Tuesday, December 6, 2011

Duuuuh... Kidume chafyeka msosi wa shilingi milioni 81



Paul Mason.
PAUL Mason, 50, yupo kwenye mateso makali. Mbali na kwamba mwili wake ulimpa umaarufu mkubwa na kutangazwa kuwa mwanaume mnene kuliko wote duniani hadi kuandikwa kwenye kitabu cha dunia cha kumbukumbu, Guinness, hivi sasa anateseka.

Mason, yupo kwenye maumivu makali, kwani umbo lake limemsababisha ugonjwa wa moyo pamoja na hali ya kushindwa kutimiza majukumu kadhaa kutokana na uzito mkubwa alionao.

Wakati Mason, anatangazwa kuwa mwanaume mnene kuliko wote duniani, alikuwa na uzito wa Kg 381. Kipindi hicho alikuwa hawezi kufanya chochote, zaidi ya hapo alikuwa anakabiliwa na tishio la kupoteza maisha.

Uzito huo, alikuwa nao mpaka miaka miwili iliyopita, kabla ya kufanyiwa upasuaji wa kupunguza mafuta na nyama. Baada ya kufanyiwa oparesheni hiyo, sasa hivi amefikisha uzito wa Kg 190, ikiwa chini ya nusu ya uzito wake wa awali.

Inabainishwa kwamba mwaka huu kabla hajafanyiwa upasuaji, tayari uzito wake ulishafikia Kg 445, hali ambayo madaktari wameielezea kuwa ni mbaya zaidi na kwamba Mason alikuwa anacheza na kifo.

Pamoja na kupungua uzito na unene, Mason, raia wa Uingereza, bado anaishi na tatizo kubwa, kwani ngozi yake imetepeta, hivyo kumfanya apoteze mvuto.

Kutokana na hali hiyo, Mason anaishi kwa unyonge, kwani hali ya mwili wake kwa sasa inaonesha kuwa amepungua unene kwa kiasi kikubwa lakini ngozi inabaki inasumbua kwa jinsi inavyolegea.

Hata hivyo, madaktari wamemuahidi kumfanyia upasuaji wa kuondoa ngozi isiyohitajika ili ibaki ile ambayo itashikana na mwili wake. Oparesheni hiyo inaitwa cosmetic surgery.

Pamoja na ahadi hiyo, madaktari wamemtaka Mason kudhibiti kwanza uzito wake, kwani ni hatari kwa sasa kumfanyia cosmetic surgery kwa sababu anaweza kuongezeka baadaye, hivyo kuibua tatizo kubwa zaidi.

Changamoto siyo masharti ya madaktari, kwani hata fedha zinazohitajika kwa ajili ya oparesheni hiyo ipo juu mno. Anahitaji shilingi milioni 16 (pauni 6000) kugharamia upasuaji huo.

Hapo kabla, Mason, alikuwa akitumia fedha nyingi kwa matumizi ya chakula na yeye mwenyewe anakiri kuwa alikuwa anateketeza mpaka shilingi milioni 81 (pauni 30,000) kwa mwaka, kwa ajili ya kununua chakula.

Madaktari wanasema kuwa unene wa Mason ni wa kujiendekeza, kwani kabla ya kufanyiwa upasuaji wa kupunguza mwili, alikuwa anaweza kula chakula chenye kalori 20,000 ambazo ni mara 10 zaidi ya kiwango kinachohitajika kwenye mwili wa mwanaume wa kawaida.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...