Saturday, February 18, 2012

UTAJIRI WA MWINGIRA WALIGAWA KANISA: Anamiliki Jumba la kifahari la zaidi ya BILLION 1..."



MADAI na gumzo kwamba baadhi ya viongozi wa dini wanajilimbikizia mali yameibuka upya wiki iliyopita baada ya baadhi ya waumini wa Kanisa la Efatha jijini Dar es Salaam kugundua kuwa  Mtume na Nabii wao, Josephat Mwingira  ameiambia Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi kuwa  ‘amefyatua’ jumba la kifahari lenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja katika kiwanja kilichopo Kawe Beach, wilayani Kinondoni.

Waumini hao wamekuja juu baada ya Mwingira (pichani) kudai mahakamani kuwa jumba hilo amelijenga kwa fedha zaidi ya shilingi bilioni moja lipo kwenye eneo lake ambalo ni kiwanja namba 548 (b)  Kawe na alipewa na Wakili Evarist Hubert Mbuya aliyeibuka mahakamani hapo na kudai kuwa eneo hilo ni lake kihalali. 

Wakizungumza, baadhi ya waumini walioomba majina yao kuhifadhiwa walidai kuwa Mwingira amejilimbikizia mali kwa sababu jumba lenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja ni la kifahari mno ukilinganisha na hali ya uchumi ya waumini wake wengi.

“Sadaka zingetumika kufanya shughuli za kijamii zaidi. Hatuoni sababu ya kiongozi wetu kujenga jengo la kifahari kiasi hicho wakati kuna mipango mingi ya maendeleo ya kanisa inahitaji fedha,” alisema muumini mmoja wa kike ambaye alionesha waziwazi kuwa upande mwingine wa imani baada ya kudai kuwa waumini wananyonywa.

Hata hivyo, muumini mwingine wa kiume alisema alishtushwa sana aliposoma kwenye gazeti kuwa Mwingira aliiambia mahakama kuwa ana jengo lenye thamani ya zaidi ya shilingi 1,000,000,000.
“Hayo ni mambo ya kidunia, anatufundisha tusiwe na tamaa ya kuwa na vitu kama hivyo na badala yake tuwekeze mbinguni, iweje anakuwa na jengo lenye thamani kubwa kiasi hicho?” alihoji muumini huyo.

Mwandishi wetu alimpigia simu Mwingira ili aweze kufafanua kuhusu madai ya waumini wake, awali mtu aliyepokea alisikiliza kile alichoulizwa na mwana habari huyo, akajibu kuwa yeye siyo kisha akakata simu.

Hoja ya kiongozi huyo kujenga jumba kubwa la kifahari aliibua mwenyewe wakati wa kesi yake na Wakili Mbuya ambapo kupitia kampuni ya uwakili ya Ligal Link Attorney, amedai kujenga jengo hilo la thamani kwenye kiwanja hicho hali iliyofanya waandishi wetu kwenda na kuliona (Angalia picha ukurasa wa mbele).
Nabii Josephat Mwingira.

Mwingira kupitia kampuni hiyo  ya Mawakili ya Ligal Link Attorneys alifungua kesi namba 226 /2010, Agosti 23, mwaka jana katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi akitaka itoe amri ya utekelezaji wa kile alichokiita mkataba wa ugawaji wa eneo.

Katika madai hayo, Mwingira anaomba Mbuya alipe gharama  ya kesi na mambo yote ambayo mahakama itaona inafaa.
Hata hivyo, Mbuya naye kupitia kwa wakili wake, Michael Ngalo ameiambia mahakama hiyo kuwa eneo hilo alilojenga Mwingira ni lake na alishaghairi kulipa kanisa.

Ameiomba mahakama iamuru ‘mjengo’ huo ubomolewe kwa kuwa haukujengwa kihalali na imuondoe na Mwingira aamuriwe kulipa gharama zote za zoezi hilo.
Mbuya amekwenda mbali zaidi kwa kuiambia mahakama kuwa gharama za kubomoa mjengo huo ni shilingi za Kitanzania milioni 56.

Alisisitiza hoja yake kuwa eneo hilo ni lake kwa kutoa nakala za nyaraka za serikali kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi yenye kumbukumbu namba LD/184624/17 ya Juni 17, 2010  na nyingine ya Machi 11, 2011 yenye kumbukumbu namba LD/184624/24.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...