu hajatoa tamko kuueleza umma kuwa Mungu ametoa neno lake ndani ya mti huo au la na wananchi wachache wanaendelea kwenda kupata kikombe licha ya vifo kuongezeka kila kukicha.
WAZEE WA SAMUNGE
Aidha, baadhi ya wazee wa Samunge waliowahi kuzungumza na wanahabari kwa nyakati tofauti walidai kuwa mti huo anaotumia Babu kutibu watu una majina mawili ambayo ni Mgamryaga na Mbaghayo na walisema unapatikana kwa wingi katika Mlima Mwegari kijijini hapo.
Walidai kuwa mti huo ulikuwa ukitumika kama kinga ya kansa kwa kuuchemsha na kunywa supu yake na pia ulikuwa ukitibu baadhi ya magonjwa ya wanyama.
Lakini walitoa angalizo kuwa hapo kwao hakuna waganga wa kienyeji pengine katika jitihada ya kusititiza kwamba yanayotokea huko siyo masuala ya kishirikina kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodai.
Baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakipinga tiba hiyo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe alimuambia mwandishi wa habari hii kuwa dawa za vikombe vyote inayotolewa sasa kama tiba ni mambo ya shetani.
Alinukuu aya ya Biblia Wakorintho 1;10 msitari wa 14-22 ambayo inasema Wakristo wanaoshiriki meza ya Bwana na kukinywea kikombe cha Bwana kamwe wasishiriki kikombe cha mashetani.
“Kwa hiyo kinachofanyika Loliondo ni ushirikina na ni kazi ya pepo wa uaguzi,” alisisitiza Askofu Kakobe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment