Monday, March 12, 2012

MAHABA: MAMBO 5 YA KUEPUKA MARA TU UNAPOCHUMBIWA




Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wasichana juu ya matukio ya wao ‘kupotezewa’ na wapenzi wao baada ya kuchumbiwa.

Hili si jambo geni masikioni mwako. Wapo wengi tu ambao walichumbiwa na wengine kufikia hatua hadi ya kutolewa mahari lakini cha kushangaza wameachwa kwenye mataa bila sababu za wazi.

Labda niseme tu kwamba, kuna baadhi ya watu wanafanya makosa madogo sana ambayo mwishowe yanakuwa na madhara makubwa katika maisha yao ya kimapenzi.
Kimsingi msichana anapompata mwanaume mwenye nia ya dhati ya kutaka kumuoa kwanza achukulie hiyo kama bahati kwake kwani wapo wengi wanaoitamani fursa hiyo lakini mpaka leo hii wapo wapo tu.

Lakini baada ya hapo, kuna mambo kadhaa ambayo msichana anatakiwa kuwa makini nayo katika kuhakikisha uchumba wake unadumu na kufikia hatua ya kuolewa na kwenda kuanza maisha mapya.
Yapo mengi ila wiki hii nitagusia matano ambayo kwa utafiti wangu ndiyo
yamekuwa yakiwafanya wengi wakimbiwe na wachumba wao na kuachwa wakilia.

Mazoea na wanaume
Wapo ambao wamejikuta wakiachwa solemba kufuatia tabia zao za kuwa na mazoea ya kijinga na wanaume.

 Yawezekana kabla ya kuchumbiwa marafiki zako wakubwa walikuwa wanaume (Wapo wanawake wa aina hiyo). Unachotakiwa kufahamu ni kwamba hakuna mwanaume anayefurahia ukaribu wa mchumba wake kwa wanaume wengine.
Hata kama hakuna uhusiano wa kimapenzi lakini epuka sana kujichekelesha kwao, kuongozana nao, kukaa nao au hata kuwasiliana nao. Ukifanya hivyo utakuwa unamkwaza mchumba wako na inaweza kuwa moja ya sababu za kukuchenga.

Marafiki micharuko
Ukishachumbiwa, kuna marafiki zako ambao ‘automatikale’ unatakiwa kuachana nao. Nazungumzia wale micharuko ambao hawawezi kukushauri vizuri juu ya maisha yako.
Hata wale ambao wamekuwa wakikushawishi kila wikiendi muende mkajirushe, baada ya kuchumbiwa unatakiwa kujiweka mbali nao ili kumpa amani mchumba wako.

Tabia za kisichana
Ukishachumbiwa wewe si msichana tena, utakuwa ni mama mtarajiwa wa familia yako. Tabia za kisichana kama vile kuvaa mavazi yasiyo ya heshima, kukaa vijiweni kuongea mambo ya umbeya na nyinginezo kama hizo hutakiwi kuendelea kuwa nazo.

Kujifanyisha
Alichokupendea huyo mchumba wako anakijua mwenyewe, kwa maana hiyo unatakiwa kuendelea kubaki wewe kama wewe. Usijifanyishe kwa namna yoyote kama ambavyo baadhi ya wasichana wamekuwa wakifanya.

Eti umeshaolewa
Kuolewa ni mpaka pale mtakapoingia kanisani, msikitini nk na kufungishwa ndoa. Kama bado hamjafika huko, wewe bado ni mchumba tu na hata kwenye ndoa unaweza usifike.
Kwa maana hiyo hutakiwi kuhamia kwa mwanaume kama ambavyo baadhi wamekuwa wakifanya. Unachotakiwa kufahamu ni kwamba kitendo cha wewe kuchumbiwa kisha kuamua kubeba virago vyako na kwenda kuishi na mwanaume ni kuwakosea wazazi.

Msomaji wangu, yapo mengi ya kuepuka mara tu unapochumbiwa lakini haya machache yanatosha kwa leo. Jiangalie tabia zako, zile ambazo unajua wanaume wengi haziwafurahishi, jiepushe nazo ili kumjengea mchumba wako mazingira ya kukamilisha taratibu za ndoa yenu. 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...