Thursday, November 1, 2012

MAHABA: IJUE JANJA YA WANAUME WANAOJIFANYA WANAJUA KUHUDUMIA SANA!


HUKO mtaani kuna wanaume ambao ni wasanii sana. Kwa usanii wao huo, wameweza kutembea na wasichana wengi kwa kuwatangazia ndoa lakini mwishoni ndoa inayeyuka baada ya wanaume hao kuonja penzi.

Ukijaribu kufuatilia utabaini wahanga wa tabia hii ni wengi sana hasa wale ambao ni wazuri na wamekuwa na misimamo ya kuhakikisha hawachezewi ovyo na wanaume.


Hivi karibuni nilizungumza na msichana mmoja ambaye hakika mapenzi yanamtesa. Kwa maelezo yake anasema, yeye ni mtu ambaye akipenda amependa na mara nyingi akimpenda mtu anajitahidi kumtimizia kila kitu ili asije akamkosa.


Bahati mbaya kwake ni kwamba, amekuwa ni mtu wa kutendwa sana. Wanaume wamekuwa wakimtokea sana kutokana na uzuri alionao lakini mwisho huachwa solemba. 


Nilibahatika kukutana naye uso kwa uso, hakika ni msichana ambaye kila mwanaume atatamani amuite mkewe na sifa za muonekano wake huo ndizo zinazomfanya leo hii mapenzi ayaone ni shubiri. 


Mwaka mmoja uliopita aliolewa na mwanaume mmoja mwenye fedha zake lakini ndoa yake haikudumu, akapewa talaka kwa sababu ambazo haziingii akilini kabisa.


Alipoachika, mwezi mmoja baadaye akapata mwanaume mwingine ambaye alionesha kumpenda sana. Dada wa watu akaingia mkenge akijua amependwa na mwanaume sahihi kumbe ametamaniwa.
Mwanaume huyo akawa anahudumia ile mbaya huku akiahidi ndoa lakini kumbe alikuwa na lake kichwani. Siku ya siku yule mwanaume akaomba apewe penzi, yule msichana akaona si vyema kumnyima raha mchumba wake.


Masikini kumbe mwanaume yule naye alikuwa akihudumia huku dhamira yake ikiwa ni kumuonja binti huyo mrembo. Mpaka sasa binti huyo yupo singo, mapenzi anayaona ni kituo cha polisi licha ya kwamba anatamani kuitwa mke wa mtu.


Dada huyu anatufundisha nini? Ni kwamba, huko mtaani kuna wanaume ambao wako tayari kuoa ili mradi tu wawaonje wasichana wanaoonekana ni wazuri lakini wagumu kutoa penzi kabla ya kuingia kwenye ndoa.


Msichana anaweza kujitunza sana akiwa na dhamira ya kumpata mwanaume ambaye atamuoa na si kumchezea lakini mwishowe akajikuta anampata mwanaume ambaye anamuoa ili tu amuonje.
Wapo wanaume wa sampuli hiyo, wana fedha zao na wanahakikisha kwa gharama yoyote wanawapata wasichana wazuri wanaojifanya wana misimamo. 


Mwanaume anaweza kukutokea kwa upole kabisa na kukuambia amekupenda na anataka kukuoa. Utamchunguza na utabaini ni mwanaume mwenye vigezo vyote vya kuwa mumeo. Unamkubalia na kumtaka aende kujitambulisha kwa wazazi wako.


Mwanaume huyo anafanya hivyo, haraka haraka anatangaza ndoa. Unashangaa mambo yanakwenda fasta, unaingia ndani na baada ya mwanaume huyo kukufaidi kwa siku kadhaa, anakutafutia visa kisha anakuacha.


 Jamani watu wa aina hiyo wapo hivyo kuwa makini na hawa wanaume wanaojifanya wanajua kuhudumia sana lakini pia kaa ukijua kwamba si kila anayekuja kwa lengo la kukuoa ni mtu mwema, wengine ni waongo wanaotumia mbinu hiyo ili wakuonje tu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...