ZIKIWA zimebaki siku 141 tu kufikia Desemba 21, 2012 ambapo ilitabiriwa kuwa ndiyo mwisho wa dunia, wasiwasi umeongezeka miongoni mwa jamii huku baadhi ya wanasayansi wa Magharibi wakisisitiza kuwa siku hiyo haitapita.
Baadhi ya imani kama ya Kikristo wao wanasikitika kuwa kama ni kweli, basi tukio hilo litatokea siku 4 kabla ya sikukuu ya kuzaliwa mkombozi wao, Yesu Kristo ‘Krismasi’, Desemba 25.
Wengi waliozungumza na gazeti hili walionesha dhahiri hofu yao juu ya mwisho wa dunia wakisema haiingii akilini wala hawapati picha itakavyokuwa.
MWISHO WA KISAYANSI NA KIIMANI
Hofu imezidi kutanda kuelekea Desemba 21, 2012 kwa sababu kuna miisho miwili ya dunia. Wanasayansi wanazungumza vyao, lakini imani nayo haijabaki nyuma kuhusu hilo.
Hakuna shaka kuwa kuwepo kwa utabiri wa kiimani na ule wa kisayansi kuhusu tukio moja ni dalili ya kuwepo kwa ukweli juu ya tukio lenyewe, licha ya kwamba kuna upinzani kutoka pande mbalimbali kuhusu ukweli wa tukio husika.
MWISHO WA KISAYANSI
Kwa mujibu wa kalenda ya Maya, Desemba 21, 2012 dunia itafikia kikomo chake cha mzunguko wa mamilioni ya miaka kisa kikiwa ni sayari ijulikanayo kwa jina la Nibiru kuigonga dunia na kutokea mlipuko ambao hautabakiza kitu duniani.
Wanasayansi wa utabiri huo walisema sayari hiyo imeshaanza safari ya kuikaribia dunia na siku hiyo ndiyo itahitimisha mwelekeo wake.
Hata hivyo, taasisi kubwa ya mambo ya anga nchini Marekani, Nasa imekuwa ikikanusha madai hayo kwamba si ya kweli na kuongeza kuwa ni mbinu ya baadhi ya wanasayansi kuitia hofu dunia.
MWISHO WA KIIMANI
Viongozi mbalimbali wa imani za Kikristo na Kiislam duniani kote hawawezi kumaliza mahubiri yao bila kuwaambia waumini wao kuwa wapo katika nyakati za mwisho wa dunia huku wakinogesha na maandiko kuwa dalili zote zilizoandikwa katika vitabu vitakatifu zimeanza kufanya kazi.
Dalili ambazo viongozi wa kiimani wamekuwa wakizitolea mifano ni watu kupenda fedha kuliko kumpenda Mungu, binadamu kuuana kinyama wenyewe kwa wenyewe, vita ndani ya nchi moja, makabila kwa makabila na falme kwa falme.
Yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika nchi za Tunisia, Misri, Libya, Yemen, Irak, Syria, Sudan (zote) na Ethiopia ni kielelezo tosha.
Hata hivyo, katika mwisho wa kiimani, licha ya viongozi wake kukiri umekaribia, hawakubaliani na kujulikana kwa siku wakisema hakuna ajuaye.
Akizungumzia hilo, Mchungaji Florian Katunzi wa Kanisa la Kiroho la EAGT, Sabasaba, jijini Dar es Salaam alisema wanaoamini kuwa Desemba 21, 2011 ni mwisho wa dunia, wamepotoka.
“Ni uzushi mkubwa, Yesu na malaika wote hakuna anayejua mwisho wa dunia, sasa hao wanaosema ni Desemba 21 wametokea wapi?” alihoji mchungaji huyo.
KWA NINI 21?
Kwa mujibu wa tabiri mbalimbali, tarehe 21, ndiyo zinatajwa sana kuhusika na mwisho wa ulimwengu.
Itakumbukwa kuwa Mei 21, mwaka huu, ilitabiriwa kuwa ingekuwa mwisho wa dunia lakini ikapita. Tarehe nyingine ambazo ziliwahi kudaiwa kutokea kwa mwisho wa dunia ni Novemba 21, mwaka jana, Januari 21, mwaka 1980 na Juni 21, 1987.
WAUMINI HAWAPENDI?
Mchungaji John wa Madhehebu ya Kisabato aliwahi kuzungumza kupitia Radio Morning Star ya jijini Dar es Salaam, Februari 27, mwaka huu saa nne usiku ambapo alisema waumini wengi wa kizazi cha sasa hawataki kusikiliza mahubiri yanayohusu habari za mwisho wa dunia kwa vile hayana faraja kwao.
FREEMASON NA MAANDIKO
Nayo imani ya Ki-freemason haiko nyuma kutajwa katika imani kwamba kwa kipindi hiki cha mwisho wa dunia inavuna waumini wengi kwa vile siku za kufikia mwisho wa dunia zimebaki chache.
Wengi wanaamini kuwa imani hiyo inafanikiwa kuvuna kwa wingi kwa sababu maandiko yanasema ‘njia iendayo upotevuni ni pana na wanaopita huko ni wengi’.
YESU FEKI NAYE APATA WAUMINI
Wakati hali kwa Freemason ikiwa hivyo, yule binadamu anayejiita Yesu lakini ‘feki’ naye anaendelea kuzoa wafuasi wake ambao wanaamini yeye ndiye Kristo aliyeandikwa katika vitabu vya Mungu.
Sergei Torop (48) amekuwa akipita mitaani nchini Russia akihubiri Injili na kuwaombea watu wenye matatizo mbalimbali. Jamaa huyu ana mke na watoto sita.
MEZANI KWA MHARIRI
Hakuna ubishi kwamba imani huja kwa kusikia neno la Mungu, kila binadamu anaamini kwa staili yake kuhusu uwepo wa mwisho wa dunia, lakini ukweli unabaki palepale, kesheni mkisali kwa maana siku wala saa haijulikani. Mwisho wa dunia utakuja kama mwizi.
No comments:
Post a Comment