Wema Sepetu.
Jokate Mwegelo.
Naseeb Abdul ‘Diamond’.
MASTAA wa kike wanaotambiana Bongo, Wema Sepetu na Jokate Mwegelo, ilibaki kidogo wazichape kavukavu kisa kikiwa kilekile, msanii anayetingisha katika Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond’.
Chanzo chetu makini kimenyetisha kwamba mtiti huo ulitokea Ijumaa Mei 25, mwaka huu katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo, Dar ambapo kulikuwa na Shindano la Miss IFM, 2012.
CHANZO KINADADAVUA
Katika ‘event’ hiyo, Wema alikuwa mmoja wa majaji waliochagua washindi wakati Jokate alifika kama mdau wa urembo huku uwepo wa Diamond ukiwa kwa ajili ya kupiga shoo.
“Wema alikuwa mmoja wa majaji, Jokate alikwenda kama shabiki tu, lakini mambo yalianza kuharibika baada ya mshindi kutangazwa ambapo Jokate hakuridhishwa na matokeo.
“Hata hivyo, watu walisema ni chuki zilizosababishwa na wivu wa kimapenzi kwa Diamond,” chanzo kilieleza.
JOKATE ALIANZA HIVI
Habari zinasema kwamba, Jokate aliamua kupita mbele ya meza ya majaji na kumuuliza Wema kama yeye aliridhika na matokeo yale.
“Ilikuwa balaa, Jokate alikwenda kwenye meza ya akina Wema (majaji), akaanza kumuuliza, yaani huyu ndiyo mshindi mliyetuchagulia? Miss gani anakuwa hivyo?” kilisema chanzo na kuongeza:
“Kifupi alikuwa akitoa kejeli kwa majaji hasa Wema kwa vile aliwahi kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia.”
WEMA AKAMALIZA
Baada ya chokochoko za Jokate ambaye inasemekana alikuwa ‘amechangamka’ kidogo, Wema alijibu mashambulizi kwa staili ya aina yake, alikaa kimya akiendelea na shughuli nyingine.
“Ukimya wa Wema ukasababisha Jokate azomewe kwa sauti kubwa na mashabiki huku wakimsonya. Kiukweli bila ushabiki, Wema alionesha ukomavu siku ile.
“Kama naye angepandisha hasira, ilibaki kidogo sana wakung’utane, maana Jokate alionekana dhahiri kutaka ugomvi lakini mashabiki wakaununua kwa kumzomea. Aliabika sana,” kiliendelea kupasha chanzo hicho.
DIAMOND AAMSHA SOO UPYA
Wakati Diamond akiwa jukwaani ‘akipafomu’ wimbo wa Nimpende Nani? ikawa kama ameamsha ‘muziki’ upya kabisa kwa upande wa Jokate.
“Diamond alipouliza nimpende nani? Watu wakawa wanapiga kelele wakisema, Wemaaaa, lilipotamkwa jina la Jokate, ilifuatiwa na zomeazomea, hali hiyo ilizidi kumpa Jokate wakati mgumu.”
Habari zinadai, hali ilizidi kutibuka zaidi baada ya mashabiki kumzonga Wema wakimtaka kupiga naye picha huku wakimtupia vijembe vya wazi Jokate.
JOKATE APOTEA GHAFLA
Kutokana na hali hiyo, Jokate alishindwa kuvumilia kashikashi za mashabiki waliokuwa upande wa Wema, hivyo akatoweka ukumbini humo.
Chanzo kikaendelea kufafanua kuwa kuna wakati alitafutwa kwa ajili ya kupiga picha ya pamoja na washindi waliotinga Tatu Bora wakiongozwa na Miss IFM 2012, Fina Revocatus aliyeshinda lakini bila mafanikio.
WEMA ANASEMAJE?
Baada ya madai hayo, mapaparazi wetu walianza kazi ya kumsaka Wema ili aeleze anachokijua kuhusu habari hiyo ambapo walifanikiwa kumpata siku ya pili ya tukio, Mei 26 mwaka huu na kutoa ushirikiano wa kutosha.
Akizungumza kwa njia ya simu na paparazi wetu, Wema alikiri kutokea kwa tafrani hiyo akisema ameiona nguvu ya jamii katika kusimamia ukweli.
Huyu hapa mwenyewe anafunguka: “Malipo ni hapa hapa duniani. Namshukuru Mungu, aibu haikuja upande wangu, nimeamini mashabiki wengi walisimama na mimi na ukweli ulijulikana.
“Siku zote penye ukweli, uongo hujitenga. Kila mtu ameamini kuwa kuachana kwangu na Diamond sikuwa na makosa. Sikunyanyua mdomo wangu kusema chochote, mashabiki ndiyo wamekuwa mabalozi wangu. Niseme nini tena?”
JOKATE NAYE?
Jitihada za kumpata Jokate ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa hewani kila alipopigiwa.
Hata hivyo, ‘polisi’ bado wapo mzigoni wakiendelea kumsaka atakapopatikana mbivu na mbichi zitawekwa peupe.
KUMBUKUMBU MUHIMU
Wema na Jokate walichuana vikali katika Shindano la Miss Tanzania mwaka 2006 ambapo Wema alitwaa taji na Jokate kuchukua nafasi ya pili.
Wote wawili, nje ya fani ya urembo, wamejaribu kwenye ulingo wa filamu. Hakuna ubishi kuwa Wema ndiye aliyefanikiwa zaidi kuliteka soko la sinema za Bongo huku Jokate akipiga hatua moja zaidi kwenye mitindo.
TUMEFIKAJE HAPA?
Awali, Wema aliwahi kuwa mpenzi wa Diamond na kumwagana kabla ya kurudiana na kuendelea na penzi lao.
Baadaye wawili hao wakamwagana tena huku Wema akitoa madai mazito kuwa shogaye Jokate alikuwa akitoka na shemeji yake, Jokate alikanusha kwa nguvu zote.
Kukiwa bado kuna wingu la sintofahamu, penzi la Jokate na Diamond likawa peupe kabla ya wiki chache zilizopita kudaiwa kwamba limevunjika.