Friday, March 30, 2012

HATIMAYE VENGU AINUKA KITANDANI...




MUNGU ni mkubwa! Hatimaye dua za Watanzania zimesikika kwa staa wa Kundi la Orijino Komedi aliyepo Hospitali ya Appolo nchini India kwa matibabu, Joseph Shamba ‘Vengu’ (pichani) ambaye ameinuka na kukaa mwenyewe kitandani...

Kwa mujibu wa chanzo makini ambaye ni mtu wake wa karibu, mbali na hatua hiyo, pia nyota huyo ameanzishiwa mazoezi ya kuongea baada ya kitambo kirefu kutomudu kuzungumza.


Chanzo hicho kiliweka wazi kuwa, jitihada kubwa zilifanywa na madaktari wa Hospitali ya Appolo ili kuhakikisha kuwa Vengu anarudi katika hali yake ya kawaida.


“Dalili zimeanza kuonekana, hivi sasa Vengu yuko katika hali nzuri, anaweza kuinuka na kukaa kitandani ila bado anapewa mazoezi ya kuongea,” kimesema chanzo hicho.


Habari zaidi zilisema kuwa kinachomfanya Vengu kushindwa kuzungumza vizuri ni kupoteza kumbukumbu kwa muda mrefu na kufanya mdomo wake kuwa mzito.


“Jumatatu (Machi 27, mwaka huu) madaktari walianza kumfanyisha mazoezi ili aweze kuzungumza vizuri, ingawaje haijulikani zoezi hilo litachukua muda gani,” kilisema chanzo hicho na kudai kuwa kama Vengu angeachwa Tanzania, asingefikia katika hatua aliyonayo sasa.


Mbali na kufanyishwa zoezi hilo la kuzungumza, pia Vengu ameanza kufanyishwa mazoezi ya viungo ili kumfanya aweze kutembea mwenyewe.


“Madaktari wameonekana kufurahishwa na hatua hiyo na wanamfanyisha mazoezi ya viungo na kumzoesha kuongea kama unavyojua ana siku nyingi hajazungumza,” kilisema.
Baada ya kupata taarifa hizo, gazeti hili lilimtafuta ndugu wa karibu wa Vengu ambaye anaishi jijini Dar lakini hakuweza kupatikana kuzungumzia hali ya staa huyo.


Hata hivyo, HOT POT ilifanikiwa kumpata mchumba wa Vengu ambaye ni Miss Kinondoni 2011/12, Stella Mbuge na kumuuliza kama ana taarifa zozote kuhusiana na mgonjwa huyo, naye alisema ameambiwa na kaka wa Vengu kuwa sasa jamaa yake yuko katika hatua ya kufanyishwa mazoezi ya kuongea.


“Kaka yake amefurahishwa na hali ya Vengu na amenihakikishia kwamba qnaendelea vizuri, kwa sasa anaweza kuinuka na kukaa mwenyewe ila wanamfanyia mazoezi aweze kuongea tena,” alisema kwa kifupi Stella.


Vengu alianza kuumwa mwaka 2009 ambapo Agosti, mwaka jana alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kabla ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi akisumbuliwa na ugonjwa unaoshambulia sehemu ya kichwa, hasa ubongo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...