Wednesday, January 4, 2012

KANUMBA; MAPENZI NA MASTAA MATATIZO




HANDSOME boy anayefurukuta katika tasnia ya filamu za Kibongo, Steven Kanumba amesema, kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mastaa ni matatizo matupu...
Kanumba anayewakilisha kampuni kadhaa kama balozi huku akivuna fedha za kutosha katika filamu, alisema katika kipindi alichokuwa na uhusiano na mastaa mambo yake mengi yalikwama.
Staa huyo alibainisha hayo katika mahojiano maalumu, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Sinza-Mori, Dar ambapo pamoja na mambo mengine alieleza kuhusu mafanikio aliyopata mwaka huu.
“Mapenzi na mastaa ni pasua kichwa kaka...ni matatizo matupu. Nasema hivi kwa sababu nilishapitia. Unajua mastaa wana mambo mengi, kwanza wao wenyewe, halafu watu wanaowazunguka.
“Ni kama wanaendeshwa na vyombo vya habari, ndiyo maana kila siku skendo kwenye magazeti haziishi. Usipokuwa makini unaweza kujikuta unatumia muda mwingi kujadili skendo za magazetini badala ya kuangalia mipango mingine,” alisema Kanumba.
ANAISHI KISTAA
Alisema kwa sababu ameshatambua thamani ya ustaa wake, analazimika kuishi katika hadhi hiyo ili aweze kuilinda heshima yake.
“Kuwa staa si kazi kubwa sana kama kuulinda ustaa, ndiyo maana siku hizi nipo makini zaidi. Mitoko yangu yote ina sababu maalum na ipo kwenye ratiba.
“Natumia muda mwingi kufanya kazi zangu na kumtumikia Mungu. Sina muda wa kupoteza...nisipokuwa kwenye vikao kanisani, nitakuwa ofisini, kama sivyo basi nitakuwa location (eneo la kurekodi) au nipo na editor (mhariri) wangu tunaendelea na editing (uhariri) ya sinema zijazo,” alisema Kanumba na kuongeza:
“Kwa mambo hayo, huwezi kuyatimiza kama utakuwa kwenye uhusiano na staa. Mh! Wana mambo mengi hao?! Wakati mwingine utalazimika kuwa naye kila anapokwenda, sasa ya kazi gani yote hayo? Presha tupu.”
MIKATABA
Kanumba alisema, kwa sasa ana mikataba ya matangazo ya biashara na makampuni mengi na bado kuna mengine yapo mbioni kusaini naye.
“Nafanya kazi na kampuni nyingi kama balozi wao, hawajanikubali hivi hivi, ni baada ya kunichunguza na kuona nina maadili mazuri, isingekuwa rahisi kuniteua kama ningekuwa kwenye mapenzi na staa.
“Mialiko mingi sana inakuja, tena wakati mwingåine ya hadhi ya juu, ambapo nakaa eneo moja na viongozi wakubwa wa nchi. Inatia faraja, lakini lazima nilinde hii heshima,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...