Monday, October 17, 2011

BSS 2nd CHANCE: Alichotendwa Rodgers Lucas mmmh.....


                                                                Haji Ramadhan.

NO! No! No! Hapana! Haiwezekani! Hayo yalikuwa makelele yaliyosikika ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita baada ya kutangazwa mshindi wa Shindano la Bongo Star Search ‘Second Chance’ 2011, Haji Ramadhan...

Kabla ya kutangazwa kwa Haji aliyekomba Sh. milioni 40, alianza kutangazwa mshindi wa tatu, Waziri Salum ambaye alilamba Sh. milioni 5 na wa pili, Rogers Lucas aliyeondoka na Sh. milioni 10 huku mrembo pekee aliyekuwa ameingia kwenye nne bora, Bella Kombo akiambulia cheti pekee.

Awali ilielezwa kuwa Rogers ndiye aliyekuwa akikimbiza kwa kupigiwa kura nyingi hivyo baadhi ya wadau waliamini angeibuka kidedea, lakini matokeo yakawa ndivyo sivyo.

“Alichotendewa Rogers siyo ‘freshi’ kabisa. Ndiye msanii mkali kuliko wote kwani ukiachilia mbali kutunga, ana sauti nzuri na anajua kutumia vyombo vya muziki kama gitaa,” alisema mdau mmoja wakati akitoa maoni yake juu ya ushindi wa Haji.

Aliongeza: “Majaji hawakuwa ‘fea’ kwa sababu walikuwa wakiwakatisha tamaa baadhi ya washiriki na kuwapongeza ambao hawaimbi bali wanapiga makelele tu na kukata viuno.

“Kwa jumla ni kazi nzuri, lakini majaji wanatakiwa kuboresha baadhi ya vitu hasa kwenye ukosoaji. Wanapaswa kumwambia mshiriki mahali alipokosea na siyo kuponda au kusifia tu.”

Mdau mwingine aliyezungumza alisema: “Haji? Aah! Wapo wanaomkubali lakini kwa upande wangu naamini hafui dafu kwa Rogers.”

MSHINDI ALIJULIKANA KABLA
Baada ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Bench Mark Production inayoratibu shindano hilo, Rita Paulsen ‘Madam’ kupanda jukwaani, aliwataka wadau kusema mshindi ni nani ambapo katika hali ya kuonesha kuwa mshindi alijulikana kabla, kundi la watu lilijibu kwa sauti kuwa ni Haji.
Hata hivyo, Madam hakuwa na haja ya kufungua bahasha ili kuona jina la mshindi hivyo akamtangaza jamaa huyo.

VIBWEKA VYA MASTAA BONGO
Kama ilivyo ada, mastaa wa Kibongo hawakuwa nyuma katika kuonesha vibweka vyao.

LULU KAMA KAWA, FULL MCHARUKO
Staa wa filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ alizama ukumbini hapo akiwa na dada yake na kwenda moja kwa moja katika viti vya VIP.

Kama kawa, kama dawa, Lulu aliingia akiwa mpole asiye na maneno mengi, ingawa hali hiyo ilibadilika ghafla baada ya Haji kushuka  na kibao cha Dushelele cha Ali Kiba ambapo alinyanyuka na kuanza kukata mauno kimcharuko.

Badaye alichanganyikiwa kabisa alipopanda stejini msanii kutoka Nigeria, Chinedu Okoli ‘Mr Flavour’ ambapo alinyanyuka na kwenda kuchizika mbele ya steji huku akipiga mayowe ya kufa mtu.

UWOYA ASHANGAZA WATU
Irene Uwoya alishangaza watu kutokana na muda mwingi aliokuwa ukumbini hapo kuonekana akiwa ametulia kwenye kiti chake huku akiwa amejiinamia, jambo ambalo wengi walihoji ni kipi kilichomsibu kwani siyo kawaida yake.

ANTI LULU AANIKA UTAMU WAKE
Lulu Mathias Semagongo ‘Anti Lulu’ ni mtangazaji ambaye katika siku za usoni amekuwa akifanya vituko vya hapa na pale ikiwa ni pamoja na kulewa ovyo.
Naye hakuwa nyuma kwani alivalia nguo iliyoanika sehemu kubwa ‘tamu’ ya mwili wake huku akipagawa na wasanii wote waliopanda jukwaani.

MBONI, JACK PATRICK SHUGHULI YAO
Kwa upande wao mastaa Mboni Masimba na Jacqueline Patrick walikuwa wakijiachia vilivyo utadhani shuguli ilikuwa yao.
Walishangilia na kuserebuka kwa raha zao na kali kuliko walikuwa wakishangilia kila tukio.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...