Friday, January 27, 2012

AISHA MADINDA YUKO HOI ...




MNENGUAJI wa Bendi ya Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo,’ Aisha Mohammed Mbegu ‘Aisha Madinda’ (pichani) yuko hoi tena akisumbuliwa na tatizo lilelile la kuvimba miguu.


Akizungumza nyumbani kwake Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam huku afya yake ikionekana kudhoofika sana, Aisha alisema ni takribani mwezi wa pili sasa hajapanda jukwaani kutokana na hali aliyonayo.


Alisema kinachomchanganya zaidi ni kwamba amekwenda hospitali mbalimbali lakini tatizo halijaonekana zaidi ya kupewa dawa za kupunguza maumivu na kutakiwa kurudi nyumbani.
“Hali yangu kwa kweli siyo nzuri kabisa, miguu imevimba tena kiasi cha kinikosesha amani. Nimekwenda hospitalini wameniambia hawajaona tatizo ila wakanipa dawa flani ambazo nimetumia na sasa kidogo huu mguu moja umepungua ila huu mwingine bado,” alisema Aisha.


Akaongeza kuwa, kwa hali aliyonayo anaamini ni mambo ya dunia hivyo akawaomba mashabiki wake wamuombee dua ili apone na arudi jukwaani kuwapagawisha.
 “Kikubwa mashabiki wangu waniombee, nina imani nitapona na kuondokana na mateso haya,” alisema Aisha ambaye mara kwa mara amekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...