Thursday, August 25, 2011

MASWALI 10 YA KUJIULIZA KWA WAPENZI



Mpenzi msomaji wangu, binafsi kuna wakati huwa nakaa na kujiuliza maswali mbalimbali kuhusu uhusiano wangu, yapo maswali ambayo nayapatia majibu lakini mengine naishia kuyapotezea.

Naamini siko peke yake yangu na leo nimeona niwaandikie maswali 10 ambayo kama uko kwenye uhusiano unatakiwa kujiuliza. Kumbuka sitayajibu bali majibu unatakiwa kuyatoa mwenyewe kisha kuyafanyia kazi.

1. Unaufurahia uhusiano wako?
Hili ni swali la msingi kujiuliza. Ni vizuri ukajua kama unayo furaha katika uhusiano wako. Ukibaini kwamba hauko na furaha ujue kuna tatizo na uamuzi utakuwa si kuendelea kumng’ang’ania huyo uliyenaye bali unatakiwa kumuacha.

Kumbuka maisha yaliyotaliwa na huzuni hayawezi kuwa marefu, unaweza kujikuta unafupisha maisha yako kwasababu ya mapenzi tu. Kwa maana hiyo leo hii kaa na ujiulize kama unaufurahia uhusiano wako ama laa, isiwe bora liende tu.

2. Uko tayari kwa mtoto?
Hili si kwa walioolewa/walioa tu bali hata walio katika uhusiano wa kawaida.

Uko na mpenzi wako, kaa jiulize kama unadhani ni wakati muafaka kujiachia kwake ili upate mtoto kabla ya kuoana? Ukiwa makini suala la kupata mtoto haliwezi kutokea kama ajali ni ishu ya kuamua tu.

Kama uko ndani ya ndoa pia, ni kweli mtoto ni sehemu ya furaha katika maisha yenu lakini unadhani mmejipanga kwa kulea kwa muda huu? Usifanye mambo kibubusa, jiulize kisha jibu utakalolipata ulifanyie kazi.

3. Lipi la kujibadilisha?
Chukulia kwamba umepewa nguvu ya kujibadilisha vile ulivyo. Unadhani ni kitu gani ambacho unahisi kinamkwaza mpenzi wako au kinamboa lakini huwezi kukiacha?

Naamini kipo hivyo kama utakibaini ni vyema ukakifanyia kazi hata kabla hujapewa nguvu hiyo ya kujibadilisha kwani kuendelea kuwa hivyo ni kuliathiri penzi lako.

4. Kipi kinakufanya uhisi unapendwa?
Unahisi huyo uliyenaye anakupenda? Kama ndiyo ni lazima ukae na kujiuliza sababu za kukufanya uhisi hivyo.

Unadhani ni kutokana na mambo unayomfanyia, muonekano wako au tabia zako? Haiwezekani ikawa unahisi tu kwamba huyo uliyenaye anakupenda bila sababu za msingi.

Ukishabaini yale yanayokufanya uamini kwamba anakupenda basi tia chumvi, hakikisha hutoki kwenye mstari, mtadumu.

5. Kipi kinakuchukiza sana kwa mpenzi wako
Huenda vipo vitu vingi vinavyokuchukiza kwa mpenzi wako, hilo siyo tatizo kubwa kwani huo ndiyo udhaifu tunaousema kwamba kila mmoja anao.

Huwezi kumpata mpenzi ambaye atakufurahisha kwa kila kitu, ni lazima yatakuwepo mambo kadhaa ambayo huyafanya na huwa yanakuchukiza. Katika hayo angalia moja kubwa kuliko yote kisha uanze nalo katika kukabiliana nayo.

Naamini si ya kukufanya uachane naye ila ukiyajua itakuwa ni rahisi kuyazoea kwani inawezekana naye ni vigumu kuyaacha mara moja.

6. Umejifunza nini kwenye uhusiano wako wa zamani?
Huko nyuma ulikuwa una mpenzi mkaachana kutokana na sababu mbalimbali. Sasa umempata huyo uliye naye sasa, je, umejifunza nini kutoka kwenye uhusiano wako wa nyuma?

Je, unahisi kuna ambayo ulikuwa ukiyafanya yaliyosababisha wewe kutengena na mwenzako huyo? Je uko tayari kuyarudia?
Katika hili namaanisha kwamba, kutoka kwenye uhusiano wako wa nyuma kuna mambo unayoweza kujifunza yatakayokusaidia kuboresha penzi lako la sasa na hatimaye kuweza kudumu.

7. Yapi unayoyapenda kutoka kwa mpenzi?
Kuna uwezekano mpenzi wako anakufanyia mambo yanayokufanya udate, ni yapi hayo? Kama yapo usisite kumwambia mpenzi wako ili ajue na awe anakufanyia hivyo kila siku.

Unapenda anapokutoa ‘out’? Unapenda anapokutania au anapokufanyia mambo ya kiutundu na kiuchokozi mnapokuwa faragha? Hili ni swali muhimu kwakuwa yawezekana mwenzako anafanya kwa kuwa anajisikia kukufanyia lakini hajui ni furaha ya aina gani unayoipata.

8. Anakupenda?
Hili ni swali ambalo kila aliye katika uhusiano wa kimapenzi anajiuliza. Ni lazima kila mmoja kujiuliza swali hilo kutokana na ukweli kwamba mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu.

Unaweza kukuta mtu anakufanyia mambo yanayokufanya uamini anakupenda kwa dhati kumbe hamna kitu. Ndiyo maana nikasema kwamba kila unapokaa jiulize anakupenda kweli au unatwanga maji kwenye kinu.

9. Ngono ina nafasi gani kwenu?
Ni hili na jambo linalosababisha mtafaruku kwa wapenzi wengi. Unakuta mmoja anapenda sana ngono lakini mwingine siyo kiivyo.

Wewe kama wewe jiulize kama kukutana na mpenzi wako faragha kuna umuhimu katika kuliboresha penzi lenu?

Unadhani unaweza kuishia kumwambia unampenda bila hata siku moja kumwambia unahisi kuwa naye faragha? Hilo jiulize mwenye kisha jibu utakalolipata ulifanyie kazi.

10. Penzi lenu lina maadui?
Unadhani kila mmoja anafurahia kuwaona jinsi mnavypendana au wapo ambao ni maadui  wanaotamani siku moja mtengane?

Huenda wapo na unawajua kabisa. Unadhani kwanini wanauchukia uhusiano wenu? Wanaona mnaringa au ni roho zao mbaya tu? Kwa vyovyote vile, kikubwa ni kuhakikisha huwapi nafasi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...