Friday, March 9, 2012

ASKOFU MWINGINE ADAKWA NA UNGA



http://api.ning.com/files/NGHxxVgVd17fuWKh*v1l7*4NyFc2GYTkLp2o69tup7nXuo4nQgBPU2OuQ-it1jCnSiXwKCGVj6KQ*c8ylkYzAyOgRGizDiJb/IMG_0532.jpg
Madawa ya kulevya.


Aina ya magari yaliyokamatwa.

IGP Mwema.

Nabii Flora.
MORIS Charles anayejitambulisha kuwa ni askofu  wa kanisa  moja la kiroho jijini  Dar es Salaam  amedakwa  na unga  hivi karibu  katika Kijiji cha  Mchingambili,  mkoani Lindi.

Vyanzo vya  habari  vimeeleza kwamba Charles ambaye wakati  fulani hujitambulisha  kwa jina la Yusuph Mohamed Lutengwe alidakwa nyakati  za usiku Januari 11, mwaka  huu akiwa katika  gari lake aina ya Toyota Land Cruiser (namba  zinaifadhiwa ).

Taarifa hizo zimedai kwamba  kudakwa kwa mtu huyo kulifuatia habari zilizowafikia polisi mapema ambapo waliarifiwa na aina ya gari analotumia Charles kupokea  ‘unga’ au dawa za kulevya  aina ya Heroine kilo 210 zenye thamani  ya shilingi  bilioni 9.4.

MTEGO WA POLISI
Imeelezwa kwamba siku ya tukio polisi waliweka mtego baada ya kupata taarifa  ya kiongozi  huyo kuwa atakuja katika kijiji hicho na gari lake la kifahari, wakapewa namba na raia wema.

Habari zinasema ilipofika saa tano  usiku  waliliona gari kwa mbali na lilipowakaribia,   walilisimamisha lakini inadaiwa kuna mtu alichomoka ndani ya gari hilo na kutokomea gizani. 

Vyanzo hivyo vinadai kuwa jeshi la polisi halikumjua mtu huyo lakini baadaye wakaambiwa kuwa aliyekimbia ndiye huyo anayejiita Askofu Charles ambapo mtu mmoja aliyekuwa akiliendesha gari hilo alitiwa mbaroni.

Habari hizo zilieleza kwamba muda huo  huo watu aliokuwa akiwapokea wakiwa na madawa walikamatwa na polisi wa kikosi kazi. 

 Waliokamatwa  wametajwa kuwa ni pamoja na Ismail Adamu (28), Hamad Said (27), Morine Amatus (22) na Pendo Mohammed Chausi (67) ambaye ni mwenye  nyumba yalipokamatwa madawa hayo. Tayari watu hao wamepandishwa kizimbani.

Habari zinasema polisi walimfuatilia askofu huyo na kugundua kuwa anaishi  Mikocheni, jijini Dar es Salaam na wakafanikiwa kukamata mali nyingine ambazo ni magari mawili ya kifahari aina  ya Porsche Cayenne na Jeep Wrangler.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa askofu huyo amefanikiwa kuwakimbia polisi na ametorokea nje ya nchi Januari 15, mwaka huu.

Vyanzo hivyo vya  habari vimedai kwamba  kiongozi  huyo wa dini huwa ana hati mbili za kusafiria, moja anatumia  jina la Kiislam na huitumia anapotembelea nchi za Kiislam na nyingine yenye jina la Kikristo.

 Uchunguzi wetu  umebaini  kuwa hata magari anayotumia, usajili wake una utata kwani tulipofuatilia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) anayedaiwa kumiliki gari  hilo Toyota Land Cruiser lililokamatwa na polisi ni Rashida Abushir Jumanne  na  aliuziwa na huyo kiongozi Januari 16, mwaka huu.

Afisa mmoja wa TRA alisema mmiliki wa kwanza wa gari hilo ni Makame .O. Juma na kumbukumbu zao zinaonyesha  kwamba  Juni 9, 20011 aliliuza kwa kiongozi huyo anayejulikana pia kwa jina la Lutengwe.

 UTATA WA GARI
Kinachoshangaza ni kwamba Lutengwe  alikimbia nchini  Januari 15, mwaka huu, iweje auze  gari kwa Abushiri Januari 16, mwaka huu wakati  gari hilo tangu  likamatwe Januari 11,  mwaka huu bado lipo polisi hadi sasa?

 Hata  hivyo,  mwandishi wa habari  hii akiwa TRA alipata namba ya simu ya Abushiri, alipopigiwa alipokea mtu ambaye alijitambulisha kuwa yupo Morogoro na alisema kwamba anamfahamu Abushiri  ambaye anaishi Sinza jijini Dar es Salaam.

 Kijana aliyepokea simu  aliwasiliana  na Abushiri alimpa  namba ya mwandishi  na akapiga simu. Katika mahojiano alikana kwamba yeye hana gari aina ya Toyota Land Cruiser na hajawahi kulimiliki, akadai inawezekana jina lake na namba yake ya simu inatumika vibaya na wahalifu.

Abushiri  alipohojiwa zaidi na mwandishi  sababu ya simu yake kumkabidhi mtu  ambaye yuko Morogoro wakati yeye yupo Dar es Salaam alijitetea kuwa huyo ni mdogo wake, hivyo ameamua kumpa hiyo simu ili aitumie.

 Uchunguzi umebaini kwamba  hata  baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa na madawa ya kulevya, simu zao zimegundulika kuwa waliosajiliwa ni marehemu waliokufa kati ya miaka miwili na mitatu na wengine walikuwa wakiishi Morogoro.

Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alipoulizwa  kuhusu kiongozi huyo alisema kwamba hayupo tayari  kulizungumzia suala hilo kwa vile bado  linachunguzwa. 

Hata hivyo,  alikiri  kwamba  kuna mfanyabiashara mkubwa wa madawa ya kulevya aliyekimbilia nje ya chini na kwamba  magari yake yanashikiliwa na jeshi la polisi.

 VIONGOZI WA MAKANISA
Baadhi ya wachungaji wa makanisa waliozungumza na gazeti hili kufuatia kadhia hii ya dawa za kulevya nchini, wameitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara hiyo haramu.
John Said wa Kanisa la Victorious la Ubungo  External amesema kwamba sasa imefikia  muda wa serikali na jamii kwa ujumla kupiga  vita biashara hiyo na wanaokamatwa na dawa wachukuliwe hatua kali haraka. 

Nabii Flora  Peter wa Kanisa  la Huduma ya Maombezi lililopo Mbezi Beach, Dar es Salaam amesema kwamba  wanaokamatwa  na biashara hiyo  wachukuliwe  hatua mahakamani kwani  wanaumiza nguvu kazi ya taifa kutokana na ukweli kwamba vijana wengi wanaangamia na dawa hizo.
Mchungaji Timoth Mwankenja  alisema:

“Kunahitajika  jitihada  za pamoja kati ya raia na polisi ili kupambana na biashara hii haramu. Kanisa  letu  tumewahi kutoa elimu mitaani, kunahitajika ushirikiano katika vita hii. Kama kuna viongozi wa dini wanajihusisha wachukiliwe hatua kali.”

Mchungaji Alponce Mtemela wa Kanisa la Pentekoste lililopo Kawe, amesema kwamba dawa za kulevya  ni janga la taifa  kwani  wanaohusika na biashara hiyo haramu ni matajiri na wanaweza kufanya  chochote, hivyo ameiomba serikali kuchukua hatua kali.

Mwanzoni mwa mwaka jana jeshi la polisi  kitengo cha  dawa za kulevya lilimkamata  Askofu wa Kanisa la Lord Choose Chaersimatic Revived, aliyejulikana kwa jina la Chidi Okechuku.
Okechuku alikamatwa maeneo ya Mbezi Beach katika nyumba aliyopanga na alikutwa na kilo 81 za Heroine na kwa sasa kesi yake ipo mahakama kuu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...