Wednesday, January 4, 2012

MWINGIRA ANUSURIKA KUUAWA...



KATIKA tukio lisilo la kawaida kufanyiwa kwa viongozi wa makanisa ya kiroho, wananchi wa eneo la Mapinga wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani nusura wamuue Nabii Josephati Mwingira kutokana na kugombea shamba lililopo kijijini hapo. 
Tukio hilo lilitokea Jumatano iliyopita baada ya Nabii Mwingira kwenda katika shamba hilo akiwa na walinzi lukuki wa Kimasai na wa kampuni binafsi ya ulinzi ambayo iliwapa askari wake bunduki ya kumlinda.

BUNDUKI NJENJE
Mwanahabari wetu maalumu aliyekuwa na wenzake, alishuhudia ghasia zikiibuka mara baada ya Nabii Mwingira kufika katika shamba hilo na wananchi kudai alikwenda kwa lengo la kubomoa nyumba zao hali iliyozusha zogo na nabii huyo akalazimika kujificha kichakani huku askari wanaomlinda bunduki zao zikiwa nje nje tayari kwa lolote.

Waandishi wa habari na wananchi waliojaribu kumsogelea Mwingira ilibidi wasimame baada ya askari kuwajia juu na mmoja kusema: “Nimeshakoki, atakayemsogelea nabii shauri yake.”
Aidha, askari huyo  aliendelea kukoki bunduki yake licha ya wana habari kumuomba awaruhusu wazungumze na Mwingira ili naye aweze kutoa ufafanuzi juu ya tukio hilo.

Ombi la wanahabari hao liligonga mwamba kutokana na ubabe uliooneshwa na askari hao ambao walikuwa na bunduki aina ya shortgun, huku Wamasai waliokuwa na sime wakizuia kiongozi huyo kuhojiwa.
Mwanakijiji mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Saidi alisema Mwingira na askari wake walikwenda kijiji kwao kwa nia ya kuwafukuza wao (wanakijiji) katika mashamba yao kwa madai kuwa wamevamia eneo lake.
Alidai kuwa mara baada ya Nabii Mwingira na kundi lake kufika katika ardhi hiyo aliyodai wanaimiliki kwa muda mrefu, baadhi ya nyumba zilivunjwa, hali iliyofanya wanakijiji kupandwa na hasira na kutaka kumdhuru mtume huyo.

WAOMBA AKAMATWE
Hata hivyo, mjumbe mmoja wa serikali ya kijiji aliyezungumza kwa sharti la kutoandikwa jina lake kwa kuwa siyo msemaji,  alisema wanakijiji walichukizwa na Mwingira kuja katika ardhi yao na askari kwa sababu wamefungua kesi Mahakama Kuu na ameitwa mara tatu bila kutokea.
“Hivi sasa tunataka akamatwe kwani amekuja kutuvunjia wakati kesi ipo mahakamani, ameingilia uhuru wa mahakama, tutaiomba korti itoe hati ya kukamatwa ili afikishwe mbele ya sheria,” alidai mjumbe huyo huku akishangiliwa na wanakijiji.

KAMATI YA ULINZI YA MKOA
Habari za uhakika zinasema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani iliketi Ijumaa iliyopita kujadili mgogoro huo unaotishia amani katika eneo hilo, hata hivyo kilichojadiliwa kimekuwa siri.
Wakati huo huo, kuna habari zinadai kuwa yupo mwanamke mmoja anayeitwa Rose Liyimu naye anadai eneo hilo ni lake, madai ambayo mjumbe wa serikali ya kijiji amekanusha na kusema mmiliki halali kati yao atajulikana mahakamani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...