Saturday, February 11, 2012

Mwingira atuhumiwa kubaka mke wa mtu...



TUHUMA nzito ya ubakaji imemwangukia Nabii na Mtume wa Kanisa la Efatha la Jijini Dar es Salaam, Josephat Elias Mwingira (pichani) ambapo Wakili Eliya Hubert Mbuya amedai katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kuwa, kati ya mwaka 2005 na 2009, mtumishi huyo wa Mungu alimbaka mkewe...
KESI YA MSINGI
Kesi ya msingi yenye namba 226/2010 ilifunguliwa mwaka jana na Nabii Mwingira ikimtaka Wakili Mbuya ambaye ni mlalamikiwa awe amefika mahakamani hapo Novemba 10, 2011 mbele ya Jaji Nchimbi ili ajibu madai ya  mlalamikaji anayemshitaki kwa suala lenye utata wa umiliki wa kiwanja nambari 548 (a) kilichopo Kawe, Dar es Salaam.
Mwingira anamlalamikia Mbuya kwa kuvunja mkataba wa kumpa sehemu ya kiwanja hicho ambacho tayari nabii huyo amejenga nyumba na kuboresha miundombinu kwa thamani ya shilingi 1,000,000,000.
Katika majibu ya Mbuya yayowasilishwa mahakamani hapo na Kampuni ya Mawakili ya Ngalo (Ngalo and Advocates), Mbuya amedai kuwa mke wake alibakwa na Mwingira, hivyo akaghairi kutoa kipande cha ardhi kwa mlalamikaji kama alivyofanya awali.
MWANZO WA SAFARI
Akieleza kwa urefu sakata hilo, Wakili Ngalo alidai kuwa,  Julai 2003, Mbuya akiwa na mkewe Betha alihudhuria semina iliyoendeshwa na  Mwingira katika Kanisa la Efatha, Mwenge Jijini Dar es Salaam ambapo kutokana na mahubiri yake, waliamua kuokoka na kuwa wanachama wa kanisa hilo.
Wakili Ngalo akaongeza kuwa, Mbuya alidai kwamba Oktoba 2003, katika kanisa hilohilo, iliendeshwa semina nyingine iliyokuwa chini ya Ibrahim Mlay na mlalamikiwa (Mbuya) alichangia basi dogo aina ya Toyota Coaster.
Alisema kuwa baada ya muda Mlay aliendesha semina tena katika kanisa hilo ambapo Mbuya na mkewe walihudhuria na walichangia kipande cha ardhi kilichopo Ploti Namba 548, Kawe Beach.
Sehemu ya majibu hayo ya kinga ikasema kuwa mwaka 2005, Mwingira alimtaka mlalamikiwa kutafuta mnunuzi wa kiwanja hicho ambapo fedha ambazo zingepatikana, zingejenga makanisa ya Efatha sehemu nyingine.
Ikadaiwa kuwa, alijitokeza mnunuzi aliyekuwa tayari kulipa shilingi 176,000,000, mwingine akiwa tayari kwa kulipa shilingi 450,000,000 kwa lengo la kujenga hoteli.
Ikasemekana kwamba, Novemba 2006, mlalamikaji alimwambia mlalamikiwa kuwa Mungu alimwonesha maono yakimtaka mlalamikiwa asikiuze kiwanja hicho, bali amkabidhi mlalamikaji hivyo amwandalie ‘dokumenti’ za makabidhiano ya  kiwanja hicho, naye akatii.
DALILI ZA UBAKAJI
Akizungumzia madai ya mkewe kubakwa, Wakili Ngalo alisema kuwa mwaka 2009, mke wa Mbuya alitubu kwa mumewe kwamba siku moja mwanaume huyo akiwa kazini, yeye alizini na mtumishi huyo wa Mungu kwenye ndani ya nyumba yao.
Sehemu ya waraka huo ikasema kuwa, mke huyo aliamua kuchukua uamuzi huo baada ya  kupata ugonjwa mbaya (tunausitiri) uliomsumbua kwa muda wa miaka mitatu ambapo katika kumwomba Mungu, aliisikia sauti ikimwambia ili apone lazima atubu dhambi ya uzinzi kwa mumewe.
MUME NA MKEWE WANAMKABILI MWANGIRA
Baada ya kusikia hayo, mlalamikiwa akiwa na mkewe walikwenda kumkabili mlalamikaji ofisini kwake  ambapo walimkuta akiwa na mkewe.
Kwa mujibu wa wakili huyo, mke wa mlalamikiwa aliweka wazi uhusiano wake wa mapenzi na mtumishi huyo wa Mungu ambapo mke wa mlalamikaji naye akasema amewahi kusikia tetesi za kuwepo kwa uhusiano huo.
 “Mke wa mlalamikiwa alimuomba radhi mke wa mlalamikaji ambapo alimsamehe lakini mlalamikaji hakujibu chochote,” ilisema sehemu ya nyaraka ya Wakili Ngalo iliyopo mahakamani.
NINI KIINI CHA TATIZO?
Aidha, Mbuya alinukuliwa na wakili wake akidai kwamba kwa sababu walikuwa wakihudhuria hafla mbalimbali za maombi kanisani  hapo na kutoa michango hiyo ndiyo ilikuwa kivutio cha Mwingira kumtembelea nyumbani kwake mara kwa mara na kutenda hayo.
KWANINI MUME ALIGHAIRI KUTOA KIWANJA?
Nyaraka hizo zimesema kuwa kutokana na Mbuya kugundua uhusiano huo usiofaa ambao mke wa mlalamikaji alikiri kuusikia, aliamua kufuta uamuzi wake wa awali wa kugawa ardhi aliyokusudia kumpa Mwingira na akaifahamisha Wizara ya Ardhi, mlalamikaji pamoja na mkewe (Mbuya).
Wakili Ngalo amesema Mbuya aliiomba mahakama hiyo kuitupilia mbali kesi hiyo na mlalamikaji aamuriwe kulipa fidia.
ANACHOTAKA NABII MWINGIRA
Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali za kimahakama (nakala tunazo), Mwingira alifungua kesi Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi Agosti 23, 2010 akiitaka itoe amri ya utekelezwaji wa kile alichokiita ‘mkataba wa ugawaji eneo.’

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...