Thursday, August 2, 2012

Alama za Kishetani Kila Mahali


Alama kuu ya 'kanisa' la kilimwengu la kishetani
Maandiko yanasema kwamba: Nao wanaoufuatia uhai wangu hutega mitego; nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya; na kufikiri hila mchana kutwa. (Zab. 38:12).
Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; wametandika wavu kando ya njia; wameniwekea matanzi. (Zab. 140:5).
Pia imeandikwa: Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo. (Isaya 5:14).
Shetani halali. Usiku na mchana, karne hadi karne yuko katika hekaheka za kuwakusanya wanadamu ili kwenda nao kwenye jehanamu ya moto.
Zipo njia maelfu za kutekeleza malengo yake hayo. Lakini msingi wa hayo yote, ni kumtumia mwanadamu mwenyewe. Wako wanadamu wengi leo ambao ni waabudu shetani na wanajua kabisa; na wameamua toka mioyoni mwao kwamba wao watakuwa ni raia wa kuzimu.
Wako wengine, walio kundi kubwa zaidi, ambao wameingizwa kwenye uraia wa kuzimu bila wao kujua. Lakini ukiwauliza kama wao ni raia wa kuzimu watakataa katakata. Hata hivyo, ukweli ni kwamba ni washirika wa huko kwa asilimia mia moja.
Sitaongelea kila njia anayotumia shetani kuwanasa wanadamu, lakini nitapenda tuangalie njia ambayo si wengi wanaweza hata kuidhania.
Biblia inamtaja ibilisi kama kerubi afunikaye (Ezekieli 28:14). Kwa hiyo yeye ni fundi wa kufunika mambo na kuyafanya yaonekane ya kawaida au ya kuvutia kumbe ni mitego ya mauti.
Ulimwengu wa giza unatumia sana alama (symbolism). Ziko alama mbalimbali za kishetani ambazo zimeingizwa sehemu nyingi mno kiasi kwamba si rahisi kuzigundua maana sasa zinaonekana kama ni mambo ya kawaida tu. Zinaweza kuwa kwenye bidhaa tunazotumia kila siku kama vile mavazi, mikufu, bangili, pete, hereni, muziki, sinema, video games, nk.
Shetani hafanyi mambo yake kwa haraka. Amepanga mambo yake kwa miaka mingi na kuyaingiza polepole kiasi kwamba muda si mrefu, dunia itashuhudia mlipuko wa kazi zake za uharibifu. Hata sasa uovu umeshashika kasi kubwa; na bado unazidi kufunguka zaidi na zaidi; maana kuzimu kumeongeza tamaa.
Tambua kwamba waabudu shetani wana ajenda kubwa moja, nayo ni kufika mahali ambapo watauteka ulimwengu wote. Sasa ili kutekeleza malengo hayo, wanahitaji pia fedha. Njia mojawapo ya kupata fedha ni kuuza bidhaa mbalimbali, zikiwamo za mapambo. Lakini bidhaa hizo zinakuwa na lengo jingine zaidi ya lile la kuleta fedha. Nalo ni kuyatuma mashetani ulimwenguni kote ili kukamata akili na fahamu za watu na kuziweka mbali na Mungu wa kweli. Kwa hiyo, mara zinapotengenezwa, kabla ya kusambazwa, wanasema kuwa ‘wanazibariki.’ Na ni wazi kuwa shetani anapobariki kitu ina maana kuwa anakilaani.
Kwa hiyo, unapokuwa nazo, huo ni mlango tosha wa shetani na laana zake kuingia maishani mwako na kuanza kukuongoza katika njia yake, hata kama wewe hujui.
Zifuatazo ni baadhi tu ya alama ambazo inawezekana umeshaziona au hata kuzivaa; lakini ni alama za kishetani ambazo kimsingi zinakuwa zimepandiwa au kunuiziwa mapepo.
  • Alama ya kwanza inahusiana na kuwaingiza vijana kwenye ushetani (teenage satanism). Huo mshale uliovunjika na kukwepa tundu lililo mbele yake unamaanisha uasi na kukataa kuwa chini ya mamlaka yeyote, iwe ni wazazi au serikali. Inaitwa ni alama ya njia ya kushoto.
  • Alama ya pili ni msalaba uliogezwa juu chini na kuvunjwa. Hii ina maana ya kusema kuwa hakuna Mungu. Ni uasi dhidi ya Mungu Mwenyezi.
  • Alama ya tatu ilianzia kwenye ubudha ikiwa na maana ya bahati. Lakini Hitler aliigeuza na kuifanya alama au nembo yake na majeshi yake. Hitler alikuwa ni mwabudu shetani. Kwa hiyo, alifuata ushauri wa mwabudu shetani mwingine mkubwa kabisa (Aleister Crowley) aliyesema kwamba, ukitaka kufanikiwa katika kumwabudu shetani, basi fanya kila kitu kinyumenyume.
  • Alama ya nne, ambayo nayo ilitumiwa na Hitler (SS), ina maana ya ‘wafalme katika jeshi la shetani’ (kings in satan service).
  • Alama ya tano, ambayo huenda hata umeiona kwenye hereni za akina mama, ni alama yenye asili ya Misri ya kale. Hii ni alama ya mungu wa Misri Ra na mwanawe Horus. Kumbuka siku zote kuwa, unaposikia miungu, maana yake ni mashetani.
  • Alama ya sita inaitwa ‘tau’. Ni ya asili ya Babeli.
  • Alama ya saba ni msalaba uliogeuzwa juu chini. Ina maana ya kumkufuru Kristo kwamba alichokifanya msalabani si lolote si chochote.
  • Alama ya nane inaitwa alama ya mungu mke wa utatu (symbol of triple goddess). Kama ambavyo Wakristo tunaamini kuwa kuna Mungu mmoja katika nafsi tatu – Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, waabudu shetani nao wanaamini kuwa mungu wao mkuu ana nafsi tatu, lakini wa kwao ni mungu mke.
  • Alama ya tisa inaitwa gurudumu la uhai (wheel of life). Kila mara duara humaanisha kuwa maisha yanaendelea bila mwisho.
  • Alama ya kumi ni alama maarufu ya kishetani inayowakilisha ‘kanisa’ la ulimwenguni kote la shetani (universal church of satan). Kwa kawaida huwa na kichwa cha mbuzi katikati ambacho ni alama ya shetani (Lusifa) mwenyewe.
  • Alama ya kumi na moja ni pembetatu. Hii huwakilisha vitu vitatu ambavyo ni muhimu katika mambo ya kishetani, yaani ardhi, upepo na moto.
  • Alama ya kumi na mbili inaitwa ‘msalaba wa mkanganyiko’ (cross of confusion). Tundu lililo katikati ni dhihaka kwa Ukristo kwamba una tundu. Na mkunjo wa chini nao ni dhihaka nyingine kwamba Kristo alikufa lakini hakufufuka – aliishia huko huko kuzimu.
  • Alama ya kumi na tatu ni alama ya mungu mke Diana. Huyu ni mungu mkubwa kabisa anayeabudiwa na waabudu shetani pamoja na dini za kipagani kama tulivyoona kwenye makala mojawapo huko nyuma. Unaweza kusoma kuhusu makala hayo hapa.
  • Alama ya kumi na nne ni sawa na ya kumi na tatu. Nayo inamwakilisha mungu mke Diana kwa waabudu shetani.
  • Alama ya kumi na tano hutumika sana katika mapambo ya wanawake, hasa hereni – japo inaweza kuwa kokote kwingine. Hii ina maana ya kusema kwamba, “Ninamwamini shetani katika kupata mapato yangu.”
  • Alama ya kumi na sita ina maana ya nguvu za kijoka za kiume (male serpentine power). Ukiitazama ni mfano wa nyoka aliyejiviringa. Na nyoka ni alama muhimu kabisa ya kumwakilisha shetani.
  • Alama ya kumi na saba ina maana ya nguvu za kijoka za kike. (female serpentine power). Ni sawa na alama ya 16 hapo juu.
  • Alama ya kumi na saba ni mdudu yule ambaye hukusanya kinyesi, kwa mfano cha ng’ombe na kutengeneza kama gololi, kisha anaanza kukisukuma kwa miguu yake ya nyuma (beetle). Alama hii ina asili ya Misri na ilihusishwa na roho iliyokufa kupewa mwili upya, yaani wafu kurudi tena duniani kwa umbo jingine (re-incarnation).

Kama nilivyogusia hapo nyuma, alama hizi zinakuwa zimenuiziwa mashetani. Unapozivaa, hilo linakuwa ni agano kati yako na kuzimu. Hivyo, unamruhusu shetani kupitia mapepo hayo kuingia maishani mwako na kuyamiliki na kukuvuvia tabia fulanifulani za kishetani ambazo ni uasi na ni kinyume cha Mungu aliye hai. Na Mungu wa mbinguni huwa haingilii kati uamuzi wa mtu binafsi hata kidogo. Ndiyo maana shetani akishakufungisha agano – uwe unajua au hujui – wewe unakuwa kisheria ni wake kabisa.
Ndugu, shetani yuko kazini. Sasa na wewe usilale!!

Unawezaje kupona?
Jambo moja la busara ni kukana na kuachana na maagano hayo. Lakini sasa swali litakuwa kwamba utaacha vingapi? Maana si rahisi kuvijua vyote. Karibu kila bidhaa tunayotumia imechezewa kwa namna fulani za kishetani. Kukwepa kila kitu cha kishetani kwa asilimia mia moja ni mtihani mkubwa sana.
Cha kufurahisha ni kuwa yuko Mungu ajuaye vyote. Sisi ni wanadamu tu na ulimwengu huu ni ‘so complex’ kiasi kwamba ujanja wetu wote haufui dafu. Yesu Kristo ana hamu kubwa sana ya kumsaida kila mwanadamu aliye tayari. Lakini kama nilivyosema, huwa halazimishi mtu hata kidogo. Ni hadi wewe mwenyewe umkaribishe moyoni na maishani mwako ndipo mnaingia katika agano na Yeye. Na hapo Yeye anachukua jukumu la kusimamia maisha yako.
Lakini ukiamua kujitumaini amwenyewe au kutumainia dini, utakwama, utakwama tu. Mungu akubariki na kukufungua macho ya rohoni ili uweze kulitambua hilo.
Kama una jambo lolote, tunaweza kuwasiliana kupitia: ijuekweli77@yahoo.co.uk. Vilevile nakukaribisha kutembelea www.injiliyakweli.blogspot.com. Yesu anakupenda, anakuthamini, na anakuonea shauku ili akupe uzima wa milele.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...