Saturday, May 19, 2012

A-Z kifo cha mafisango

WADAU wa soka ndani na nje ya Bongo wamepigwa na butwaa kufuatia kifo cha ghafla cha kiungo mshambuliaji wa Simba Sports Club, Patrick Mafisango Mutesa (32) kilichotokea kwa ajali ya gari Barabara ya Chang’ombe, eneo la Chuo cha Ufundi cha Veta, Dar es Salaam.



Mchezaji huyo alifariki dunia saa 9 usiku wa kuamkia Alhamisi, akitokea Klabu ya New Maisha iliyopo Masaki, Dar akiwa na mdogo wake, Lolilembe, mwanamke mmoja na dereva wake aliyefahamika kwa jina moja la Boaz.

Habari zilisema, Mafisango alifika kwenye klabu hiyo akiwa na Boaz na mdogo wake lakini walipata kampani ya wanawake wawili.
Akizungumza na waandishi wetu, mwanamuziki wa Bendi ya Akudo Impact, Boteku Clary ambaye alikuwa akipewa ofa ya kinywaji na marehemu, alisema walifurahia  muziki uliokuwa ukiporomoshwa na Bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’, mwishowe wanawake hao walimtaka marehemu waondoke.
Ikadaiwa kuwa mjadala wa kuondoka ulichukua muda kwani marehemu alitaka kuendelea kuwepo kwenye klabu hiyo kwa kuwa ‘mfuko’ ulikuwa bado ukimruhusu kuendelea kutanua.
Baada ya wanawake hao kumbembeleza sana, marehemu aligawa fedha kwa wanamuziki wa Akudo ambapo rapa wa bendi hiyo, Kanal Top alipewa shilingi 5,000 akimtaka waendelee kupata vinywaji.
Baada ya hapo, marehemu, mdogo wake, dereva wake na wanawake hao waliingia kwenye gari aina ya Toyota Cresta lenye namba za usajili T 387 BMZ  kwa ajili ya kurudi makwao.
Katika safari hiyo, inadaiwa mwanamke mmoja alipelekwa kwake na kwenye gari wakabaki Mafisango, mdogo wake, dereva na mwanamke mmoja.
Njiani, habari zinadai, marehemu alimuomba dereva amuachie gari aendeshe ambapo alimudu mpaka alipofika Barabara ya Chang’ombe, baada ya kumaliza ukuta wa Chuo cha Ufundi Veta ndipo walipokutana na mwendesha pikipiki akiwa ameingia upande wao. Marehemu alijaribu kumkwepa lakini gari likamshinda na kuingia mtaroni.
Mmoja wa walinzi wa eneo hilo aliyeshuhudia ajali hiyo, alisema walifika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada ambapo waliwatoa majeruhi lakini Mafisango alikuwa tayari ameshapoteza maisha huku  akivuja damu nyingi juu ya jicho la kushoto na sehemu mbalimbali kichwani.
Kwa mujibu wa mlinzi huyo, walifanya utaratibu wa kuwakimbiza majeruhi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mwili wa Mafisango ukapelekwa kuhifadhiwa kwenye chumba cha maiti.
Akizungumza, ‘Prezidaa’ wa Bendi ya Akudo Impact, Christian Bella alisema marehemu alikuwa amewaandalia ‘pati’ nyumbani kwake Keko Bora, Dar  jioni ya siku ya ajali.
Marehemu alisafirishwa kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa mazishi.
Ingawa alikuwa na uraia wa Rwanda na aliichezea timu ya taifa ya nchi hiyo (Amavubi), Mafisango alikuwa ni mzaliwa na raia wa DRC na uamuzi wa kuzikwa huko ni wa familia yake.




Askari akiwapangua waombolezaji kupisha njia kwa ajili ya magari kupita.

Magari yaliyoongoza msafara huo kuelekea uwanja wa ndege.

Gari lililobeba mwili wa marehemu Mafisango, likiwa limezingirwa na mashabiki.

Mashabiki wakikimbiza magari.
Baada ya mashabiki kuuaga mwili wa aliyekuwa mchezaji wa timu ya soka ya Simba, Patrick Mafisango, katika uwanja wa TCC Chang’ombe uliopo Temeke jijini Dar es Salaam, ulianza msafara kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl.  Julius Nyereree,  ambapo utalala na kesho asubuhi kusafirishwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya maziko.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...