Tuesday, August 28, 2012

BABU LOLIONDO NI TAPELI




SERIKALI imethibitisha kuwa kitendo alichokuwa akifanya babu wa Loliondo, Mchungaji Ambilikile Masapile, cha kutoa dawa ya kutibu magonjwa, ukiwemo Ukimwi aliyokuwa amedai kuwa ameoteshwa na Mungu ni cha kitapeli.

 Utafiti umebaini kwamba dawa hiyo  ya babu wa Loliondo ni feki na kwamba haina uwezo wa kutibu Ukimwi wala kisukari.

Kwa mujibu wa  Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, utafiti wa kulinganisha wagonjwa wa Ukimwi na kisukari waliokunywa dawa hiyo na wale ambao hawakunywa, umebaini kwamba hakuna utofauti wa afya ya mgonjwa.
Alisema utafiti huo unafanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), ulianza Machi mwaka huu na kwamba unahusisha wagonjwa 200 wanaofuatiliwa kwa kupimwa damu, kinga ya mwili (CD4) na uzito wa mgonjwa, ambao ulifanyika tangu mgonjwa alipokunywa kikombe cha babu.
“Matokeo ya awali ya utafiti yameonyesha kuwa hakuna utofauti katika vipimo vya kimaabara pamoja na damu, CD4, uzito na ubora wa afya ya wagonjwa kati ya waliokunywa na wale ambao hawakunywa dawa ya mchungaji,” alisema Dk. Mwinyi.
Alisema lengo la utafiti huo ni kubaini uwezo wa dawa hiyo katika kutibu magonjwa aliyosema dawa yake inayatibu ili kuona kama kuna utofauti wowote baada ya mgonjwa kutumia dawa.
Kufuatia hali hiyo, jeshi la polisi nchini limesema kwamba linafuatilia kwa makini sakata la Mchungaji Masapile anayeishi katika kijiji cha Samunge mkoani Arusha kufuatia malalamiko ya wananchi kuwa licha ya dawa yake kuonekana haitibu, bado watu wanakwenda na kunywa.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni ofisini kwake makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,  Advera Senso, amesema kwamba kutokana na malalamiko hayo polisi watawasiliana na wizara ya afya ili kuchukua hatua stahiki.
Msemaji huyo amesema kwamba wanataka kujua kama wizara ya afya imepiga marufuku dawa hiyo au inasema nini baada ya kubainika kuwa haitibu na amewataka wananchi kutoenda huko.
 Wananchi wengi waliozungumza na gazeti hili wamedai kwamba Babu amewatapeli wananchi na kinachowauma ni kuona kuwa kuna watu wanaendelea kwenda kunywa kikombe japokuwa hawatangazwi.
“Wananchi wengi waliuza mali zao na kukimbilia kwa babu kupata tiba, kumbe ulikuwa ni utapeli, ukweli ni kwamba serikali imechelewa mno kutoa tangazo hili,” alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja tu la John.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyama  vya Watu  Wanaoishi  na Virusi vya Ukimwi  nchini (TAMOPHA), Julius Kaaya,  ameitupia  serikali   lawama  kwa  kuipigia  debe dawa  ya Babu  na  kuwafanya  wagonjwa  kutoroka hospitali huku wengi  wao wakiacha  kuendelea na  dawa wakiamini  wangepona  baada ya kunywa kikombe kimoja .
“Huyu Babu inatakiwa ashitakiwe apelekwe  mahakamani afilisiwe mali zake zote alizochuma  toka kwa wagonjwa na ikiwezekana afungwe ili iwe fundisho kwa watu wengine,” alisema Kaaya na kuongeza kuwa wao wanajiandaa  kumfungulia  kesi.
Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste (TAG) Mkoani Arusha, Steve Wambura, amemtaka babu huyo amrudie Mungu kwa kutubu kuwa aliwatapeli wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Waganga wa Tiba Asili Mkoa wa Dar es Saalam, Maneno Tamba,  amesema babu huyo siyo  mwanachama wao na walishangazwa na serikali kumpigia debe, hali iliyosababisha vifo vya watu wengi waliomkimbilia na kuacha tiba sahihi.
Baadhi ya mawakili, akiwemo Mabere Marando   wamesema kwamba wapo tayari kumfikisha  mahakamani babu huyo wakijitokeza waliotapeliwa na watamfungulia kesi ya kujipatia  fedha kwa njia ya udanganyifu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...