Tuesday, October 18, 2011

Steve Jobs: Shujaa wa dunia aliyeendeleza mfumo wa kompyuta...



•    Amefariki  wiki iliyopita
•    Alikuwa madhehebu ya Buddha
•    Baba yake alikuwa Mwislam kutoka Syria
OKTOBA 5, wiki iliyopita ulimwengu ulipoteza mmoja wa watu muhimu katika maendeleo yake.  Ni mtu aliyechangia kiasi kikubwa kuendeleza kompyuta, moja ya vyombo vya “maajabu”   katika maendeleo duniani tangu maofisi ya New York, (Marekani,  hadi vijiji vya wilayani Igunga, Tanzania.

Ni Steve Jobs, Mmarekani aliyefariki akiwa na umri wa miaka 56.  Mtu huyo alikuwa mvumbuzi na mfanyabiashara na mmoja wa wenyeviti waasisi na ofisa mtendaji mkuu wa kampuni la kompyuta la Apple Inc.

Jobs aliyezaliwa Februari 24, 1955, na ambaye hakufanikiwa kupata elimu ya chuo kikuu,  alianza kuonyesha kipaji tangu miaka ya 1970 hadi kuanzisha kompyuta maarufu duniani zinazojulikana kwa jina la Apple na Macintosh.

Alifanya hivyo kwa kushirikiana na Steve Wozniak na Mike Markkul ambapo muda mwingi wa utaalam wake alipitia makampuni ya Pixar na The Walt Disney.

Jobs alikuwa mfuasi wa madhehebu ya dini ya Buddha na alipokuwa mdogo aliasiliwa na  familia ya Clara na Paul Jobs  na kupata jina hilo la ukoo la Jobs na kuwa Steve Jobs.

Baba yake mzazi alikuwa ni Abdulfattah John Jandali, Mwislam mwenye asili ya Syria aliyehamia Marekani akiwa na umri wa miaka 18.  Mama yake alikuwa ni Joanne Simpson, Mmarekani, ambaye Steve Jobs alikuja kumfahamu ukubwani na kuamua kuwa karibu naye.

Hata hivyo, alikataa kurudiana na baba yake mzazi ambaye sasa anaishi huko Reno, Nevada, Marekani.
Alikuja pia kumgundua dada yake aitwaye Mona Simpson, msomi na mtunzi wa vitabu.  Jina lake la kuzaliwa alikuwa ni Mona Jandali.

Mwaka 1991 alimuoa Laurene Powell kwa taratibu za dini ya Buddha ambapo akamzalia watoto watatu.  
Umaskini ulimfanya ashindwe kuendelea  chuo Kikuu huko Reeds ambapo anasema: “Mambo yalikuwa mabaya.  Sikuwa na bweni la kulala, hivyo nililala sakafuni katika chumba cha rafiki yangu.  

Nilikuwa nikikusanya na kuuza chupa tupu za Coca Cola kwa ajili ya chakula.  Nikikosa hivyo nililazimika kutembea kiasi cha  kilomita nane kwenda kupata chakula kizuri kwenye hekalu la Hare Krishna mara moja kwa wiki.”

Kompyuta maarufu alizoongoza kuzibuni ni iPod, iPhone na iPad na kompyuta nyingine nyingi za michezo.
Shujaa huyo wa dunia, aliyekuwa hali nyama, akipendelea zaidi samaki, alifariki nyumbani kwake Palo Alto, California, Marekani saa tisa mchana kutokana na uvimbe kwenye kongosho uliosababishwa na kansa iliyogunduliwa miaka saba iliyopita.

Ameacha utajiri wa dola bilioni saba kwenye kampuni ya Apple Inc na watoto Reed, Erin na Eve kutoka kwa mkewe Laurene, na amemwacha binti Lisa Brennan-Jobs aliyezaa na Chris Ann Brennan hapo kabla.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...