Tuesday, May 8, 2012

SKENDO YA UNGA: KANUMBA ACHAFULIWA...



Obi Okedia.

Madawa ya Kulevya.


                                      Steven Kanumba.

ALIYEKUWA nyota wa filamu Bongo, marehemu Steven Kanumba, anaendelea kutajwa, safari hii jina lake limewekwa kwenye rekodi za kipolisi katika Kitengo cha Kudhibiti Madawa ya Kulevya.

Kanumba, amechafuliwa na raia wa Nigeria, Obi Okedia,  ambaye alinaswa na madawa ya kulevya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa, Obi baada ya kukamatwa, alijitambulisha kwamba ni msanii wa filamu wa Nigeria na alikuja nchini kurekodi ‘muvi’ na marehemu Kanumba.

Kabla ya Nzowa, mmoja wa askari wa kitengo hicho alimueleza mwandishi wetu kuwa Obi baada ya kukamatwa, aliomba asikaguliwe kwa sababu yeye ni swahiba mkubwa wa Kanumba na alikuja nchini kwa ajili yake.

“Tukamuuliza, kwa hiyo ulikuwa unashirikiana na Kanumba kuuza madawa ya kulevya, akasema wao ni wasanii wa filamu na huwa wanashikirikiana kikazi,” alisema askari huo (jina tunalo) na kuongeza:
“Tulipomkagua, tukakuta amemeza pipi za madawa ya kulevya. Hii ikatufanya tuone anamchafua Kanumba. Alitaka kutumia jina lake kutufanya tusimkague, na sina uhakika kweli kama yeye ni msanii wa filamu.”

Kwa upande wa Nzowa, alisema kuwa Obi alikamatwa usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Nzowa alisema, Obi alifika nchini tangu Aprili mwaka huu na alikuwa akiishi kwenye Hoteli ya Rainbow, Dar es Salaam.

“Hivi sasa (juzi asubuhi), tumempeleka Muhimbili (Hospitali ya Taifa) kwa uchunguzi zaidi. Tutamfikisha mahakamani uchunguzi ukikamilika.

“Huko mahakamani ndiyo itajulikana kama kweli alikuwa anashirikiana na Kanumba kikazi au alimtaja kwa lengo la kumchafua ili asifanyiwe upekuzi wa kipolisi,” alisema Nzowa.

Kanumba, alifariki dunia Aprili 7, 2012 na katika maelezo ya Nzowa kuwa Obi aliwasili nchini tangu Aprili, haijawekwa wazi kama ni kabla ya kifo cha staa huyo au baada.

Kwa upande mwingine, binamu wa Kanumba (jina tunalihifadhi), amesema kuwa familia yao ina kazi kubwa kuweka sawa mpasuko kati ya mama mzazi wa msanii huyo, Flora Mtegoa na mzazi mwenzake, Charles Kusekwa Kanumba.

Alisema, mgogoro wa kugombea mali za Kanumba ni mkubwa na endapo suluhu ya haraka haitapatikana, wazazi hao wa staa huyo wa filamu, wanaweza kutoana roho.

“Kila mmoja sasa anaamua lake na kupanga anavyojua kuhusu mali za Kanumba. Mama hataki Mzee Charles ahusike kwa namna yoyote. Mzee Charles yeye anasema atafunga mtu atakayecheza na mali za mwanaye. Sasa huoni kama hiyo ni vita?

“Kama familia kuna mambo mazito sana sasa hivi yanazungumzwa. Mengine ni makali sana na siyo ya kuzungumza ila napenda watu wajue kwamba ni vita. Ingependeza kama familia ingeketi kulimaliza hili,” alisema binamu huyo wa Kanumba ambaye alisisitiza hifadhi ya jina lake kwa sababu za kiusalama.

Habari zinasema kuwa mgogoro mzito umeibuka baada ya Flora kudaiwa kuanza kupiga mnada mali za Kanumba, jambo ambalo limemuudhi Mzee Charles.

Hata hivyo, Flora alishanukuliwa na vyombo vya habari kwamba Mzee Charles hahusiki kwa namna yoyote kwa sababu hakukutana na Kanumba tangu mwaka 1999.

Kauli hiyo, ilikosolewa baada ya picha za Kanumba na baba yake, zilizopigwa mwaka jana, wakati msanii huyo alipomtembelea Mzee Charles nyumbani kwake mkoani Shinyanga.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...