Friday, October 28, 2011

MAHABA: Wanaojua kupenda ndiyo wanaolia kila siku




NI wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini Mungu amekujaalia afya njema na nguvu za kutosha kiasi cha kukufanya uendelee na mchakamchaka wa maisha kama kawaida.

Jamani, hii ni safu ya mashamsham, mahususi kwa masuala ya mapenzi kwa ujumla. Wapo wanaonitaka niingie ndani kuzungumzia mambo ya chumbani kama vile namna wanandoa/wapenzi wanavyoweza kudatishana wawapo faragha.

Ni sawa kwani hapa ndiyo mahali pake kuyazungumzia lakini niseme tu kwamba mengine tukakuwa tunaelekezana kwa njia ya simu kwani hayastahili kusomwa na kila mtu.

Wiki hii nataka kuzungumzia hili suala la machozi katika mapenzi. Mapenzi kiukweli yanawatesa wengi. Wapo ambao kila siku ni watu wa kububujikwa na machozi kutokana na yale wanayofanyiwa na wapenzi wao. Kuna wanaofikia hatua ya kujuta kwa nini wamependa, wanajuta kwa kuwa wanaona hawapati ile furaha waliyotarajia.

Hili linauma sana na niseme tu kwamba, tunapoingia kwenye uhusiano tuwe tayari kwa lolote. Kuna suala la kutendwa na kufanyiwa ndivyo sivyo na wale ambao mioyo yetu imetua kwao.

Mapenzi ni kitu cha ajabu. Leo unaweza kutokea kumpenda mtu kwa dhati kabisa na ukaamini huyo ndiye uliyepangiwa na Mungu awe wako wa maisha lakini matokeo yake unakutana na mazingira tofauti.

Unajikuta umeingia kwa mtu asiye na penzi la dhati kwako na mbaya zaidi mtu huyo hakuambii kuwa huna nafasi kwenye moyo wake. Atakukubalia kwa sababu tu aidha anataka akuonje au kuna kitu anakihitaji kutoka kwako (fedha au vitu vingine).

Hayo ndiyo mapenzi ya siku hizi, kumpata mtu anayekupenda kama unavyompenda ni bahati sana. Wengi tunapenda pasipo na penzi matokeo yake sasa ni majuto kila siku.

Kwa nini machozi?

Unajua mapenzi ni upofu, unaweza kuwa na mtu ambaye unaona dalili za wazi kabisa kwamba hakupendi lakini eti kuogopa kumkosa unasema huenda atabadilika. Bahati itakuwa kwako kama kweli atabadilika kwa kuwa wapo ambao kadiri siku zinavyokwenda ndivyo wanavyozidisha mapenzi.

Kwa bahati mbaya ukakutana na mtu ambaye haupo kabisa moyoni mwake, suala la kulia huwezi kulikwepa. Atakuwa anakutenda kila siku na kukufanyia vioja vya kila aina lakini kwa kuwa ndiyo umeshapenda, unajikuta unalia weee kisha baadaye unasahu na kuendelea naye eti ili usimkose, mh! Mapenzi bwana!

Ni sahihi kuvumilia?

Sisemi usimvumilie yule uliyetokea kumpenda lakini ninachoeleza ni kwamba, uvumilivu una kikomo. Kwa mfano umetokea kumpenda mtu lakini kila unavyojaribu kumuweka kwenye mizani unabaini umeingia sehemu isiyo sahihi, piga moyo konde kisha muache.

Usimpe nafasi mtu akayafanya maisha yako yakawa ni ya huzuni kila siku. Tambua una haki ya kupenda lakini huna haki ya kulizwa na mtu unayempenda. Kama anakuliza si ndiyo ujue kwamba hana mapenzi ya dhati na wewe? Sasa kwa nini umng’ang’anie?

Ni safari ya kumpata mtu sahihi

Wataalam wa mapenzi wanaeleza kuwa, wengi ambao wanaishi maisha ya kimapenzi yaliyotawaliwa na furaha walipitia hatua ya kulizwa.

Ni wachache ambao walibahatika kuwapata watu sahihi moja kwa moja. Hivyo basi kama huyo uliyenaye hakupi ile furaha uliyotarajia, elewa ni hatua ya kuelekea kwa mwingine ambaye huenda ndiye alipangiwa kuwa wako.

Muwahi kabla

Huyo anayekuliza itafika wakati atakuacha na naamini kwa kuwa utakuwa umempenda sana utaumia kupita maelezo. Kwa msingi huo, endapo utaona dalili za wazi kwamba hupendwi, unatakiwa kumuacha haraka kabla hajakuacha. Hiyo itakusaidia kisaikolojia kwani utakuwa umejiandaa kumkosa tofauti na ile unaamka asubuhi unakutana na sms akikuambia wewe na yeye basi, utaumia sana.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...