Wednesday, October 12, 2011

HILI NDILO KANISA LA WAUZA UNGA



SINEMA imefika patamu, serikali imepanga kuwaonesha waandishi wa habari mkanda wa video wa mtandao haramu wa viongozi wa dini wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.


Wakati tukio hilo likisubiriwa kwa hamu, UTAMU inakuwa ya kwanza kulitaja kinagaubaga kanisa ambalo linaundwa na viongozi wanaojihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya.

Askofu John Said.
Uchunguzi wa Uwazi kwa kuhakikishiwa na kikosi kazi cha kudhibiti madawa ya kulevya cha Jeshi la Polisi Tanzania, umebaini kuwa Kanisa la Lord Choose Charismatic Revived ni moja ya makanisa yaliyo chini ya mtandao huo.

Kanisa hilo, lipo Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam na waumini wake ‘hupigwa domo’ kuwa kuna uponyaji lakini ndani kwa ndani, viongozi wake wanajihusisha na biashara hiyo haramu.

Askofu mkuu wa kanisa hilo, Chidi Okechuku, alishatiwa nguvuni na kikosi kazi cha kudhibiti madawa ya kulevya, hivi sasa anasubiri hatima yake kutoka kwa ‘pilato’.

Askofu Chesa Elias.

Okechuku, raia wa Nigeria, ndiye anatajwa kuwa mkuu wa mtandao wa viongozi wa dini wauza madawa ya kulevya nchini.

NI AIBU YA KANISA
Siri kwamba kanisa hilo linajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, ilibainika Machi 4, 2011 usiku wa manane.
Siku hiyo, Kamanda Nzowa aliongoza kikosi chake na kuvamia nyumba aliyopanga Askofu Okechuku, Kunduchi, Dar na kunasa idadi kubwa ya madawa ya kulevya.

Okechuku, alikutwa na kilo 81 za madawa ya kulevya aina ya Heroine.
Askofu huyo alikamatwa akiwa na wapambe wake, Hycenth Stan, raia wa  Afrika Kusini, Shoaib Mohamed, Pakistan na Paul Ikechuwi Obi wa Nigeria, wote walikutwa kwenye nyumba hiyo yenye namba 593.
Askofu Chidi Okechuku.

KANISA LAPOTEZA WAUMINI
Uwazi limebaini kuwa kutokana na kashfa hiyo, waumini wengi waliokuwa wanaabudu kupitia kanisa hilo, wameanza kupukutika.

Anatory Magesa, aliyekuwa muumini wa kanisa hilo alisema: “Wengi tumeondoka, tumehamia makanisa mengine. Ni aibu, kumbe kanisa letu ndilo kitovu cha madawa ya kulevya.”

NI MAISHA JELA
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Madawa ya Kulevya katika Jeshi la Polisi nchini, Godfrey Nzowa alisema kuwa mtu anayekutwa na hatia ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya adhabu ya juu kabisa ni kifungo cha maisha jela.

Nzowa alisema: “Tumekuwa wakali sana, tunasimamia kifungo cha maisha jela ili kukomesha biashara hii haramu. Inawezekana hakimu akapima kosa la mshtakiwa na kumhukumu miaka 30 jela lakini ukweli ni kwamba sasa hivi adhabu ya juu ni kifungo cha maisha jela.”

MAASKOFU WALIZUNGUMZIA KANISA HILO
Mchungaji wa House Prayer of Information, Kaleb Simba alisema: “Tatizo wachungaji wameacha kazi waliyopewa kufanya na kuingia kwenye tamaa za dunia.

Mchungaji Christopher Mtikila.

“Wameacha misingi ya kanisa, ukiwaona ni mbwa mwitu wakali.”
Askofu Chesa Elias wa Kanisa la Victorious, Tabata alisema: “Kuhusu hilo, binafsi nadhani hakuna msamaha kwa huyo askofu. Watumishi wanapaswa kuwa watiifu na waaminifu, kutokana na hilo, ni lazima nchi ikae chonjo kuhakikisha wote wanaoingia kuendesha masuala ya dini hapa nchini wamethibitishwa.”

Askofu John Said wa Kanisa la Victorious, Mabibo, alisema: “Nchi isifanye suala la madawa ya kulevya ni la kitoto. Kutokana na hili, lazima nchi ione madawa ya kulevya makanisani ni janga la kitaifa.”

Mchungaji Christopher Mtikila wa Kanisa la Full Salvation, Mikocheni alisema: “Sheria haibagui nchi, kwa kuwa amekamatiwa huku kwetu ni lazima sheria ya Tanzania ichukue mkondo wake. Hivi sasa wachungaji wengi ni matapeli.”

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...