Saturday, December 31, 2011

MAHABA: Kabla ya ndoa jiulize, kwa nini umempenda?


IMEBAKI siku moja kabla ya kumaliza mwaka huu na kuanza mwingine kwa ridhaa yake aliyeumba Mbingu na Dunia. Rafiki, huu ni wakati wako wa kufanya tathmini ya jumla ya mwaka huu katika maisha yako ya kimapenzi.

Wakati tunaelekea ukingoni mwa mwaka huu, ni vyema kama utajiuliza; umefanya nini kwa ajili ya penzi lako? Mpenzi wako anakufurahia au anakuona kero?
Ndoa yako inaendeleaje? Je, umekuwa mbabe na kumnyanyasa mwenzako? Una nyumba ndogo au unamheshimu mwenzi wako? Maswali haya yatakuongoza na kukuweka kwenye mstari mzuri wakati unaingia mwaka mpya.

Rafiki yangu, ni vizuri kama utamaliza mwaka ukiwa na tabasamu la nguvu na mwenzako, haina maana yoyote kununiana. Kama mmependana kweli, basi mkubali kwamba kuna kukosana na kuombana msamaha. 

Hakuna mkamilifu wa kila kitu ndugu zangu. Watu wanakosea sana, kukosea ni sehemu ya ukamilifu wa binadamu. Tafuta amani ya kudumu kwa mwenzi wako. Acha kusikiliza maneno ya watu. Wewe ndiye umemchagua, hivyo mwenye kibarua cha kumuweka sawa, anaendelea kuwa wewe mwenyewe!

Umeelewa rafiki? Hizo ndizo salamu zangu za Krismasi na Mwaka Mpya. Sasa narudi katika mada yetu ya leo, mada ambayo itabadilisha kabisa fikra zako katika sayari ya mapenzi.
Yapo mambo muhimu sana ambayo watu wamekuwa wakiyapuuza kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa. Rafiki, ukishaingia ndani ya ndoa, hakuna njia ya kutoka tena, hata ikiwepo si sahihi. Inakuchafua. Inaharibu historia ya maisha yako ya uhusiano.

Uamuzi wa ndoa si wa kujaribu. Unatakiwa kujihakikishia kwamba ni kweli umevutiwa na kila kitu cha mwenzako, kwamba utakuwa naye katika shida na raha. Hayo ndiyo mambo ya kuzingatia.
Nimeshaandika mengi kuhusu sifa za anayetakiwa kuoa au kuolewa, lakini nasogea mbele zaidi na kuangalia sababu za kumpenda mtarajiwa wako katika ndoa. 

Zipo sababu za msingi sana ambazo unatakiwa kuwa nazo kabla ya kuingia kwenye ndoa ambayo mimi hapa kwenye All About Love naiita kifungo!
Twende tukaone.

KWA NINI UJIULIZE
Lazima nifafanue hili kwanza kabla ya kuendelea. Hivi unafikiri ni kwa nini ni lazima kujiuliza sababu za kumpenda mwenzi wako?
Yes! Ni kwa lengo la kujiwekea usalama katika ndoa yako ijayo. Kujiandalia amani na pumziko la kweli. Kwenye mapenzi ya dhati pekee ndipo vinapopatikana vitu nilivyotaja hapo juu.

Kwa maneno mengine kuwa na majibu ya swali linalosomeka kwenye kichwa cha mada hii ni kujihakikishia ndoa bora. Tuendelee kujifunza. 

NI MWENZI WA NDOTO ZAKO?
Jambo kubwa kuliko yote ambalo unatakiwa kuliangalia kwa jicho la tatu ni kama mwenzi huyo ni wa ndoto zako. Je, yukoje? Rafiki, siku zote kabla ya kuamua kufanya chochote lazima ujiulize kama ndicho ulichokuwa ukikifikiria.
Hata kwa upande wa mwenzi wako, lazima ujiridhishe, ni kweli ni yule uliyekuwa unamtarajia? Ana sifa unazohitaji? Acha tabia ya kujifariji kwamba utampenda taratibu ndani ya ndoa, hicho kitu hakipo.

Hakuna kujifunza kupenda katika ndoa, lazima ujihakikishie mwenyewe kuwa mwenzi wako ni yule mwenye sifa ulizokuwa ukizitarajia. Hili ni la msingi, maana unaweza kuwa naye siku mbili, ukatamani mwingine nje, kwa  nini? Kwa sababu si yule mwenye sifa ulizotarajia.
 
NI SURA, UMBILE?
Kuna baadhi ya watu utawasikia wakisema: “Mpenzi wangu ananivutia sana, yaani ni mzuri sana. Najua hata nikitoka naye, marafiki zangu watanisifia kwa kuchagua vizuri...”
Hizi ni fikra potofu ndugu zangu. Mapenzi ya kweli hayapo kwenye sura wala umbile la mtu. Vipo vigezo vya muhimu kabisa vya kuzingatia tofauti na uzuri wa sura.

Sura hubadilika ndugu zangu, binadamu wanazeeka, kuna kuugua na matatizo mengine ambayo yanaweza kubadilisha mwonekano ambao ulikuvutia. Je, yakitokea ndiyo utakuwa mwisho wa kumpenda?
Kama leo hii unamuoa kwa sababu umevutiwa na matiti yake madogo, akishazaa na kunyonyesha kisha yakaanguka, ndiyo mwisho wa kumpenda? Umempendea ngozi yake nyororo, akipata ‘aleji’ ya mafuta, ngozi ikaharibika na kuwa na mabakamabaka utakuwa mwisho wenu?

Wewe mwenye mpango wa kuolewa na mwanaume mwenye kigezo cha kifua cha kimapenzi, kesho akifutuka na kuwa na kitambi utamuacha? Rafiki yangu, kiukweli ni kwamba kigezo cha uzuri wa sura na umbile si sahihi kabisa katika kuchagua mwenzi. Vipo vitu vingine muhimu zaidi vya kuangalia.

Kama ulikuwa unaishi katika dunia ya fikra hizo, hama ndugu yangu. Wiki ijayo nitakupa sifa bora zaidi za kuzingatia kabla ya kuamua kufunga ndoa na mwenzi wako. Bila shaka utaanza mwaka vizuri, maana hata fikra zako zitakuwa mpya kabisa.
Je, unatarajia kuoa hivi karibuni? Wiki ijayo nitakufungua kuhusu sifa anazotakiwa kuwa nazo huyo mwenzi wako. Si ya kukosa rafiki.
HERI YA MWAKA MPYA!

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...